Wednesday, November 14, 2018

TAKUKURU YAWASHIKILIA VIGOGO WATANO MAKETE KWA TUHUMA ZA UPOTEVU WA FEDHA MILIONI 500/- , YUMO MKURUGENZI WA HALMASHAURI

Na Amiri Kilagalila ,Njombe 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Njombe inawashikilia watumishi watano wa Halmashauri ya Makete akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Francis Namaumbo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha zaidi ya Sh.milioni 500.

Akizungumza leo Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Njombe Chalse Nakembetwa amesema kuwa upotevu wa fedha hizo umetoka katika makusanyo ya Julaihadi Semptemba ambapo yalikuwa ni zaidi ya Sh.bilioni moja huku taarifa zikionesha kuwa zaidi ya Sh.milioni 500 zimepotea na wahusika wakishindwa kutoa maelezo ya kutosha baada ya kuhojiwa na taasisi hiyo.

Amesema katika uchunguzi Takukuru imebaini wizi na ufisadi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Makete zaidi ya Sh.milioni 5.69 sawa na asilimia 46 zilizokusanywa kwa utaratibu wa POS kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2018 hazijulikani zilipo.

Amefafanua makusanyo hayo yalikuwa ni sehemu ya Sh.1,245,632,633 yaliyokusanywa katika kipindi tajwa .Kutokana na uchunguzi huo Takukuru Mkoa wa Njombe inawashikiria baadhi viongozi na watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Makete kwa ajili ya uchunguzi.

Baadhi ya viongozi wanaoshikiliwa kutokana na tuhuma hizo za upotevu wa fedha ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Makete Francis Namaumbo,Mweka Hazina Edward Mdagachule,Ofisa Biashara Wilaya ya Makete Edonia Mahenge,Mtaalam wa Tehama Wilayani humo Goden Mbilinyi na Mhasibu wa mapato wa Wilaya Isaya Madock.

Pia imeelezwa watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa na kwamba katika hatua nyingine Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Njombe Cherls Nakembetwa amesema kuwa watuhumiwa wote hapo juu wanashikiliwa kwa uchunguzi kwa makosa ya matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri K/F 22 cha PCCA/2007, Ubadhirifu na ufujaji K/F 28 cha PCCA/2007, Wizi chini ya kifungu cha 273 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (penal code) na kujipatia manufaa K/F 23 cha PCCA/2007

Aidha Takukuru kama chombo cha uchunguzi na mashtaka kinategemea kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuhujumu mapato ya serikali mara uchunguzi utakapokamilika ikiwa ni pamoja na kufungua kesi mahakamani.

No comments: