Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) na Mkuu wa MKoa wa Ruvuma Christina Mdeme (kulia ) wakichanganya kokoto katika Kituo ch Umahiri Songea wakati wa ziara Kairuki kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho
Sehemu ya jengo la Kituo cha Umahiri Songea katika hatua zake za ujenzi
Afisa Madini Mkazi wa Songea Abraham Nkya akieleza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Madini Angellah Kairuki alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mdeme (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Songea Ploliti Mgema wakijadiliana jambo wakati Waziri Kairuki alipomtembelea Mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake.
Baadhi ya Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri Songea.
Waziri wa Madini ANgellah Kairuki akiteta jambo na AFisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma Abraham Nkya wakati wa ziara ya Waziri Kairuki kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Songea. Wa Pili Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mdema , Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Madini Gladness Mkambaita na wa kwanza kulia ni Meneja wa Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini, Andrew Eriyo.
Na Asteria Muhozya, Songea
Serikali imesema haijaruhusu uchimbaji wa Madini katika Mto Muhuwesi na kwamba tayari Wizara ya Madini ilikwishakutoa maelekezo yapatayo matano ambayo wahusika wanatakiwa kuyafanyia kazi ili itoe maamuzi.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Songea, wakati akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ambaye alimwomba Waziri asimamishe uchimbaji huo na kwamba tayari Mkoa umezuia shughuli hizo kuendelea kwa kuwa ndiyo chanzo cha maji mkoani humo na kwamba, alifanya hivyo ili kulinda miundombinu ya barabara.
Waziri Kairuki alimweleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa, wizara ilitoa maelekezo kwa wahusika kwamba wanatakiwa kuwasilisha barua ya ridhaa ya Waziri wa Maji, ridhaa ya Wakala wa Barabara nchini (TANROAD), ridhaa ya Bodi ya Bonde la Mto Ruvuma/Pwani na Kusini ili wizara ijiridhishe kabla ya kutoa maamuzi.
“ Tunataka tujiridhishe na approval kutoka katika maeneo hayo na vikipatikana vyote, nitafanya uamuzi. Kwa sasa ipo ridhaa ya bodi ya bonde la mto Ruvuma,” alisisitiza Waziri Kairuki
Pia, akifafanua kuhusu kusimama kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya Uranium unaofanywa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, waziri Kairuki alisema kuwa, kampuni hiyo iliomba kusisitisha shughuli zake kwa kipindi cha miaka mitano kutokana na bei ya madini hayo kushuka katika soko la dunia na kwamba , suala hilo bado linafanyiwa kazi kitaalam na kiuchumi hivyo, bado serikali haijatoa majibu kuhusu suala husika.
Kuhusu upatikanaji wa masoko kwa wachimbaji wa madini, Waziri Kairuki alieleza kuwa, tayari serikali imepanga kuanzisha masoko ya madini katika maeneo mbalimbali nchini, na hivyo kutoa rai kwa Wakuu wa Mikoa nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishwaji wa masoko hayo. Waziri Kairuki alitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina ambaye alitaka kujua ni namna gani serikali inawasaidia wachimbaji wadogo kupata masoko ya kuuzia madini madini yao.
“Mhe. Waziri Mkoa wetu umejaliwa kuwa na madini ya aina mbalimbali na madini haya yamekuwa ni kichocheo cha uchumi. Sasa, bado wachimbaji wetu wanapata changamoto ya masoko kwa ajili ya kuuza madini yao,” alisema Mkuu wa Mkoa Mndeme.
Akizungumzia ujenzi wa Vituo vya Umahiri, Waziri Kairuki alisema, ujenzi wa vituo vya umahiri vinavyojengwa maeneo mbalimbali nchini vinagharimu takribani Bilioni 11 ambao ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Aliongeza kuwa, Songea ni eneo ambalo serikali inaliangalia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za ukataji na uongezaji thamani madini.
Alisema kuwa, serikali iliona umuhimu wa kuwepo na vituo hivyo kutokana na wananchi wengi kutamani kuingia katika shughuli za uchimbaji lakini bado uchimbaji wao umekuwa si salama na wenye tija hivyo, uwepo wa kituo hicho utawezesha kutoa elimu ya uchimbaji sahihi na wenye tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Christina Mndeme akizungumzia uwepo wa kituo hicho alisema, kukamilika kwa kituo hicho kutawezesha shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika mkoani humo, kupanua wigo wa shughuli za uchimbaji na wachimbaji kuchimba kwa faida.
Aliongeza kwamba, wachimbaji watapata taarifa sahihi wa mahali gani wauze madini yao na pia uwepo wake utawezesha kutangaza aina ya madini yanayopatikana mkoani huo.
Vilevile, alisema kuwa, kituo hicho kitawezesha kupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa kwani kitawezesha kupata taarifa sahihi za wapi wachimbe madini.
Naye, Afisa Madini Mkoa wa Ruvuma Abraham Nkya alisema kuwa, ujenzi wa kituo hicho utawezesha kurahisisha upatikanaji wa takwimu za madini za mkoa huo, wachimbaji kupata elimu ya utaalamu wa uchenjuaji bora wa madini, elimu ya ujasiliamali wa shughuli za madini, afya na usalama mahali pa kazi.
Pia, aliongeza kuwa, uwepo wa kituo hicho chenye nafasi kubwa, kitaweza kuwahudumia wachimbaji wengi zaidi.
Waziri Kairuki alitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Songea Novemba 26.
No comments:
Post a Comment