Thursday, November 29, 2018

DODOMA ITAKAVYOKUWA USIPIME....JIJI LAKE KUFANANISHA NA MIJI YA MAJUU SIO LA DAR

*Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma aweka wazi mikakati yao
*Aeleza jinsi tamko la Rais lilivyoleta mabadiliko makubwa

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAKATI Rais Dk.John Magufuli akitarajiwa kuhamia rasmi katika Jiji la Dodoma Desemba mwaka huu, tayari mikakati mbalimbali inaendelea la kuliweka sawa Jiji hilo kuhakikisha linaendana na hadhi ya kuwa makao makuu ya Serikali.Kwa sasa kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa maendeleo inayoendelea kufanyika kwa kasi kubwa kuhakikisha Jiji la Dodoma linapendeza na kuwa na muonekano wa aina yake ambapo Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi ameeleza hatua kwa hatua namna ambavyo wamejipanga.

Akizungumza na Michuzi Blog na Michuzi TV kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika Mjini Dodoma Kunambi amesema kuwa baada ya Rais Dk.John Magufuli kutangaza Dodoma kuwa Jiji na Serikali kuhamia rasmi kuna hatua mbalimbali zimechukuliwa.

"Kuna mambo makubwa ambayo Rais wetu mpendwa ameyafanya baada ya kutangaza Dodoma kuwa Jiji na kuhamishiwa kwa shughuli za Serikali Kuu.Tunakumbuka aliamua kuivunja CDA na shughuli za CDA kuhamishiwa Manispaa ya Dodoma na baadae kuwa Jiji.Niwahakikishie Watanzania baada ya tamko la Rais la kuhamishia Serikali Dodoma kuna mambo makubwa yamefanyika,"amesema.

Amefafanua baada ya tamko hilo, Jiji la Dodoma nalo likaanza kuweka mikakati yake kufanikisha dhamira ya Rais ambapo moja ya mambo ambayo walifanya ni kuandika maandiko kwa ajili ya kupata fedha za kwa ajili ya miradi mitano waliyoamua kuanza nayo katika kuboresha Jiji hilo.

"Maandiko yetu yalisaidia kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kituo kikubwa cha mabasi ambacho tunaamini kitakuwa cha kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki, soko la kisasa , maeneo ya kupumzika, ujenzi wa miundombinu ya barabara, dampo la kisasa la kuhifadhi taka na eneo la kuegesha malori,"amesema Kunambi.

Amefafanaua kupitia andiko hilo wamepata fedha Sh.bilioni 77.8 na tayari sehemu ya fedha hizo zimeanza kufanya kazi kutokana na miradi yote ambayo wameikusudia kuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi."Tunaendelea kuisuka Dodoma , tunataka iwe Dodoma ambayo Jiji lake huwezi kulifafanisha na Jiji la Dar es Salaam, bali litaweza kufananishwa na miji kama ya Tokyo nchini Japan au Pritorio na Durban nchini Afrika Kusini ama Woshington nchini Marekani,"amesema Kunambi.

Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara,Kunambi amesema wanaendelea na ujenzi na wapo hatua mbalimbali na kwamba katika eneo hilo la miundimbinu wameweka ramani ambayo itaunganisha Jiji la Dodoma kwa usafiri wa anga, reli na barabara.

Pia amesema kwa namna barabara za Jiji la Dodoma zinavyojengwa hakutakuwa na msongamano kama ilivyo kwenye miji mingine iliyopo nchini na kwamba Rais Dk.John Magufuli ametoa maelekezo ya namna ambavyo barabara za Jiji la Dodoma zinatakiwa ziwe.

"Kutakuwa na barabara ambazo zinaondoa msongamano kati kati ya Jiji na ujenzi unaendelea kuhakikisha miundombinu inakamilika kwa wakati .Kutakuwa na barabara mchepuko ambazo lengo kuu ni kuondoa msongamano.Kutakuwa na taa za barabarani.Kwenye kituo cha mabasi ambacho kinajengwa kwa wakati mmoja kitakuwa na uwezo wa kuegesha mabasi makubwa 250, gari ndogo 600, bajaji na bodaboda 500.Eneo la kituo cha mabasi kina ukubwa wa hekari 86,"amesema Kunambi.

Pia ameeleza namna ambavyo ramani ya Jiji hilo katika miundombinu ambavyo itakuwa na muunganiko wa usafiri wa anga, reli na magari. "Dodoma tumeamua msafiri ataamua mwenyewe atumie usafiri wa aina gani kwenda anakotaka.Kwa watakaoutumia usafiri wa anga kutakuwa na treni ya Jiji inayoanzia uwanjani wa ndege unaojengwa eneo la Msalato.Pia kwenye kituo cha mabasi nako kutakuwa na treni za Jiji ,"amesema.

No comments: