Thursday, November 22, 2018

MHE HASUNGA AKABIDHIWA RASMI OFISI, DKT TIZEBA ASHAURI MAZITO KUHUSU KILIMO

Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Kulia) akifurahi jambo pamoja na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya kilimo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. 
Picha ya pamoja waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Naibu mawaziri wizara ya kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, na Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wote wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. 
Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza leo tarehe 22 Novemba 2018 amemkabidhi rasmi ofisi Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb).

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa mikutano maarufu kama Kilimo IV Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu mawaziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, na Wakuu wa idara na Vitengo.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mhe Dkt Tizeba amempongeza Mhe Hasunga kwa kuteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo ambapo amesisitiza kusimamiwa kwa weledi huduma za ugani ambazo kwa kiasi kikubwa hakuna jambo la kujivunia katika eneo hilo kutokana na mgawanyo wa kimajukumu kuwa katika wizara mbili ya kilimo na TAMISEM jambo ambalo linapunguza ufanisi wa kiweledi.

Alisema kuwa wizara inapaswa kuendelea kusomesha wataalamu mbalimbali nchini wakiwemo wa ugunduzi na utafiti ili kuongeza tija ya kilimo na utoaji elimu kwa wakulima na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa wananchi sambamba na Taifa kwa ujumla.

Vilevile amesema kuwa Wizara ya kilimo ni tanuru muhimu kwa mahitaji ya wananchi hivyo inapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi na serikali ikiwa ni pamoja na kupewa fedha kwa wakati ili kukamilisha miradi mbalimbali ambayo tayari imeanzishwa.

Kuhusu mfumo wa uzalishaji wa mbegu alisema kuwa serikali ina Wakala wa mbegu za kilimo (ASA) ambao wanafanya kazi nzuri ya uzalishaji wa mbegu lakini wanapaswa kuwezeshwa ili waweze kuzalisha mbegu kwa kutumia mfumo wa umwagiliaji badala ya kuzalisha mbegu wakati msimu wa kilimo unaendelea.

“ASA wanazalisha mbegu wakati ambapo msimu wa kilimo umefika hivyo mbegu zao zinakosa umuhimu kwa wakulima, hivyo wanapaswa kuzalisha mbegu kabla ya msimu wa kilimo kufika” Alisisitiza Dkt Tizeba.Kuhusu mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa unaendelea vyema lakini hausimamiwi ipasavyo na Taasisi zingine za serikali zilizopewa jukumu kubwa na muhimu la kusimamia shughuli hiyo wakiwemo Wakala wa majengo Tanzania (TBA).

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amempongeza waziri huyo mstaafu Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye wizara ya kilimo ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa weledi ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kipindi cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2018/2019 ambayo imekuwa kwa asilimia 7.1

Waziri Hasunga alisema kuwa Dkt Tizeba ni mfano wa kiongozi bora nchini ambaye ametekeleza majukumu yake kwa weledi na kutoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi wengine jambo ambalo linatoa chachu na kuonyesha jinsi alivyo mzalendo kwa Taifa.

“Kutokana na alama alizoziacha Dkt Tizeba kwenye wizara ya kilimo hakika tunastahili kumuona kama Mtakatifu kwani kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa chakula nchini lakini alisimamia kidete na kuhakikisha kuwa swala hilo linamalizika na sasa nchi ina ziada kubwa ya chakula hakuna njaa” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Dkt Tizeba alihakikisha kero ya Tozo na Kodi zinafutwa na kusaliwa na Tozo na Kodi chache jambo ambalo limeongeza ufanisi katika wizara, usimamizi huu mzuri uliofanywa hauwezi kusahaulika daima”Mhe Hasunga aliongeza kuwa mfumo wa uagizaji mbolea wa pamoja ulisimamiwa vizuri na Dkt Tizeba jambo hilo litasalia kuwa muhimu na alama kwa Taifa.

Aidha, Alisema kuwa katika uongozi wa Dkt Tizeba nchi imezidi kuimarika kupitia manufaa wanayoyapata wananchi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na mfumo wa ushirika ambao wananchi walipoteza imani kwa kiasi kikubwa na Ushirika lakini kwa kipindi cha muda mfupi umeimarika kwa kiasi kikubwa.

No comments: