Thursday, November 1, 2018

STAA WA ZAMANI WA ARSENAL ROBERT PIRES AWASILI NCHINI KWA MUALIKO WA BARCLAYS

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

MCHEZAJI maarufu wa zamani wa Timu ya Arsenal ya Uingereza Robert 
Pires amewasili nchini Tanzania leo Novemba 1,2018 kwa mwaliko maalum wa Benki ya Barclays kwa lengo la kushiriki uzinduzi wa Kampeni ya benki hiyo inayoitwa Superfans.

Pires akiwa nchini kwenye kampeni hiyo ambayo itampa nafasi mteja mwenye akaunti ya biashara au anayetumia kadi kufanya manunuzi mara nyingi kipindi cha kampeni fursa ya kujishindia bahati nasibu ya safari ya Uingereza kushuhudia mechi moja mubashara ya ligi Kuu ya Uingereza.

Akizungumza leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya Pires kutua nchini, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Barclays Tanzania Aron Luhanga amesema ujio wa mchezaji huo ni maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni hiyo na atakuwa nchini kwa siku tatu.

"Gwiji wa zamani wa timu ya Arsenal Robert Pires amekuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuzindua kampeni ya wateja iitwayo Superfans inayomwezesha mteja anayemiliki akaunti ya biashara au anayetumia kadi ya Barclays kufanya manunuzi mara nyingi kuzawadiwa safari ya Uingereza kushuhudia  mechi mubashara ya Ligi Kuu ya Uingereza,"amesema.

Ameongeza kwa siku ya kesho mchezaji huyo atakuwa Mliman City jijini 
Dar es Salaam ambako ataungana na mashabiki halisi wa soka na tutakuwa na Club House ambayo mara nyingi hujumuisha watu maarufu kwenye soka kama ilivyo kwenye Ligi ya Uingereza.

Amesema akiwa hapo Pires atapata nafasia ya kutia saini yake kwenye 
mpira, jezi na vitu vingine kutoka kwa mashabiki wa soka huku akielezea kuwa benki yao ndio mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya nchini Uingereza na Pires wamekuwa wakimtumia kwenye shughuli nyingi na kwamba kuna wachezaji wengine wengi ambao wanatumia na Barclays.

Ameongeza pia Pires atashuhudia mechi ya wachezaji wa benki ya Barclays ambayo itachezwa kwenye viwanja vya Mgulani jijini Dar e Salaam huku akitoa mwito kwa Watanzania kuhakikisha ujio wa mchezaji huyo unakuwa sehemu ya kuhamasisha mchezo wa soka nchini.

Kwa upande wake Pires amesema amefurahi kuja nchini Tanzania kwani hiyo ni mara yake ya kwanza huku akionesha kufurashwa na aina ya mapokezi aliyoyapata kutoka kwa Watanzania.Akiwa uwanjani hapo baada ya kuwasili alipata nafasi ya kushuhudia ngoma za asili zilizonogeshwa na mchezo wa sarakasi.

No comments: