Wednesday, November 28, 2018

PROFESA MBARAWA AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI MUKABUYE



Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Paul Bura (kushoto) mara baada ya ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Mukabuye, wilayani Kibondo katika Mkoa wa Kigoma.
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa akiwa kwenye kisima cha IOM kilichopo eneo la Kumwayi kinachotumiwa na Mradi wa Maji wa Kibondo Mjini, mkoani Kigoma.
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa akikagua ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Mabamba/Mukurazi uliopo Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma.
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa akizungumza na viongozi na watendaji wa Wilaya ya Kibondo katika ofisi za wilaya, mkoani Kigoma.
Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa akijibu maswali ya wakazi wa Kijiji cha Mukabuye kabla ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Mukabuye, wilayani Kibondo katika Mkoa wa Kigoma.

……………………

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Kampuni ya KGG Investment Ltd & Tanafri Group Ltd inayojenga Mradi wa Maji wa Mukabuye kuhakikisha inakamilisha mradi huo ifikapo mwezi Disemba, 2018 ili wakazi wa Mukabuye na vijiji jirani wapate huduma ya majisafi na salama.

Profesa Mbarawa ametoa maagizo hayo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mukabuye kwenye ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma. “Mradi wa Maji wa Mukabuye umeanza kutekelezwa Juni, 2018 na unategemewa kukamilika mwezi Aprili, 2019 kulingana na mkataba. Lakini mimi nataka mkandarasi akamilishe mradi huu mwishoni mwa mwaka huu ili wananchi hawa wapate maji haraka iwezekanavyo’’, amesema Profesa Mbarawa.

“Hakuna sababu ya kusubiri mpaka mwakani mradi huu ukamilike, kama fedha zipo na tutamlipa mkandarasi kiasi kilichobaki. Sina mashaka na uwezo wa mkandarasi kwa sababu uwezo anao, kikubwa ni kuongeza bidii na kasi ya utekelezaji’’, aliongeza Profesa Mbarawa. Akisisitiza ziara yake imelenga kubaini na kutatua changamoto zote za miradi ya maji katika Wilaya ya Kibondo kwa kuwa Serikali imelenga kuwa karibu na wananchi na kutatua kero zao kwa wakati.

Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo inatekeleza Mradi wa Maji wa Mukabuye kupitia Bajeti ya 2018/19 kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1 unaohusisha vijiji vitatu vya Mukabuye, Kageyo na Nyakilenda.

Vilevile, Profesa Mbarawa amekubali ombi la Mkuu wa Wilaya ya KIbondo la kuongeza mtandao wa bomba la maji la Mradi wa Mabamba/Mukurazi kwa umbali wa kilomita mbili mpaka kwenye Soko la Pamoja la nchi za Tanzania na Burundi lilipo mpakani mwa nchi hizo katika Kijiji cha Mabamba kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwenye soko hilo. Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Wilaya ya Kibondo, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Paul Bura amemshukuru Waziri wa Maji kwa kukubali ombi lao kutokana na soko hilo kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa halmashauri.

Pia, ameishukuru Serikali kwa jitihada inazozifanya katika kuhakikisha inamaliza kero ya maji wilayani Kibondo, kitu ambacho kimekuwa tatizo kubwa Kibondo ikizingatiwa asilimia 29 ya wakazi wa wilaya hiyo ndio wanapata huduma ya majisafi na salama. Akisema kwa sasa Serikali imetoa zaidi ya Sh. Milioni 359 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kibondo Mjini, ambapo awamu ya kwa

nza ikikamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji mpaka asilimia 56. Huku awamu ya pili itakayohusisha uchimbaji wa visima vitatu kazi itakayofanywa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) inayotegemewa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2019, itafikisha huduma ya maji asilimia 90 katika Mji wa Kibondo.

No comments: