Thursday, November 29, 2018

KORTI YATAKA UPELELEZI KESI YA UHUJUMI UCHUMI INAYOMKABILI ALIYEKUWA MFANYAKAZI MSTAAFU TAZAMA,WENZAKE UKAMILIKE MAPEMA

Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa utetezi katika kesi ya kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia(Tazama), Samwel Nyakirang'ani(63) na wenzake 11 kukamilisha mapema upelelezi dhidi ya kesi hiyo ili kigundua nani anahusika na nani hausiki kwenye kesi hiyo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ameeleza hayo leo Novemba 29, 2018 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa.

Kabla ya kueleza hayo Wakili wa Serikali Patrick Mwita alidai kuwa upelelezi katika shauri hilo haujakamilika, jalada bado lipo katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa ajili ya kulichambua na kisha kulitolea maamuzi kuangalia washtakiwa gani washtakiwe na washtakiwa gani waachiwe huru.

Kutokana na hayo, Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka wajitahidi kumaliza shauri hilo mapema kwani shauri lenye watu wengi kama hili ni vema ikajulikana mapema kwani inawezekana baadhi yao hawahusiki.Nyakirang’anyi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

 Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 10 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia upelelezi kama utakuwa umekamilika ama la.Washtakiwa wote wapo rumande kutokana DPP kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana.Mbali Samweli, washtakiwa wengine katika kesi  hiyo namba 1/2018 ni Nyangi Mataro( 54) Mwalimu wa Shule ya  Msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.

Mfanyabaishara, Farijia Ahmed(39)mkazi wa Soko Maziwa Kigamboni, Malaki Mathias(39) mkazi wa Magogoni, Kristomsi Angelus(25) mkazi wa Soko Maziwa,  Fundi Ujenzi Pamfili Nkoronko(40) mkazi wa Tungi Kasirati na Henry Fredrick (38) mkazi wa Tungi Kigamboni.Wengine ni Audai Ismail (43) ambaye ni mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa  kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, kinyume cha sheria  ya Uhujumu uchumi.Katika shtaka la kwanza, kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilaya ya Kigamboni, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoa katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Bandari nchini(TPA).

Pia wanadaiwa kuharibu miundo mbinu ambapo wanadaiwa kutoboa  bomba la hilo, ambalo  lilikuwa likitumika kufirisha mafuta,  mali ya Mamlaka ya Bandari nchini( TPA).

Aidha washtakiwa wanadaiwa kuharibu  bomba la mafuta mazito( Crude oil) lenye upana wa Inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali ya Mamlaka ya Bandari nchini( TPA).

No comments: