Sunday, October 21, 2018

MHAGAMA AAGIZA NEEC KUFANYA TATHIMINI YA UHALISIA WA WANUFAIKA WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA TAASISI ZA KIFEDHA

Na EmanuelMadafa,MichuziBlog,Mbeya 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu anayeshughulikia Sera,Bunge, Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kufanya tathamini ya wananchi walionufaika na mikopo iliyotolewa kwenye Taasisi za kifedha ili kubaini idadi halisi ya wananchi hao.

Ametoa kauli hiyo hii leo (Oktoba 20, 2018) wakati akifungua maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji na Vikundi vya Kifedha vya kijamii yaliyofanyika katika viwanja vya Nzovwe Mbeya ambapo yalijumuisha wajasiliamali kutoka Wilaya 15 za Mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.Amesema Lengo la kufanya tathimini hiyo ni kupata uhalisia wa wanufaika wa mikopo hiyo ili kuenenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekusudia kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025.

Aliongezea kuwa, tathimini hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya Serikali yao hususani wenye mtizamo hasi kuwa serikali haijafanya jambo lolote kuwawezesha kiuchumi.“Tathimini hii itasaidia kuwa na utaratibu mzuri wa kutunza takwimu sahihi zinazoonesha uhalisia wa wanufaika pia italeta chachu kwa kuhakikisha maonesho haya yanafanyika kwa mzunguko na kutoa fursa kwa wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini kufahamu mifuko na programu za uwezeshaji nchini”.Alisitiza Mhagama

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa aeleza kuwa ofisi yake itaendela kutekeleza kwa vitendo eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuyachukua maagizo ya waziri ili kuhakikisha malengo yaliyoainishwa yanafikiwa.Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe.Albert Chalamila alipongeza juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote wanawezeshwa kiuchumi na kujikwamua katika hali za umasikini na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

“Lazima tuendelee kuunga mkono jitihada za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vitendo na kuhakikisha changamoyo ya ajira kwa vijana inakomeshwa na kuwa na Taifa lenye maendeleo na wananchi wake”.Alisema Chalamila.Aidha, kaulimbiu ya maonesho ya Mwaka huu inasema “Vikundi vya Kifedha, Programu na Mifuko ya Uwezeshaji ni Chachu ya Maendeleo ya Viwanda”.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akisalimia wananchi walioshiriki katika maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji na Vikundi vya Kifedha vya kijamii (hawapo pichani) yaliyofanyika Oktoba 20, 2018. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akikata utepe wakati wa uzinduzi wa Programu ya malengo endelevu ya kuongeza ajira kwa vijana uliozinduliwa wakti wa maonesho hayo. 
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa akihutubia wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji na Vikundi vya Kifedha vya kijamii yaliyofanyika katika viwanja vya Nzovwe Mbeya Oktoba 20, 2018
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akipokea maelezo ya nyaraka zilizoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka kwa Mkurugenzi wa mifuko ya Uwezeshaji (NEEC), Bw.Edwin Chrisant wakati wa maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji na Vikundi vya Kifedha vya kijamii yaliyofanyika katika viwanja vya Nzovwe Mbeya Oktoba 20, 2018 
Baadhi ya wananchi wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa maonesho hayo. 

No comments: