Wednesday, November 14, 2018

WAFANYAKAZI WATANO NEMC WAPATA DHAMANA KESI YA UHUJUMU UCHUMI

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

WAFANYAKAZI watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wamefanikiwa kupata dhamana baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi kuridhia wapate dhamana na kuwapangia masharti ya dhamana.

Hatua hiyo imekuja baada ya washtakiwa kupitia mawakili wao kupeleka maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa washtakiwa wameshtakiwa chini ya sheria ya Uhujumu Uchumi ambapo kesi hizo zinasikilizwa Mahakama Kuu.

Washtakiwa waliopata dhamana ni Ofisa wa Mazingira NEMC, Deusdith Katwale(38) na Mtaalam wa IT NEMC, Luciana Lawi(33) wote wakazi wa Ubungo Msewe, Katibu Muhasi wa NEMC (Sekretari), Edna Lutanjuka (51) Mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, Msaidizi wa ofisa Mwaruka Mwaruka (42) na Ofisa mazingira Nemc, Lilian Laizer (27) wote wakazi wa Ukonga Mombasa.

Washitakiwa hao Octoba31, Mwaka huu walisomewa mashtaka sita ya uhujumu uchumi likiwamo la kughushi saini ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa Mazingira.

Akiwasomea masharti sita ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama Kuu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando amewataka kila mshtakiwa kuweka fedha benki kiasi cha Sh. Milioni 13.3 au kuwasilisha mahakamani hapo hati ya mali isiyoamisha yenye thamani hiyo ya fedha.

Pia kila mshtakiwa ametakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika mmoja wapo awe mwajiliwa wa Serikali wenye vitambulisho vya Taifa watakaosaini bodi ya Sh. Milioni 2.5.Aidha, washtakiwa hao wametakiwa kutotoka nje ya Dar es Salaam pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani hapo. 

Washtakiwa hao pia wametakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kama watakavyopangiwa.Ni washtakiwa watano ndio waliofanikiwa kutimiza masharti na wako nje kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. 

Mapema, Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Jenipher Massue ulidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa upelelezi bado haujakamilika, pia wameomba tarehe ya karibu ya kutajwa kwa kesi hiyo kwani wanania ya kumuongeza mshtakiwa mwingine. 

Baada ya maelekezo hayo, Wakili wa Utetezi Bernard Mbakileki alidai Mahakama Kuu kitengo cha Uhujumu Uchumi imeridhia mshtakiwa wa Pili hadi wa sita kupewa dhamana hivyo wanaiomba Mahakama ya Kisutu iweze kiruhusu utekelezwaji wa amri hiyo. 

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo la kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh.Milioni 160.

No comments: