Saturday, October 13, 2018

MABORESHO YA MIUNDOMBINU YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MBARALI YAWANUFAISHA WAKULIMA



Katika Picha Mhandisi Elibariki Mwendo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akizungumza kuhusu maboresho yaliyofanywa katika banio (halipo pichani) lililopo katika chanzo cha maji cha mto Mbarali kinachopeleka maji katika skimu ya umwagiliaji ya Igomelo, nyuma pichani ni mto Mbarali.
Bibi Victoria Kinyega akifanya kazi ya kuchambua vitunguu katika skimu ya umwagiliaji wa Igomelo.
Vijana wanaofanya kazi katika shamba la vitunguu kwenye skimu ya Igomelo iliyopo Mbarali Mkoani Mbeya wakijaza vitunguu katika gunia maarufu kwa jina la net, tayari kwenda sokoni kuuzwa.
Kulia Afisa Kilimo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kanda ya Mbeya, Bw. Mnadi Taribo akimuelezea mgeni aliyetembelea shamba la mpunga katika skimu ya Umwagiliaji Igomelo, kuhusu teknolojia ya kisasa ya kilimo cha mpunga inayotumia kiasi kidogo cha maji, yaani kilimo shadidi.
moja ya ghala la kuifadhia vitunguu linalotumiwa na wakulima katika skimu ya umwagiliaji ya Igomelo.
Miundombinu inayopeleka maji katika mashamba ya mazao ya mbogamboga na mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Igomelo.



Imeelezwa kuwa maboresho ya miundombinu ya skimu ya kilimo cha umwagiliaji ya Igomelo iliyopo wilayani Mbarali Mkoani Mbeya, imewanufaisha kwa namna mbalimbali wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha mbogamboga. 

Hayo yameelezwa jana na Mhandisi wa kanda ya Mbeya wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Elibariki Mwendo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea skimu hiyo.

Mhandisi Mwendo alisema kuwa, Serikali imetumia kiasi cha shilingi Milioni mia mbili hamsini (250Milioni) kukarabati miundombinu ya skimu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa banio kubwa linalotoa maji katika chanzo cha maji cha mto Mbarali na mifereji inayopeleka maji mashambani.

“katika skimu hii wakulima wanajikita zaidi katika kilimo cha mbogamboga kama vile vitunguu, nyanya, matango, na hata zao la mpunga, ambapo kabla ya marekebisho na maboresho ya miundombinu hii, hali haikuwa nzuri kwani wakulima walikuwa wanajichotea maji kiholela ili kuweza kumwagilia mazao yao, lakini kwa sasa kama mnavyoona, maji yanakwenda moja kwa moja mashambani kwa utaratibu maalum ulivyopangwa ambapo kila mkulima ana zamu yake ya kuingiza maji mashambani tayari kwa kilimo, jambo ambalo limepelekea wakulima hawa kuongeza uzalishaji katika mazao wanayolima na kujiongeza pato la familia.” Alisisitiza Mhandisi Mwendo.

Mmoja wa wakulima wanaojishughulisha na zao la kilimo cha vitunguu katika skimu hiyo Bw. Yohana Mbuna (52) amesema amekuwa akijishughulisha na kilimo katika skimu hiyo kwa takribani miaka ishirini sasa, “ Kabla ya maboresho katika skimu hii hali ilikuwa mbaya kwanza tulikuwa tunalima bila kufuata utaratibu, tulikuwa tunagombania maji na hata mavuno hayakuwa mengi kwa heka moja nilikuwa napata magunia 30 lakini kwa sasa kwa heka moja ninaweza kupata zaidi ya magunia 100 na hii hunisaidia kupata fedha za kusomesa watoto wangu, na ninalima vitunguu kama zao la biashara, pamoja na hilo mazao mengine ya chakula kama mpunga ninalima kwa ajili ya familia yangu.” Alisema Bw. Mbuna.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Umwagiliaji kanda ya Mbeya Mnadi Taribo amesema kupitia Mradi wa kuwajengea Uwezo wataalam na wakulima Tanzania Capacity Building for Irrigation Development (TANCAID) wakulima wameweza kupata Elimu kuhusu mafunzo matumizi sahii ya maji katika kilimo hususan kilimo cha mpunga kitaalam kilimo shadidi , usimamizi bora wa maji na kanuni sahihi za kilimo.

Aliongeza kwa kusema kuwa sambamba na hilo, kupitia mradi uliopita miaka miwili nyuma wa (PHRD) Policy Human Resouce Development uliofadhiliwa na Bank ya Dunia, pamoja na wakulima kupatiwa mafunzo pia walipata vifaa vya kuvunia mazao kama vile Mpunga, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao yao na mashine za kukobolea zao la mpunga, jambo ambalo limesaidia pia vijana wengi kupata ajira na wakulima kujua matumizi sahihi ya maji, kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza thamani ya mazao.

Akiongelea changamoto ya wadudu aina ya onion thrips wanaoshambulia zao la vitunguu na kusababisha mnyauko, Bw. Taribo amesema kuwa serikali imeshafanya jitihada ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuchukua sampuli za wadudu hao na kupeleka katika chuo cha Kilimo Uyole kwa ajili ya kufanyia tafiti.

Awali imeelezwa kuwa kanda ya kilimo ya mbeya inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Songwe ina jumla ya ukubwa wa Hekta laki 268,350 ambapo Hekta 66,974 zimeendelezwa na Hekta 201,376 hazijaendelezwa na zipo kwenye mpango kabambe wa kitaifa wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji unaolenga kuendeleza hekta milioni moja (1,000,000,) katika awamu ya kwanza ya 2020 mpaka 2025 na awamu ya pili ya 2025 - 2035.

No comments: