Wednesday, November 28, 2018

LUGOLA ASEMA POLISI WACHACHE WANAOLICHAFUA JESHI KWA KULA RUSHWA DAWA YAO IPO JIKONI



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola (kushoto), akifurahi jambo wakati alipokua anasalimana na Diwani wa Kata ya Nyamihyolo, Mgendi Patrick, wakati Waziri huyo alipopokelewa na mabango na wananchi wa Kijiji cha Mahyolo, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambayo yalikua yana ujumbe mbalimbali. Lugola aliwataka wananchi wa Kijiji hicho wafanye shughuli za maendeleo bila kuvunja sheria za nchi. Pia alitoa onyo kwa baadhi ya askari kuiacha tabia hiyo haraka iwezekanavyo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola (kulia), akimsikiliza Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahyolo, Clifford Bwire, alipokua anajibu maswali kuhusu ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Mahyolo iliyopo Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, kutokuendelea licha ya kua wananchi wa kijiji hicho walichanga fedha. Pia Lugola aliwataka wananchi wa Kijiji hicho wafanye shughuli za maendeleo bila kuvunja sheria za nchi. Pia alitoa onyo kwa baadhi ya askari ambao wanaomba rushwa kwa wananchi kuiacha tabia hiyo haraka iwezekanavyo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola, akiwasalimia wanafunzi wa Shule ya Msingi Muungano iliyopo Kijiji cha Namibu, Kata ya Neluma, Jimbo la Mwibara, Bunda, Mkoani Mara, wakati Waziri huyo alipofanya ziara shuleni hapo kwa ajili ya kuwasalimia wanafunzi hao pamoja na uongozi wa shule hiyo. Lugola yupo katika ziara ya kuhamasisha maendeleo na pia kuwapa elimu ya ulinzi na usalama jimboni kwake. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.



WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola maesema licha ya kuwa Jeshi la Polisi linapambana usiku na mchana kuwaondoa askari wala rushwa lakini ana taarifa ya baadhi yao wanaendeleza tabia hiyo, hivyo dawa yao ipo jikoni inachemka.

Amesema licha ya kutoa taarifa mara kwa mara kuwataka askari hao kufanya kazi kiuhadilifu kwa kuacha tabia ya kuomba rushwa lakini baadhi ya askari hao hawajamuelewa hivyo atapambana nao mpaka Jeshi hilo litakapokuwa safi.

Lugola amesema anapokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi kuwalalamikia baadhi ya Polisi kufanya matukio hayo ambayo hayakubaliki lakini anawataka askari polisi hao wajue kuwa kati ya maagizo aliyopewa na Rais Dk. John Pombe Magufuli ni kupambana na rushwa ndani ya Wizara hiyo, hivyo hawezi kumuangusha hata siku moja.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Namibu, Kata ya Neruma, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, Lugola alisema baadhi ya polisi wanalichafua Jeshi hilo kutokana na tamaa zao, hivyo ameendelea kusisitiza kuwa, Serikali ya Magufuli ya awamu ya tano siyo ya kuchezewa.

“Jeshi la Polisi linalinda usalama wa raia na mali zao, linapambana na rushwa katika mambo mbalimbali yakiwemo ya ardhi hapa kijijini, hivyo ndugu wananchi mnapopata migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi na mengineyo akikisheni mnatoa taarifa polisi ili muweze kusaidiwa,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola aliongeza kuwa, anapofanya ziara sehemu mbalimbali nchini anapokea maswali na pia anatumiwa meseji zikilalamikia tabia ya baadhi ya askari polisi ambao wanaomba rushwa hasa askari wa usalama barabarani.

Lugola aliongeza kuwa, licha ya kuwa Polisi inaendelea kupambana na rushwa lakini nchi ipo salama hivyo wananchi popote nchini wanapaswa kuwa na amani na kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja za kilimo kijijini hapo. “Mimi sitakubali kuona mwananchi anateseka, mwananchi anaonewa, nasema hivi hao askari ambao ni wachache sana nitahakikisha ninapambana nao bila huruma, kwanini mnaonea wananchi ambao wengi wao ni maskini kwa kuwaomba rushwa, hii haijakaa sawa,” alisema Lugola.

Lugola ambaye mwezi Septemba alitangaza kuwa vituo vya polisi vifanye kazi saa 24 kwa kutoa dhamana kwa mwananchi yeyote mwenye sifa atakayekuja siku ya Jumamosi au Jumapili, akiwa na maana kuwa ataondoa rushwa katika vituo, na pia alitangaza kupambana na askari wala rushwa pamoja na watumishi wote waliopo wizarani kwake na Serikali kwa ujumla.

Aidha, Lugola aliwataka wananchi wa Kata hiyo waendelee kufanya shughuli za kimaendeleo katika vijiji vyao na pia waanze maandalizi ya kilimo, naye atahakikisha anatoa misaada mbalimbali ikiwemo mbegu ili wananchi hao waweze kupata mazao yaliyo bora kwa hapo baadaye.

No comments: