Thursday, November 29, 2018

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, BASHUNGWA ATEMBELEA NFRA APONGEZA UJENZI WA MAGHALA NA VIHENGE VYA KISASA


Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa 
Mtendaji Mkuu wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi Vumilia L. Zikankuba


Na Mathias Canal-NFRA, Dodoma

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa amefanya ziara ya kikazi kwa kutembelea na kujionea shughuli zinazofanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo Mhe Bashungwa amekagua ujenzi wa Maghala na Vihenge vya Kisasa (Silos) ambapo ameipongeza serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuanzisha ujenzi wa mradi huo utakaoongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka.

Akizungumza na wafanyakazi wa NFRA mara baada ya kuzuru katika ofisi hizo zilizopo Mtaa wa Relini-Kizota Mhe Bashungwa alisema kuwa uongozi imara wa Dkt Magufuli umepelekea Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland kusaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ametoa rai kwa Mtendaji Mkuu wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi Vumilia L. Zikankuba kuweka msisitizo zaidi katika utoaji elimu kwa wakulima kuhusu njia bora za kuhifadhi mahindi ili wakati wanapotafuta soko waweze kupata soko imara na tija kutokana na nafaka hiyo.

Alisema kuwa teknolojia hiyo ni muhimu katika kipindi hiki ambacho serikali imeamua kwa dhati kuimarisha vyama vya Ushirika nchini ili kuwa na kauli ya pamoja hivyo wakulima wanapaswa kuwa na Imani na serikali yao wakati inatekeleza mikakati mbalimbali katika sekta ya kilimo.

Mhe Bashungwa alisema kuwa serikali inatazama namna nyingine ya Kujenga maghala na vihenge vya kisasa kwa ajili ya mazao mengine ambayo yapo chini ya Ushirika ili kuimarishwa Zaidi sekta ya kilimo nchini.

“Ujenzi huu unatufundisha kwamba tunaweza kujenga maghala katika maeneo mengine nchini hususani katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ajili ya zao la Korosho” Alikaririwa Mhe Bashungwa

Mhe Bashungwa ameipongeza NFRA kwa kazi kubwa ya usimaizi wa ujenzi wa mradi huo ambao umefikia katika hatua nzuri za ujenzi huku akisisitiza NFRA kupitia idara ya masoko kupunguza mazao ambayo yamekaa kwa muda mrefu ghalani kuyauza ili fedha hizo zinunue mahindi mengine kwa wakulima.

Sambamba na hilo Mhe Bashungwa ameipongeza pia NFRA kwa kununua mahindi ya wakulima kupitia mfumo wa Ushirika katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhifadhi kwani jambo hilo linawanufaisha wakulima wengi nchini.“Na katika hili nazitaka Taasisi zingine kuja kujifunza kwa NFRA kuhusu namna bora ya ukusanyaji wa mazao kwa wakulima” Alisema

Utekelezaji wa mikataba kati ya NFRA na wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo muda wa utekelezaji ni miezi 18 tangu tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji wa mikataba ya wakandarasi, hivyo kabla ya 2020 utakuwa umekamilika.

Ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa (Silos) unatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) ambapo msimamizi wa utekelezaji wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ukihusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa pamoja na ukarabati wa ofisi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi Vumilia L. Zikankuba alisema kuwa Mradi huo utaifanya serikali kuwa na uwezo wa kuhifadhi mara mbili ya uhifadhi wa sasa kutoka Tani 251,000 hadi Tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Bi Zikankuba ameeleza kuwa Mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 55, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amesisitiza kuwa mikataba ya ujenzi ilianza kufanya kazi tarehe 9 Disemba 2017 huku akisema Mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) ambapo msimamizi wa utekelezaji wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Bi Zikankuba alisema kuwa Mradi utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa pamoja na ukarabati wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni Arusha (Babati), Dodoma, Makambako, Mbozi, Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Mpanda. 

No comments: