Wednesday, November 28, 2018

GAVANA LUOGA ATOA PONGEZI MAALUM KWA WAFANYAKAZI BOT KUANDAA MIFUMO YA KUKUSANYA MALIPO YA SERIKALI



Kushoto: Gavana wa BoT Prof. Florens Luoga akimpongeza Bi. Mota Cecilia Mlama kwa kazi nzuri. Kulia Prof. Luoga (waliokaa katikati) katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa BoT walioshirikiana na wataalam kutoka taasisi zingine za serikali kutengeneza mifumo ya kulipa watumishi wa umma mishahara kupitia Benki Kuu na kukusanya malipo ya serikali kielektroniki. Waliokaa wengine kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Kened Nyoni na kulia ni Bi. Flora Mwaigomole, Meneja wa Rasilimali Watu.


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, amewapongeza wafanyakazi nane wa Benki Kuu upande wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa mchango na uzalendo wa hali ya juu uliowezesha kusimikwa kwa mifumo ya kielektroniki ya kulipa mishahara na kukusanyia mapato ya serikali nchini.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kuwapongeza wafanyakazi hao kwa kushirikiana na wataalam kutoka taasisi zingine za serikali katika kubuni, kutengeneza na kusimika mifumo ya kukusanya malipo ya serikali kielektroniki ya GePG na kulipa mishahara kupitia Benki Kuu ya Tanzania (GSPP) kati ya mwaka 2015 na 2018.

“Siku zote, Benki Kuu imekuwa ikihamasisha wafanyakazi wake kujituma katika kazi kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu ili kuongeza tija na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea. Katika hili, tunawapongeza kwa kuwa mmetekeleza kwa vitendo falsafa hii kutokana na utendaji wenu uliotukuka. Hongereni sana!,” amesema Prof. Luoga.

Gavana Luoga alisema kwa kutumia wataalam wa ndani kusimika mifumo hiyo, sio tu kumeiwezesha serikali kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato, bali pia kumeliwezesha taifa kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kununua mifumo kama hiyo kutoka nje ya nchi.

Pamoja na pongezi hizo, Gavana Luoga amewakabidhi wafanyakazi hao barua ya pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais, Balozi John Kijazi, aliyoitoa kwao kutokana na kazi yao kutambuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati taarifa ya kazi hiyo ilipowasilishwa kwake na Wizara ya Fedha na Mipango. Waliopongezwa ni Kiongozi wa Timu ya BoT, Bw. Joel Ngussa, Bw. Eric Lwambura, Bw. Mutashobya Mushumbusi, Bw. Jeremiah Tunutu, Bi. Mota Cecilia Mlama, Bw. Emmanuel Millinga, Bw. Anthony Lyaruu na Bw. George Sije.

“Aidha, napenda kutoa rai kwa wafanyakazi wote wa Benki Kuu kuchukulia mafanikio ya wenzetu hawa wachache kama chachu katika utendaji wenu wa kazi. Heshima ya Taasisi hii katika taifa na hata kimataifa itatokana na jinsi kila mmoja wetu anavyofanya kazi kwa kujituma, kwa weledi na kwa kuleta matokeo chanya ambayo yatasaidia maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla,” Gavana amesema.

Prof. Luoga amesema Benki Kuu itaendelea kufanya kazi kwa kutumia wataalam wa ndani kwa manufaa ya taifa na kuongeza kuwa “ni wajibu wa taasisi hii na taifa kwa ujumla kutambua mchango mkubwa unaotolewa na wataalam wa ndani kwa kuhakikisha wanatumika kikamilifu.”

Katika maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Kened Nyoni, alisema utekelezaji wa miradi hiyo umeiwezesha serikali kuanza kulipa mishahara ya watumishi wake kupitia Benki Kuu ya Tanzania, kuokoa fedha zilizokuwa zinalipwa kwa mawakala katika mchakato wa ulipaji mishahara pamoja na kuharakisha mchakato mzima wa ulipaji.

Pia, mfumo wa GePG) umeiwezesha serikali kukusanya mapato ya taasisi zake kikamilifu, kuwa na uwezo wa kujua kila wakati kiwango cha makusanyo (maduhuri) yake na pia kupunguza upotevu. Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake, Bw. Joel Ngussa alisema kwamba pongezi walizopata ni “chachu ya kuongeza juhudi ya utendaji katika kazi na miradi mingine yenye tija kwa taasisi na taifa kwa ujumla.” Aidha, Bw. Ngussa ameeleza kutambua ushiriki na kazi kubwa ya watumishi wenzao katika kutekeleza miradi hiyo kutoka Benki Kuu pamoja na taasisi zingine nchini.

“Kwa niaba ya timu nzima iliyoshiriki katika kazi hizo, napenda kuchukua fursa hii kuweka katika kumbukumbu mchango wa wafanyakazi wengine wa Benki Kuu ambao waliwezesha kufanikisha kazi hiyo. Wafanyakazi hao ni Bi. Peragia Nsabi, Bw. Stephano Mwendo, Bw. Justice Faustine, Bw. Mathew Massoy na Bw. Luphingo Mwasalujonja,” alisema Bw. Ngussa

Hafla hiyo ya ilihudhuriwa pia na wafanyakazi na menejimenti Benki Kuu ya Tanzania.

No comments: