Tuesday, November 20, 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA MSIKITI NA KUSISITIZA UTUMIKE VIZURI

*Awataka waumini wautumie kwa kufanya ibada na kuhamasisha amani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua msikiti wa Nandagala na amewataka waumini wa dini ya Kiislamu katika Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa wautumie vizuri msikiti huo kwa kufanya ibada na kuhamasisha amani na si vinginevyo.

“Msikiti huu ninauzindua leo (jana) naomba tuutunze vizuri na tuutumie kwa kufanya ibada na si ibada za kiuanaharakati. Watakaokuja msikitini na kufanya mambo ya hovyo Mwenyezi Mungu atawalaani.”Waziri Mkuu alizindua msikiti huo jana jioni (Jumatatu, Novemba 19, 2018), ambapo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha muda wa kufanya swala unapofika waende msikitini hapo kufanya ibada.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka waumini hao waanzishe madrasa na kuwafundisha watoto quran lengo likiwa ni kuwafundisha misingi ya dini na kuwaandaa vizuri na kuwawezesha kukua kiimani ili waje kuwa waja wema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alimshukuru Mzee Suleiman na familia yake kwa uamuzi wao wa kujitolea kujenga msikiti huo ambao utawawezesha waumini katika kijiji cha Nandagala kufanya ibada zao. “Namshukuru na Mzee Mamboleo na mkewe kwa kutoa eneo lao bure ili litumike kujengea msikiti.”

Kwa upande wake Sheikh Hilal Kipozeo ambaye alihudhuria uzinduzi wa msikiti huo aliwasisitiza waumini wa dini ya Kiislam watumie muda mwingi kwa ajili ya kufanya ibada na wajiepushe na vitendo vyenye kumuasi Mwenyezi Mungu na wadumishe amani.“Mtume Muhammad (S.A.W) baada ya kutoka katika mji wa Makka na kuhamia Madina kitu cha kwanza alijenga msikiti ili watu waweze kumwabudu Mwenyezi Mungu, alijenga soko ili watu washiriki shughuli za kiuchumi na alifanya upatanishi kwa makabila mawili kwa lengo la kuonesha kuwa kuishi kwa amani ni kitu bora.”

Wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu katika kijiji cha Nandagala walimshukuru mfadhili aliyejenga msikiti huo kwa sababu utawawezesha kuwa na eneo la kufanyia ibada baada ya lile la awali kubomolewa kwa kuwa walijenga katika hifadhi ya barabara.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,JUMANNE, NOVEMBA 20, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika dua iliyoongozwa na Sheikh Hilal Shaweji, maarufu Sheikh Kipozeo (watatu kulia) wakati alipozindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa Novemba 19, 2018. Wapili kulia ni Mfadhili ambaye kwa pamoja na familia yake alijenga Msikiti huo, Mzee Suleyum Mohammed Ahmed. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi baada ya kuzindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments: