Sunday, October 21, 2018

“SERIKALI KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZINAZOVIKABILI VYAMA VYA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO” -DKT TIZEBA

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisisitiza umuhimu wa SACCOS nchini wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Saccos Duniani hafla iliyofanyika katika viwanja vya kichangani Mkoani Iringa tarehe 18 Septemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Sehemu ya wanachama wa vikundi vya akiba na mikopo wakifatilia hotuba ya Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Saccos Duniani hafla iliyofanyika katika viwanja vya kichangani Mkoani Iringa tarehe 18 Septemba 2018.
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisalimiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Willium Vangimembe Lukuvi (Mb) mara baada ya kuwasili kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Saccos Duniani hafla iliyofanyika katika viwanja vya kichangani Mkoani Iringa tarehe 18 Septemba 2018.Na Mathias Canal, WK-Iringa

Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imeendelea kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vinaleta tija kwa jamii.

Hatua zilizochukuliwa na serikali ni pamoja na kuchukua hatua za kiutawala na kidola kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo waliojihusisha na wizi na ubadhirifu wa fedha katika vyama hivi, mfano; Alayabe SACCOS cha Karatu Mkoani Arusha, Mbinga Teachers SACCOS Mkoani Ruvuma na Ulanga Teachers SACCOS Mkoani Morogoro ambako baadhi ya viongozi na watendaji wamefikishwa mahakamani kwa vitendo vya ubadhirifu.

Vilevile, Kutengeneza mikakati ya kuhakikisha kwamba vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo haviendelei kutengeneza madeni yasiyokuwa na tija kwa jamii na kusaidia kuweka mikakati ya kupunguza madeni ambayo tayari yapo katika vyama vyetu vya ushirika wa Akiba na Mikopo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Saccos Duniani iliyofanyika katika viwanja vya kichangani Mkoani Iringa tarehe 18 Septemba 2018.

Waziri Tizeba alisema kuwa serikali imeanza kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na waajiri kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kuwahimiza waone umuhimu wa kuwasilisha kwa wakati makato wanayokata kutoka katika mishahara ya watumishi waliokopa katika SACCOS ili fedha hizo ziweze kutumika kwa shughuli za maendeleo zilizokusudiwa.

Alisema pia, serikali itaendelea kuendesha mafunzo mbalimbali kwa viongozi, watendaji na wanachama wa vyama vya ushirika vya Akiba na Mikopo ili waweze kufahamu miongozo na taratibu mbalimbali za utendaji wa vyama hivi ili hatimaye viweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa jamii inayozunguka.

Katika utafiti uliofanyika katika siku za hivi karibuni umebaini kwamba Tanzania ina jumla ya vyama vya ushirika vya Akiba na Mikopo 5640 kati ya vyama 55000 sawa na asilimia 10.3 ya vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo Duniani. Kwa mujibu wa utafiti huo, Tanzania ina jumla ya wanachama wapatao milioni moja na laki nane kwa SACCOS zote nchini kati ya wanachama milioni miambili (200) ya wanachama wote wa SACCOS sawa na asilimia 0.9 ya wanachama wa SACCOS zote Duniani. 

Dkt Tizeba alisisitiza kuwa Licha ya uchache wa wanachama wake ukilinganisha na idadi ya wanachama Duniani, SACCOS hapa nchini Tanzania zimeendelea kuwa msaada na mkombozi mkubwa katika kuondoa umasikini wa wanachama wa vyama hivi na jamii kwa ujumla wake.

Aidha, alisema Sekta ya ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) imeendelea kupanuka katika nchini kufuatia kuanzishwa kwa SACCOS nyingi katika maeneo ya mijini na vijijini hali ambayo imechangia kuongeza huduma ya kifedha kwa wananchi wa kawaida na hivyo kuleta tija kwa jamii.

Sambamba na hayo, alieleza kuwa uwepo wa maendeleo ya ushirika wa Akiba na Mikopo nchini umesaidia wanachama wengi kujijengea utamaduni wa kuweka akiba ya fedha mara kwa mara na kuwa na matumizi bora ya fedha wanazoweka akiba. Vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vimechangia kujenga tabia ya kujiamini na kuaminiana kifedha miongoni mwa wananchi wa kawaida na kujenga.

No comments: