Saturday, October 20, 2018

Tanzania, DRC Zaanza Mazungumzo Ujenzi wa Kinu/Kiwanda cha Kuchenjua Colbat

 Waziri wa Madini Angellah Kairuki na mgeni wake Waziri wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Martin Kabwelulu (wa pili kushoto) wakimsikiliza Mtaalam Mwelezi  Martin Sezinga Akiwaonesha mashine mbalimbali zinazotumiwa katika hatua mbalimbali za uzalishaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu katika mgodi wa mfano wa Lwamgasa.
PICHA 2- BUSOLWA
Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) na Waziri wa  Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Martin Kabwelulu wakiteta jambo baada ya kutembelea mgodi wa Busolwa Mining Ltd unaomilikiwa na Mtanzania, mkoani Geita
PICHA 3 KONGO TANZANIA
Meneja wa Mgodi wa Busolwa Mining Ltd, Flex Adoph akimweleza jambo Waziri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Martin Kabwelulu (katikati) wakati alipotembelea katika mgodi huo kujifunza namna mmiliki wa mgodi huo alivyotoka katika uchimbaji mdogo hadi kuwa mchimbaji wa Kati lakini pia kujifunza namna mgodi huo unavyofanya shughuli zake za uchenjuaji na uzalishaji wa madini ya dhahabu. Anayeshuhudia ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki.
PICHA 5 B
Waziri wa Madini wa  Angellah Kairuki na Mgeni wake Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Martin Kabwelulu (Wa tatu kushoto) wakiangalia madini ya Dhahabu yanayozalishwa na kuchenjuliwa katika Mgodi wa Nsangano Gold Mine mkoani Geita walipoutembelea mgodi huo.
PICHA 5, A, B
Waziri wa Madini Angellah Kairuki na mgeni wake Waziri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Martin Kabwelulu pamoja na ujumbe walioambatana nao wa Mkoa wa Shinyanga wakiangalia namna shughuli mbalimbali za uzalishaji wa madini ya Almasi  katika Mgodi wa Almasi Mwadui (WDL) zinavyofanyika.
PICHA 8
Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) Martin Kabwelulu wakiangalia Kitabu kinachotunza uzalishaji wa madini ya Almasi katika Mgodi wa Almas Mwadui (WDL) Kitabu hicho kina kumbukumbu za uzalishaji wa tangu mwaka 1958. Anayeshuhudi ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,  Zainab Tellack.
PICHA 9
Sehemu ya mitambo mbalimbali katika Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa. Mgodi huo umejengwa na Wizara ya Madini kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) kwa lengo la kutoa elimu ya uchimbaji wenye tija kwa wachimbaji wadogo, kutoa huduma na elimu kuhusu uchenjuaji  sahihi wa dhahabu. Mgodi huo umejengwa mkoani Geita.
PICHA 10
Waziri wa Madini Angellah Kairuki, mgeni wake  Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo uongozi wa Mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Kishapu na uongozi wa mgodi wa Almasi Mwadui wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuutembelea mgodi huo.
…………………………………………………………………………………
Asteria Muhozya na Rhoda James, GEITA
 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imeanza kufanya mazungumzo na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili iweze kujenga Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Colbat nchini.
 Hayo yalibainishwa Oktoba 19, mkoani Geita  na Waziri wa Madini wa Tanzania Angellah Kairuki wakati wa kuhitimisha ziara ya siku Nne ya  Waziri wa Madini wa Kongo (DRC), Martin Kabwelulu aliyoifanya nchini kwa mwaliko wa Waziri Kairuki.

Kairuki alisema kuwa, nchi ya Kongo ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini ya Colbat duniani ambapo asilimia 70 ya madini hayo duniani yanazalishwa nchini humo.Aliongeza kuwa, kwa sasa nchi hiyo inayo changamoto ya kusafirisha madini hayo yakiwa ghafi ikiwemo ukosefu wa umeme wa kutosheleza kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hivyo.

“Tumekubaliana kuendelea na mazungumzo  na Kongo ili shughuli za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini hayo ufanyike nchini  kwa kuwa tumeshaanza kuwekeza kwenye Vinu/viwanda  vya Kuchenjua na kuyeyusha madini mbalimbali. Hivyo, tunataka wayasafirishe makinikia ya Colbat hapa na tuyachenjue hapa,” alisisitiza Kairuki.

Akizungumzia matumizi ya madini hayo, Kairuki alisema kuwa, madini ya Colbat yanatumika kutengeneza betri na vihifadhi nishati (capacitor) ambazo zinahitajika sana hususan, kwenye magari yanayotumia umeme.bali na makubaliano ya ujenzi wa kiwanda hicho, pia Waziri Kairuki alisema kuwa nchi hizo zimekubaliana masuala kadhaa ikiwemo kuendelea kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa sekta ya Madini ili kuweza kunufaisha wananchi hasa wale wanaozunguka maeneo ya migodi.

“Nchi ya Kongo DRC imefurahishwa na hatua za Mkoa wa Geita kwenye usimamizi wa mapato yatokanayo na madini pia mchango wa migodi kwa maendeleo ya wananchi wanaozunguka mgodi,”alisema Kairuki.
Vilevile, alisema kuwa nchi hizo zimekubaliana kuboresha mahusianao ya kimkakati ambapo Kongo imeahidi kuiunga Mkono Tanzania katika masuala ya Mashtaka dhidi ya makampuni za uwekezaji.

Pia, alisema Kongo imeahidi kukitumia Chuo Cha Madini Dodoma (MRI) kupata mafunzo mbalimbali yanayohusu sekta ya madini yanayotolewa kituoni hapo;
“Kongo imepanga kuja kujifunza mfumo mpya wa utoaji wa leseni za madini (cadaster) ambao umebuniwa na kusanifiwa na watanzania,” alisema Kairuki.
Kairuki aliongeza kuwa, nchi hizo zimekubaliana kuendelea kuboresha mifumo ya udhibiti utoroshaji wa madini yanayotoka Kongo na Tanzania kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Aidha, Waziri Kairuki alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Kongo wenye nia ya kuwekeza nchini kwenye migodi, viwanda vya uchenjuaji, uongezaji thamani madini (ukataji, unga’rishaji).“Lakini pia tumewakaribisha kutumia bandari yetu kupitisha madini yao pamoja na kukubaliana kuwa na Mining Forum kati ya nchi hizi mbili tu ukiachia Forum nyingine ambazo tumelenga kuziandaa na kushirikisha wadau kutoka nchi mbalimbali,” alisema Kairuki.
Aidha,  alisema nchi hiyo imeahidi kurudi nchini  katika kipindi kifupi kijacho kwa ajili ya kujifunza zaidi kuhusu namna Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)  inavyofanya kazi zake za utafiti na maabara.

Kwa upande wake, Waziri wa DRC, Martin Kabwelulu alisema atawatuma Wataalam wake kurudi nchini kwa ajili ya kujifunza mfumo mpya wa utoaji wa leseni za madini (cadaster) wa Tanzania na kuongeza ni mfumo mzuri ambao utaliwezesha taifa hilo kusimamia vema rasilimali madini na kuhakikisha kwamba zinawanuifaisha wananchi wake.

Pia, alisema kuwa nchi hiyo inao ukosefu wa umeme wa kutosha jambo ambalo linafanya nchi hiyo kusafirisha madini hayo nje yakiwa ghafi ikiwemo madini ya Colbat na dhahabu na kuongeza kuwa, Rais wa nchi  hiyo, Joseph Kabila katika ujumbe wake amemweleza kuwa, anataka madini yote ya Kongo yasafirishwe kupitia Tanzania.

“Tunataka tusafirishe madini yetu kupitia bandari ya Tanzania. Lakini pia nimeona njia ya kupitishia madini yetu kupitia reli ya Kati ya Kigoma –Dar es Salaam ni fupi sana,” alisema Kabwelulu.Akizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanywa nchini humo hivi karibuni, alisema nchi hiyo iliamua kubadili sheria yake kutokana na kutokunufaika kabisa na rasilimali hiyo hususan kwa wananchi wanaozungukwa na  rasilimali hizo na kuongeza kuwa, sheria ya sasa inapigania zaidi maslahi ya nchi na wananchi wake.

“Nafurahi nimepokelewa vizuri sana Tanzania, nimejifunza mengi kweli hii ni nchi rafiki. Sisi tunao uzoefu wa miaka mingi kwenye sekta hii lakini bado hatujanufaika kabisa,” alisema Kabwelulu.Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi alisema kuwa, amemwomba Waziri wa Madini wa  Kongo kujenga kiwanda cha Colbat nchini kwa kuwa nchi hiyo iko jirani sana na mkoa huo na kwamba mkoa huo umejipanga kwa mazingira ya uwekezaji mkubwa.

Akiwa nchini, Waziri Kabwelulu alipata fursa ya kukutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini na Taasisi zake ambapo pande zote zilibadilishana uzoefu wa namna zinavyosimamia sekta ya madini, ikiwemo masuala ya uchimbaji mdogo wa madini.Aidha, Waziri Kabwelulu na mwenyeji wake Waziri Kairuki walitembelea Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa ambao umejengwa mahsusi kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) unaosimamiwa na wizara. Lengo la mgodi huo ni kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu uchimbaji sahihi  na uchenjuaji bora wa madini dhahabu. Pia, walitembelea migodi ya Wachimbaji wa Kati inayomilikiwa na watanzania ya Buswola  Mining Ltd na Nsangano Gold Mine mkoani Geita kujifunza walikotokea katika uchimbaji mdogo hadi kuwa wa Kati na pia walitembelea mgodi wa Almasi wa Mwadui (WDL) mkoani Shinyanga.

Ziara ya Waziri Kabwelulu nchini ililenga katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika masuala ya uendelezaji na usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwemo kuimarisha zaidi ushirikiano  uliopo baina  ya hizo mbili, kuangalia fursa za ushirikiano wa kibiashara na kiuwekezaji kupitia rasilimali madini madini, kubadilishana uzoefu kuhusu Mabadiliko ya Sheria  za  Madini yaliyofanywa na nchi hizi mbili hivi karibuni pamoja na kudumisha undugu na urafiki baina ya nchi hizo mbili.

No comments: