Tuesday, October 9, 2018

Zawadi za milioni 30 kushindaniwa Rock City Marathon

Mwanza, 9 Oktoba 2018: Washindi wa michuano ya Rock City Marathon 2018  wanatarajiwa kuondoka na zawadi zenye thamani ya zaidi ya sh milioni 30 pamoja na medali, imefahamika. Mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza jijini Mwanza leo, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo zinazoratibiwa na kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Zenno Ngowi alisema pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, sh.mil 2/- kwa washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu, huku washindi wanne hadi kumi nao pia wakiibuka na medali na pesa taslimu.
Kwa upande wa mbio za  Kilomita 21, Ngowi alisema, pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh.  Mil 3/- kila mmoja, sh. Mil 1/-  kwa washindi wa pili na sh. 750,000/- kwa washindi wa tatu huku washindi wanne hadi wa kumi wakiibuka na  zawadi za pesa taslimu na medali kila mmoja.
 “Mbio za kilomita tano tunatarajia kwamba zitaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza sambamba na baadhi ya wakuu wa mikoa kanda ya Ziwa ambao pia watajumuika na baadhi ya viongozi waandamizi wa mikoa hiyo wakiwemo wabunge, viongozi na wafanyakazi wa mashirika na makampuni mbalimbali yaani corporates pamoja na ndugu zetu wenye ualbino,’’alisema.
Wadhamini watakaoshiriki katika mbio hizo ni pamoja na kampuni za Puma Energy Tanzania, Tiper, TANAPA, TTB, Nssf, Gold Crest, New Mwanza Hotel,  Cf Hospital, CocaCola, Metro Fm, Ef Outdoor,  Kk Security, Belmont Fairmount Hotel , Bigie Customs na Global Education Link.
Alibainisha kuwa mbio za Km 5 zitahusisha watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino ambapo washindi kwa upande wa mashirika watapatiwa zawadi za utambuzi ikiwemo medali na vyeti vya ushiriki huku pesa zikielekezwa kwa washiriki wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.
Alisema washindi wa mbio za Kilomita tatu ambazo zipo mahususi kwa ajili ya wazee watapatiwa sh 250,000/- kwa washindi wa kwanza huku washindi wa pili wakipata sh 200,000/ na watatu  wakipatiwa sh 100,000/-pesa taslimu.
 “Kwa washindi wa mbio za kilomita mbili na nusu zitakazohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi 10 watapatiwa sh 50,000/-kila mmoja huku wa pili na watatu pia wakipatiwa pesa taslimu.’’ Aliongeza
Bw Ngowi alivitaja vituo vinavyoendelea na usajili huo kwasasa kuwa ni pamoja na Igoma, Buzuruga, Airport Mwanza, Rock city mall, Chuo Kikuu cha Saut, Nyegezi Stand, Mwanza hotel, Nyamagana Stadium, Dampo pamoja na Nyakato.
Alisema usajili huo pia utahusisha ofisi zote za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga huku akiongeza : “Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana katika jengo la SHAMO Tower, Mbezi Beach , jijini Dar es, Salaam ”



No comments: