Thursday, November 22, 2018

CHUO CHA MISITU OLMOTONYI WAMFIKISHIA KILIO NAIBU WAZIRI MHE.KANYASU


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na Watumishi wakati alipowatembelea leo katika Chuo cha Misitu cha Olmotonyi jijini Arusha ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu aliposhika nyadhifa hiyo.( Picha na Lusungu Helela-MNRT)
Makamu Mkuu wa Chuo cha Misitu cha Olmotonnyi Bw.Steve Kigwere akisoma taarifa mbele ya Naibu Waziri, Mhe. Kanyasu wakati alipotembelea leo Chuo hicho kilichopo jijini Arusha kwa ajili ya kuzungumza na kuwasikiliza watumishi juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.( Picha na Lusungu Helela-MNRT)
Mkufunzi wa Chuo cha Misitu Olmotony,Charles Giliba akizungumza mbele ya Naibu Waziri Mhe, Kanyasu, wakati alipotembelea jana Chuo hicho kilichopo jijini Arusha kwa ajili ya kuzungumza na kuwasikiliza watumishi juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi .( Picha na Lusungu Helela-MNRT)

…………………………………………………………………. 

Watumishi wa Chuo cha Misitu cha Olomotonyi wamemuomba Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ashughulikie changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupandishwa vyeo.

Pia, watumishi hao wamesema wamekuwa hawapandishwi vyeo kwa muda mrefu jambo ambalo limekuwa likishusha ari ya kufanya kazi kwa bidii.
Wameyasema hayo leo mbele ya Naibu Waziri Mhe. Kanyasu wakati alipokuwa akisikiliza changamoto za watumishi wa Chuo hicho jijini Arusha ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na watumishi hao tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo .

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wenzake, Mkufunzi wa Chuo hicho, Philipina Shao amesema kwa muda wa miaka 12 hajapandishwa cheo na kwa sasa anakaribia kustaafu. Mbali na malalamiko hayo, Watumishi hao wamemueleza Naibu Waziri huyo kuwa Chuo hicho kimekuwa kama gereza kwa vile baadhi ya watumishi ambao wameonekana kufanya vibaya maeneo mengine huhamishiwa katika Chuo hicho kama adhabu. 

Wakizungumzia kuhusu watumishi hao ambao wamekuwa wakihamishiwa katika Chuo hicho kuwa wengi wao huwa wamebakiza miaka michache kustaafu, hivyo wanakuwa hawana mchango wowote kwa Chuo. 

Aidha, Mkufunzi wa Cho hicho,Dkt.Lupala Zacharia amesema kumekuwa na ushirikishwaji hafifu kati ya Chuo na Idara ya Misitu na Nyuki hali inayopelekea kujiona kuwa wao sio sehemu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ameongeza kuwa kumekuwa na mambo mengi ambayo yamekuwa yakifanywa na Idara pasipo kushirikishwa Naye Mkufunzi Charles Giliba amesema Chuo hicho kimetengwa kwa muda mrefu hata pale inapotea vikosi kazi vinapoundwa Wizarani vya kufanya kazi fulani wamekuwa hawapati nafasi ya kushirikishwa. 

“Hatutaki tubebwe, tuna sifa stahiki na tunajisikia tunadhulumiwa haki yetu kwa vile hatutumiwi ipasavyo” amesema Giliba Katika hatua nyingine, Wamemueleza Naibu Waziri huyo kuwa hata teuzi zinapotokea za kushika nafasi za juu katika masuala ya misitu, Chuo hicho kimekuwa hakipati nafasi ilhali kina wataalamu wabobezi na wenye uwezo hali ya juu. 

Aidha, Watumishi hao wamesema licha ya kuwa Chuo hicho kipo kwenye mfumo wa NACTE lakini hata hivyo Wakufunzi wamekuwa wakilipwa mshahara kama mafisa misitu kufuatia kukosekana kwa muundo wa utumishi. Hivyo wamemuomba Naibu Wazi huyo ashughulikie muundo huo ili waanze kulipwa stahili zao kama vyuo vingine ambavyo vipo katika mfumo huo
Kwa upande wake,Naibu Waziri Mhe.Kanyasu wakati alipokuwa akijibu kero hizo amewahakikishia Watumishi hao kuwa atazishughulikia baadhi ya changamoto hizo haraka iwezekanavyo. 


Pia, Amesema Chuo hicho hakijatengwa ila kumekuwa na mazoea ya viongozi walio wengi kuteua majina ya watalaamu kutoka vyuo vikubwa wakiamini huko ndiko kuna wataalamu. Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo ameishauri Menejimenti ya Chuo hicho isikae kimya badala yake isikume mambo hasa pale inapodhani yakifanyika yataweza kuisaidia Wizara pamoja na taifa kwa ujumla.

No comments: