Wednesday, November 14, 2018

KAMANDA MUSLIM SASA KUWANYAKUA MADEREVA WA SERIKALI WASIOFUATA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI

*Asema inasikitisha watumishi wa umma kupoteza maisha kwa ajali
*Awataka waache kukimbia mwendo kasi, kupita magari bila uangalifu

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Fortunas Muslimu ametoa onyo kali kwa madereva wa Serikali ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali zinazokatiza maisha watumishi wa umma ambao Serikali imetumia fedha nyingi kuwaandaa huku akisisitiza atakayevunja sheria atamnyakua tu na sheria kuchukua mkondo wake.

Amesisitiza umuhimu kwa madereva wote nchini wakiwamo hao wa Serikali kuhakikisha wanatii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinaepuka iwapo sheria zitazingatiwa. Kamanda Muslim ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na Michuzi Blog iliyotaka kupata kauli yake kutokana na kuibuka kwa ajali za barabarani ambazo nyingi zinahusisha magari ya Serikali ambapo amesema jambo la msingi ni kuhakikisha madereva wanatii sheria zilizopo.

"Tumedhamiria kuchukua hatua kwa madereva wote wa Serikali wanaoshindwa kuheshimu sheria za usalama barabarani na matokeo yake kusababisha ajali ambazo kimsingi zinaepukika.Madereva wote wa Serikali wote wamekwenda chuo na wanajua vema sheria za usalama barabarani.Hivyo hizi ajali ambazo zinatokea kwangu naona ni maksudi na wala hakuna sababu nyingine zozote zenye mashiko.

"Wakifuata sheria hizi ajali hazitatokea , mbona wanaweza kufunga mkanda wakiwa kwenye magari kwanini wanashindwa kuheshimu sheria nyingine ambazo zitawafanya wawe salama wakati wote wa safari.Wengine wanakwenda mwendo kasi na kupita magari mengine bila kuangalia usalama na matokeo yake wanasababisha ajali na kuua watumishi wa umma na kuharibu magari ya Serikali ambayo nayo yananunuliwa kwa gharama kubwa,"amesema Kamanda Muslim.

Amesema kikosi cha usalama barabarani kitaendelea kuchukua hatua kwa madereva wote wasiotii sheria za barabarani na kwamba ataendelea kuwanyakua kadri watakavyokosea."Nitaendelea na kuwanyakua tu na kuwatembezea moto wa sheria.Hatuwezi kukubali watumishi waendelee kupoteza maisha kwasababu ya kutozingatiwa sheria za barabarani.

"Wapo madereva wanasema wanakwenda mwendo kasi kwasababu wanaambiwa na viongozi wanaowaendesha, ujumbe wangu kwao wao ndio washauri na pale wanapolazimishwa jambo ambalo wanajua lina madhara. Watumie taaluma yao ya udereva wakati wa kuendesha na wala hakuna sababu ya kufuata kila agizo ambalo unapewa huku ukijua lina madhara yake kwani sheria haitaangalia nani katoa maagizo zaidi ya kushughulika na dereva aliyetenda kosa,"amesema Kamanda Muslimu.

Wakati huo huo amesema dereva wa gari ya Serikali ambaye amemnyakua jana atamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa pamoja na kumpeleka maakamani huku pia akielezea hatua ambazo kikosi hicho kinachukua ili kukomesha ajali za barabarani ambapo pia amezunumzia madereva wa maroli ambao magari yao yakiharibia barabarani wanaweka matawi ya miti."Wapo wanaosema watapata tabaabu sana, wengine wanasema fyekeleaa mbali lakini kwangu mimi ni Kunyakua tu na kutembeza moto wa sheria dhidi ya wakiukaji wa sheria za usalama barabarani,"amesisitiza.

No comments: