Tuesday, November 20, 2018

WAKALA WA MAJENGO TANZANIA YATAKIWA KUMALIZA KWA WAKATI UJENZI KITUO CHA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA



Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akitazama ramani ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kikazi kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akitoa maelekezo ya kuboresha ujenzi wa Kituo cha kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakati wa ziara ya kikazi kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akizungumza na Wataalam wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Kanda ya Ziwa wakati wa ziara ya kikazi kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.




Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imetakiwa kukamilisha kwa wakati mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa cha Kanda ya Ziwa uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Wito huo, umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko wakati wa ziara ya kikazi kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.

Bi. Mwaluko ameitaka Wakala hiyo kuhakikisha inakamilisha ujenzi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kukusanya, kuchambua, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma zilizopo kanda ya Ziwa kwa lengo la kulinda urithi andishi na historia ya Taifa letu.

Bi. Mwaluko ameielekeza Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuzungumza na Wakala wa Majengo Tanzania na kukubaliana tarehe rasmi ambayo jengo litakuwa limekamilika ili taarifa hiyo itolewe kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyopanga kutembelea kituo hicho hivi karibuni kwa lengo la kujiridhisha na ujenzi uliofanyika.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin M. Msiangi amesema, kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa ni kitovu cha mafunzo ya namna bora ya utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa katika kanda ya Ziwa kwa watumishi wa umma na wanafunzi wa vyuo wanaosoma masuala ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoani Mwanza, Bi. Doreen Swai amesema ili kukamilisha ujenzi kwa ubora unaotakiwa, TBA inategemea kukabidhi kituo hicho mwakani mwezi Februari, 2019.

Serikali katika bajeti ya fedha mwaka 2018/19, imeiidhinishia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jumla ya shilingi 2, 000, 000,000/= za kitanzania ili kukamilisha ujenzi wa kituo kitakachokuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha (archival boxes) 15,000 ya kumbukumbu tuli yenye uwezo wa kubeba jumla ya majalada 150, 000 kwa wakati mmoja. Aidha, kituo kitatumika kama kituo mbadala cha Mifumo ya TEHAMA ya kuhifadhi kumbukumbu iliyopo katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma.

No comments: