Tuesday, November 20, 2018

BENKI KUU YAFANYA OPARESHENI MAALUM YA UKAGUZI, UDHIBITI WA BIASHARA HARAMU YA FEDHA ZA KIGENI NA UKIUKAJI WA SHERIA KATIKA KUENDESHA BIASHARA YA UBADILISHAJI FEDHA


*Wenye maduka ya kubadilisha fedha waliokiuka sheria kukiona,leseni zao zatakiwa BoT
*Pia kuzuia kuendelea kwa ukiukaji wa sheria na kudhibiti uendeshaji wa biashara ya ubadilishaji fedha

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) imesema imefanya oparesheni ya kushtukiza ya kukagua maduka ya ubadilishaji fedha na baadhi ya maduka bubu ambayo hayana leseni lakini yalikuwa yakiendesha biashara hiyo kinyume na sheria.

Operesheni hiyo iliratibiwa na Kitengo cha Ukaguzi cha Benki Kuu katika kutekeleza majukumu yake kisheria na kwamba hiyo ni oparesheni ya tatu kufanyika. 

Akizungumza leo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania amesema uchunguzi wa kina katika miezi sita iliyopita ulibaini kuongezeka kwa biashara za kubadilisha fedha kinyume cha sheria, na kukua kwa biashara haramu ya fedha za kigeni na utakatishaji fedha, hususan kupitia maduka ya kubadilisha fedha.

Amesema BoT kupitia juhudi za Kitengo cha Ukaguzi kuwapata wahusika hazikuzaa matunda katika oparesheni mbili zilizopita. Hiyo ni kwa sababu iligundulika kuwa kuna mtandao mpana na madhubuti wa shughuli hizo na ambao ulilenga kuhakikisha kuwa shughuli za udhibiti hazifanikiwi. Baada ya mashauriano na wataalam na kushirikisha vyombo vya upelelezi na usimamizi ilionekana kuwa ili kufanikisha operesheni hiyo lililokusudiwa ni muhimu wahusika wote wadhibitiwe kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi.

" Hii ilihitaji ushiriki wa maofisa wengi sana kutoka vyombo mbalimbali na kuhakikisha kila mahali ambapo ukaguzi uliendeshwa kuna usalama wa kutosha na Wananchi wanaarifiwa kutoingia sehemu husika kwa wakati huo. Baadhi ya washiriki katika zoezi hilo ni askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania wakiwa katika sare zao bila silaha.

"Hii ni kwa sababu siku oparesheni ilipofanyika askari wengi wa Jeshi la Polisi wapo kwenye kusimamia usalama katika vituo vya mitihani ya kidato cha pili inayoendelea," imeeleza taarifa hiyo ya BoT.Napenda kuwaarifu wananchi kuwa oparesheni hii imeisha salama na bila kuathiri mtu yeyote na tunawashukuru wananchi wa Jiji la Arusha kwa ushirikiano, hasa kwa kuwa watulivu,"amesema.

Amefafanua taratibu zinazoendelea ni za kisheria na kwamba mahojiano na wahusika yanakamilishwa na wale watakaokutwa na tuhuma za ukiukaji sheria watashughulikiwa kufuatana na taratibu za kisheria. Aidha amesema Benki Kuu inachukua hatua zifuatazo kuzuia kuendelea kwa ukiukaji wa sheria na kudhibiti uendeshaji wa biashara ya ubadilishaji fedha. Kwa takribani miezi mitatu sasa benki hiyo imesitisha utoaji wa leseni za biashara ya ubadilishaji fedha. 

Gavana amesema maombi yote yamesitishwa na maombi mapya hayatapokelewa mpaka taratibu mpya za uendeshaji wa biashara hiyo zitakapokuwa tayari na kusisitiza Wale wote watakaopatikana na makosa ya uvunjaji wa sheria leseni zao zitafutwa na hawataruhusiwa kufanya biashara hiyo tena. 

"Katika kipindi hiki wakati kesi zao zinashughulikiwa kisheria na ili kuzuia kuendelea kwa biashara haramu, leseni zao zinasitishwa na wanatakiwa kuzirudisha Benki Kuu mpaka kesi zao zitakapokamilika.

" Baada ya hapo taratibu mpya zitatumika;

Wale wote ambao walipatikana na tuhuma za ukiukaji sheria katika oparesheni mbili zilizopita na kufikishwa Polisi, wanatakiwa kurejesha leseni zao Benki Kuu mara moja. Leseni hizo pia zinasitishwa mpaka kesi zao zitakapokamilika;

Uchunguzi uliofanyika umebaini waendeshaji wengi wa maduka ya kubadilisha fedha hawakukidhi vigezo vyote japokuwa leseni zilitolewa kwao baada ya taarifa kupotoshwa,"amefafanua.Amsisitiza hao wote watapewa notisi ya kusitisha leseni na maduka yao kufungwa. Yeyote ambaye anajua kuwa upatikanaji wa leseni yake una dosari anashauriwa kurejesha leseni hiyo kwa hiari; na

Wale ambao wanaendesha maduka ya kubadilisha fedha bila leseni au kwa kutumia leseni zisizo zao wanatakiwa kufunga maduka hayo mara moja kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria. "Ili kuzuia watu wasiostahili kupenyeza na kujipatia leseni za biashara ya ubadilishaji fedha Benki Kuu imefanya mabadiliko ya ndani na inakamilisha taratibu mpya kuhusu uendeshaji wa biashara hiyo. Taarifa itatolewa hapo baadaye.

"Kwa vile oparesheni hii sasa inaingia katika hatua za kisheria zinazoweza kupelekea baadhi ya wahusika kupelekwa mahakamani, Benki Kuu haitaendelea kutoa taarifa zinazowahusu wahusika kwa sababu kwa kufanya hivyo kunaweza kupelekea kuingilia uhuru wa Mahakama," amesema Gavana wa Benki Kuu.

No comments: