Friday, October 26, 2018

TPA YAWAASA WAHANDISI WAZALENDO KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI BANDARINI


WAHANDISI wazalendo wametakiwa kujipanga ili kuweza kuchangamkia fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali ya bandari nchini. 

Akizungumza wakati wa warsha iliyoandaliwa na Chama cha Wataalamu Washauri wa Wahandisi ‘Association of Consulting Engineers Tanzania’, (ACET), Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit C.V. Kakoko amesema wakati umefika kuchangamkia fursa zilizopo bandarini. 

Amesema kwamba japo malengo ya TPA kwenye warsha hiyo ni kuwafahamisha uwepo wa miradi mikubwa ya maendeleo hivyo kuchukua nafasi hiyo ili kuendeleza bandari kwa huduma zao kupitia miradi iliyopo na kuwaasa wachangamkie fursa zilizopo. 

“Bandarini kuna fursa ya kazi za ujenzi wa miundombinu katika nyanja zote kama ujenzi wa mitambo, umeme, mafuta, gesi na TEHAMA,” amesema Mhandisi Kakoko. 

Amesisitiza kwamba changamoto kubwa kwa sasa ni pamoja na kutochukua hatua za makusudi za kuchangamkia fursa kwa makampuni ya ujenzi ya ndani, uwezo mdogo wa makampuni ya wahandisi, wataalam wachache wenye weledi pamoja na vikundi vya taaluma kutoshirikiana. 

Akiwasilisha mkakati mpya wa kuboresha miradi ya miundombinu ya TPA kupitia huduma za wahandisi wazalendo, Mhandisi Kakoko ameshauri wahandisi wa ndani kuendeleza mafunzo kwa pamoja mara kwa mara. 

Mhandisi Kakoko amesema pia kwamba kuna haja ya kutoa taarifa za ufuatiliaji na maeneo ya changamoto mpya mara kwa mara na kwa pamoja ili kupata ufumbuzi wa haraka. 

“Ni muhimu zabuni zote za fedha ya ndani ziratibiwe kwa karibu na wataalam wa ndani hata ikibidi kwa kurekebisha sheria, kanuni na taratibu,” amesisistiza Kakoko. 

Aidha, amesema kuna haja ya kuendeleza mafunzo pamoja na kutoa taarifa za ufuatiliaji na maeneno ya changamoto mpya mara kwa mara. Amesisitiza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu katika miradi inayoendelea baina ya wahandisi ili kuendeleza miradi ya bandari na kuifanya iwe bora zaidi. 

Mapema wakati akifungua warsha hiyo, Rais wa ACET, Mhandisi Mpembe Ngwisa alisema TPA imefanya tukio kubwa na la kihistoria kundaa warsha kama hiyo kwa wahandisi. “Warsha kama hizi ni muhimu zikaendelea kufanyika mara kwa mara kwani hutoa fursa kwa wahandisi kuelezea changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi,” amesema Mhandisi Ngwisa. 

Mhandisi Ngwisa pia ameishukuru TPA kwa mikakati yake ya kuboresha miradi ya miundombinu yake kupitia huduma za wahandisi wazalendo. 

Amesema kwamba hatua hiyo itafungua fursa kwa wahandisi washauri wazalendo kuchangamkia zabuni za miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa. 

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu na Uwekezaji, wa TPA, Mhandisi Allen Banda amesema kwamba miradi yao mingi imefanikiwa kwa sababu ya uwepo wa wahandisi washauri. Mhandisi Banda amesema kwamba TPA inatoa fursa kwa wahandisi washauri kujipanga kwa ajili miradi mipya ya mwaka ujao wa fedha. 

“Nachukua fursa hii kushauri wahandisi washauri wazalendo wale wenye uzoefu kushirikiana na wengine ili kubadilishana uzoefu huo,” amesema Banda. Katika warsha hiyo, iliyohudhuriwa na wafanyakazi kumi (15) wa TPA, na wakurugenzi wa makapuni takribani 15 ya wahandisi washauri, michango mbalimbali ya jinsi ya kushirikiana ilitolewa. 

Aidha, Bodi ya usajili ilieleza umuhimu wa kuwepo ushirikiano baina ya wahandisi washauri na baadhi ya wahandisi waandamizi wakiwemo maprofesa waliweza kutoa ushauri wao pia.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko akizungumza wakati wa warsha iliyoandaliwa na Chama cha Wataalamu Washauri wa Wahandisi ‘Association of Consulting Engineers Tanzania’, (ACET) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

 Picha ya pamoja.

No comments: