Wednesday, November 14, 2018

Maelfu wajitokeza kuchunguza magonjwa yasioambukiza Muhimbili-Mloganzila


Na Neema Edwin

Maelfu ya watu wamejitokeza kupima afya zao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kisukari duniani, huku Mkurungezi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Lawrence Museru akiwataka Watanzania kujenga tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kubaini kama wana tatizo la kisukari au matatizo mengine ya kiafya.

Katika maadhimisho hayo hadi kufikia saa 7:30 mchana leo, watu 1,150 wamejitokeza kufanya uchunguzi wa macho, uchunguzi wa afya ya kinywa na meno, uchunguzi wa magonjwa ya kisukari, homoni pamoja na shinikizo la damu.  

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Prof. Museru amesema kati ya watu wazima 100 takribani watu 9 wana ugonjwa wa kisukari na kati ya watu wazima 3 mmoja ana shinikizo la damu. “Tatizo ni kubwa kwani takwimu zinaonyesha kliniki ya kisukari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ina wagonjwa zaidi ya 6000 wanaoudhuria kwa mwaka,” amesema Prof. Museru.

Prof. Museru amesema kwamba moja ya vyanzo vinavyochangia kuongezeka kwa magonjwa yasioambukiza ikiwamo kisukari na presha ni ulaji usiofaa kama kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa, kula mafuta na chumvi zaidi ya mwili, kutokula matunda na mbogamboga kiasi cha kutosha na kula nafaka zilizokobolewa.

Mkurugenzi huyo amesema matumizi ya pombe kupita kiasi, tumbaku na dawa za kulevya, kutofanya mazoezi na msongo wa mawazo pia yanachangia kuongezeka kwa magonjwa yasioambukiza.

Akizungumzia madhara ya kisukari, Prof. Museru amesema ugonjwa huo unasababisha kuharibika kwa macho, figo, moyo na mishipa ya damu.
“Kwa mfano, mtu anaweza kuishi miaka mingi na shinikizo kubwa la damu bila kubainika kama ana dalili zozote hadi pale anapopata kiharusi, moyo au figo unaposhindwa kufanya kazi,” amesema Prof. Museru.

Mkurugenzi huyo amewashauri watu kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa lengo la kugundua magonjwa hayo mapema ili kuepuka matumizi ya mabilioni ya fedha za kudhibiti magonjwa yasioambukiza.Amesema inakadiriwa ugonjwa kisukari pekee umeathiri maisha ya watu takribani milioni 425 duniani kote hadi mwaka 2017, huku asilimia 80 ya idadi ya watu wakiishi kwenye nchi za kipato cha chini ikiwamo Tanzania.

 “Ukubwa wa tatizo la kisukari duniani kote linaendelea kuwa tishio la uhai wa watu mwaka hadi mwaka kwani wagonjwa wa kisukari wanaongezeka kwa kasi sana ukilinganisha na ongezeko la idadi ya watu duniani,”amesema Prof. Museru.

Amefafanua kuwa magonjwa mengine yasioambukiza kama magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, figo, magonjwa ya mfumo ya hewa na kansa yanazidi kuongezeka kwa kasi na kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani kote.
Siku ya kisukari duniani huadhimishwa tarehe 14 Novemba kila mwaka ambapo Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila imeadhimisha siku hii kwa kutoa huduma bure mbalimbali za uchunguzi kwa siku tano kuanzia Novemba 12-16, 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, Prof. Lawrence Museru akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kisukari ambayo huadhimishwa Novemba 14, kila mwaka. Maadhimisho hayo yanafanyika katika hospitali hiyo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
 Mmoja wa wananchi aliyejitokeza kuchangia damu katika maadhimisho ya siku ya kisukari duniani hospitalini hapo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Museru akionyesha umuhimu wa wananchi kuchunguza afya zao kwenye maadhimisho hayo.
Wananchi wakiendelea kupatiwa huduma ya uchunguzi leo.


 Wananchi wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila wakati akizungumza nao kwenye maadhimisho hayo.
 Mmoja wa wananchi akipata huduma katika hospitali hiyo leo.
 Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma za uchunguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila wakisubiri kupatiwa huduma hiyo leo.
 Pichani ni Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (katikati), Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila, Sufiani Baruani (kulia) na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila Sr. Redemptha Matindi.

No comments: