Thursday, November 1, 2018

RAIS MAGUFULI ASEMA SERIKALI YAKE INAYO FEDHA ZA KUTOSHA

*Aamua kugusia alivyobana mianya ya upotevu wa fedha 
*Aeleza namna Serikali inavyotekeleza miradi bila wafadhili

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

RAIS Dk.John Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa hivi sasa Serikali yake inayo fedha za kutosha ambayo inaweza kuiendesha nchi kwa miezi sita kwa kununua bidhaa bila tatizo lolote huku akieleza kuwa fedha zilizopo ndio maana wakati mwingine zinasababisha kiburi 
ambacho wakubwa hawapendi.

Dk.Magufuli amesema hayo leo kwenye Kongamano la uchumi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo pamoja na kuelezea mambo mbalimbali ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano amezungumzia namna ambavyo wamefanikiwa kudhibiti upotevu wa fedha.

"Tuna pesa za kufanya mambo yetu na unapokuwa na pesa wakati mwingine unakuwa na jeuri ambayo hata hivyo haipendwi na wakubwa.Ukweli ni kwamba tumeziba mirija ya kuvujisha fedha na ndio maana hata makusanyo yameongezeka,"amesema.Amefafanua katika jitihada za kuziba upotevu wa fedha Serikali yake iliamua kuweka mkakati wa kuondoa watumishi hewa ambapo kwa mwezi Serikali ilikuwa inalipa Sh.bilioni 423 kwa mwaka kwa watu ambao hawapo."Kwa mwezi tulikuwa tunalipa mshahara wa Sh.bilioni 777 na bada ya uhakiki mishara inayolipwa kwa mwezi ni Sh.bilioni 251 kwa mwezi,"amesema Rais Magufuli.

Amefafanua kwa hatua hizo ambazo zimechukuliwa aliyekuwa ananuifaka hawezi kufurahia huku akitoa mfano kuna mfanyakazi .alikuwa na watumishi wake hewa 17 na ikifika mwisho wa mwezi 
anakwenda kuchukua fedha kwenye akaunti ambazo aliziweka.Rais Dk.Magufuli amesema wakati wakipambana na watumishi hewa kwenye maeneo mengine nako kulikuwa na hewa hewa nyingi ambazo nazo zilikuwa zinatafuna fedha za Watanzania na baada ya kuchukuliwa hatua mbalimbali fedha sasa ziko salama.

"Hatua hizi zimesaidia fedha kuonekana na ndio maana Serikali kwa sasa ina fedha zake za kutosha na nchi inaweza kujiendesha kwa miezi mitano.Pia kulikuwa kuna fedha nyingi ambazo zilikuwa zinatumika kwenye safari na makongamano .Baada ya kuzibana imesaidia maana tunaweza kutekeleza miradi kwa fedha zetu."Kuna wakati tuliomba fedha sana kwa ajili ya baadhi ya miradi ukiwamo wa reli ya kisasa na baada ya kuona hivyo tumeamua kuanza kujenga kwa fedha zetu wenyewe kwa asilimia 100 ambapo Sh.Trilioni 7.6 zote zimetolewa na Watanzania wenyewe,"amesema.

Kuhusu elimu bure ,Rais Magufuli amesema wakati anatoa ahadi ya kutoa elimu bure hata yeye hakuwa anaamini kama itawezekana lakini ahadi ni deni, hivyo baada ya kuingia madarakani aliona kuna fedha ziko mahali zimelala na hivyo amezichukua na kuzipeleka kwenye kutoa elimu bure.Amesema idadi ya wanafunzi imeongezeka kwani kabla ya elimu bure  idadi ya wanafunzi waliokuwa wanaanza darasa la kwanza ilikuwa milioni moja na sasa ni wanafunzi milioni mbili na hivyo mpango huo umesaidia na Serikali itaendelea nao.

Dk.Magufuli pia amesema kwenye mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu nako hali ni nzuri na kufafanua zamani ili wanafunzi wapate mkopo ilikuwa lazima waandamane lakini sasa ni tofauti.Pia amesema kuna vyuo vikuu ambavyo vilikuwa vinaanzishwa havina hata sifa ya kuitwa vyuo vikuu na huo ulikuwa mkakati wa baadhi ya watu wa kutumia vyuo hivyo kupeleka wanafunzi wao kwa ajili ya kupata fedha hizo ambazo zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi.

"Kwa sasa tumefanikiwa kudhibiti vyuo hivyo na kwamba kuna baadhi ya wanafunzi waliokuwa na masters lakini sasa ndio wameamua kuanza kusoma tena shahada ya kwanza baada ya kubaini hakuna ambacho wamekipata na huo ndio ukweli,"amesema.

No comments: