Saturday, October 13, 2018

SERIKALI IPO TAYARI KUSAIDIA WAWEKEZAJI WA MADINI-NYONGO



Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ( wa kwanza mbele) akiendelea na ziara katika mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited uliopo katika kijiji cha Nkomolo II Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Meneja wa mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited, Jamhuri Mbamba (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) moja ya makaa ya mawe kwenye mgodi huo.
Meneja wa mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited, Jamhuri Mbamba (katikati) akielezea hali ya uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) katika ziara hiyo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (kulia) kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kabla ya kuanza ziara ya siku moja katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 12 Oktoba, 2018.



……………………….

Na Greyson Mwase, Sumbawanga

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo tayari kuwasaidia wawekezaji kwenye shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ili uchimbaji wao ulete manufaa kwa nchi.

Aliyasema hayo leo tarehe 12 Oktoba, 2018 mara baada ya kumaliza ziara yake katika mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited uliopo katika kijiji cha Nkomolo II Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Katibu Tawala Msaidizi – Sehemu ya Miundombinu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Happiness Shayo, Wataalam wa Madini, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na waandishi wa habari.

Alisema kuwa katika kuhakikisha watafiti na wachimbaji wa madini wanafanya kazi katika mazingira mazuri, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeanza kusogeza huduma zake kwa kuhakikisha kuwa inaanzisha ofisi za maafisa madini wakazi katika mikoa yote ambapo mkoa wa Rukwa unatarajiwa kupata ofisi kwa mara ya kwanza.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliushauri uongozi wa mgodi huo kujikita kwenye uzalishaji wa makaa ya mawe ambayo ni bora na kuuza katika nchi za jirani kwa kuwa mahitaji ya makaa ya mawe ni makubwa.

Aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanashirikiana na ofisi za wakuu wa wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika zoezi la usimamizi wa upakiaji wa madini kabla ya kusafirishwa ili kudhibiti mianya ya utoroshwaji wa madini mbalimbali.

Wakati huohuo Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji wa madini nchini kufuata kanuni na sheria za madini katika kuhakikisha kuwa wanalipa kodi stahiki serikalini ili fedha ziweze kuwanufaisha wananchi kupitia uboreshwaji wa huduma za jamii.

Awali akielezea hali ya uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa makaa ya mawe wa Edenville International (T) Limited, meneja wa mgodi huo Jamhuri Mbamba alisema kuwa, uzalishaji unazingatia mahitaji ya soko na kusisitiza kuwa kwa sasa mahitaji ni takribani tani 3000 kwa mwezi na kuendelea kusema kuwa mgodi unatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 15,000 za makaa ya mawe kwa mwezi.

Aliendelea kusema kuwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Oktoba 2018 jumla ya tani takribani 9941.78 za makaa ya mawe yalioshwa na kuuzwa kwa wateja wa ndani na nje ya nchi .Akielezea changamoto za mradi Mbamba alisema kuwa, awali lengo kuu la mradi lilikuwa ni uzalishwaji wa umeme lakini mchakato wake umekuwa ukichukua muda mrefu pasipo mafanikio.

Alisema hadi sasa maongezi kati ya kampuni na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yamekuwa yakiendelea kwa kipindi kirefu na kwa sasa kampuni inaandaa zabuni kama ilivyoainishwa hapo awali.

Aliongeza kuwa pia mradi ulilenga ujenzi wa njia ya umeme ya Mbeya hadi Kigoma hadi Nyakanazi ambao haujaanza kujengwa.

No comments: