Monday, November 19, 2018

DKT. MAHIGA AMWAKILISHA RAIS MAGUFULI KATIKA MKUTANO MAALUM WA WAKUU WA NCHI WA AU

Mhe. Augustine P. Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alimwakilisha Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliyofanyika tarehe 17-18 Novemba, 2018 mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mkutano huo, uliitishwa kufuatia maamuzi ya Mkutano wa 31 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Julai 2018 mjini Nouakchott, Mauritania ambapo Wakuu hao walielekeza uitishwe Mkutano Maalum kujadili kwa kina mabadiliko ya kitaasisi ndani ya Umoja huo. 

Mkutano huo ulijadili na kutolea maamuzi mapendekezo kuhusu Muundo wa Uongozi (Portfolios) za Kamisheni za Umoja wa Afrika; chaguzi za Uongozi wa Kamisheni; Kusitisha ajira za viongozi wa Kamisheni; na Mabadiliko ya kiutawala na fedha ikijumuisha utendaji.Mkutano ulikubaliana kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamisheni klutoka 10 hadi 8 ambao ni Mwenyekiti wa Kamisheni, Makama Mwenyekiti na Makamishna 6. Maamuzi hayo yataanza kutekelezwa mwaka 2021 baada ya uongozi wa Kamisheni uliopo sasa kumaliza muda wake. Maamuzi yote yaliyotolewa yalilenga kuboresha utendaji wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. 

Mhe. Waziri aliungana na viongozi wengine waliochangia katika mjadala wa kuboresha utendaji wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kuunga mkono mabadiliko ya kitaasisi katika Umoja huo. Mhe. Waziri alieleza kwamba maamuzi hayo yanalenga kuleta ufanisi kwenye kutekeleza majukumu ya Kamisheni na kuhakikisha Afrika inapata maendeleo inayostahili haswa kwa kuzingatia Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika. 

Katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mhe. Paul Kagame alitoa salamu za rambirambi kwa Serikali za Tanzania, DRC na Malawi kufuatia vifo vya walinda amani wa nchi hizo nchini DRC.Mhe. Waziri alimshukuru Mhe. Kagame kwa salamu hizo za rambirambi na kuahidi kwamba Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele kupigania amani ya kudumu barani Afrika.

Mkutano pia ulijadili Mamlaka ya Wakala wa Maendeleo ya Umoja wa Afrika (African Union Development Agency - AUDA). Mkutano ulifahamishwa kuwa mchakato wa kubadilisha Taasisi ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi (New Economic Partnership for Africa’s Development – NEPAD) kuwa AUDA utakamilika Februari 2019 kama inavyoelekezwa katika Maaumuzi ya Umoja wa Afrika Na. 691. Mkutano ulikubaliana na mapendekezo yote kuhusu Mamlaka ya AUDA na kwamba programu na miradi ya AUDA itafadhiliwa kupitia bajeti ya Umoja wa Afrika na misaada ya washirika wa maendeleo. 

Agenda nyingine iliyojadiliwa wakati wa mkutano huo ni mabadiliko katika Taasisi ya Mchakato wa Kujitathimini kiutawala Bora Africa (African Peer Review Mechanism - APRM), ambapo mapendekezo yalitolewa ya kuiunganisha APRM kuwa moja ya taasisi za Umoja wa Afrika na kugharamia shughuli zake kwa kutumia bajeti ya Umoja huo. Aidha, iliamuliwa kuwa Wanachama wote wa Umoja wa Afrika wawe Wanachama wa APRM na APRM iwe huru katika kutekeleza majukumu yake.

Agenda nyingine kuu iliyojadiliwa na kutolewa maamuzi ni mapendekezo ya makadirio mapya ya viwango vya kuchangia Umoja wa Afrika na mapendekezo ya adhabu kwa Nchi ambazo zitachelewa kulipa michango yake. Mkutano uliazimia kuitishwa kwa Mkutano kati ya Kamati ya Kudumu ya Mabalozi, Wataalam wa masuala ya Fedha kutoka nchi wanachama na Kamati ya Mawaziri wa Fedha kupitia makabrasha yote yanayohusu Viwango vya kuchangia na adhabu kwa nchi ambazo hazitoa michango yao kwa wakati. Mkutano huo, unatarajiwa kufanyika tarehe 28-29 Novemba, 2018, Addis Ababa, Ethiopia na mapendekezo ya wataalam yatawasilishwa kwenye Kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri mwezi Februari 2019. 

Mkutano pia ulipokea mapendekeo ya mgawanyiko wa majukumu kati ya AU, Jumuiya za Kikanda na Nchi Wanachama. Mgawanyo wa majukumu unapendekezwa kuwezesha Jumuiya za Kikanda, Umoja wa Afrika na Nchi Wanachama kila moja kutekeleza majukumu yake na yale ambayo watachangia kwa pamoja. Pembezoni mwa Mkutano huho wa Dharura Wakuu wa Nchi na Serikali walizindua Mfuko wa Amani wa Umoja wa Afrika (AU Peace Fund) ambao utashughulikia masuala yote ya Amani na Usalama katika Nchi Wanachama ikiwemo viashiria vya uvunjifu wa Amani ili kuzuia kuibuka kwa migogoro. Mhe. Waziri alishiriki katika uzinduzi huo. 


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dodoma, 19 Novemba 2018 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia. Nyuma yake ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Bi. Naimi Aziz. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Rais Mpya wa Ethiopia, Mhe. Sahle Work Zewdu katika Ikulu ya nchi hiyo tarehe 18 Novemba 2018. Dkt. Mahiga alikwenda kumpongeza Mhe. Rais kwa kuteuliwa na wote wawili walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga. (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Dkt Workneh Gebeyehu alipokwenda kumtembelea kwa ajili ya kufahamiana jijini Addis Ababa. 

No comments: