Saturday, October 13, 2018

UWEKEZAJI KATIKA ELIMU SULUHISHO LA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI AFRIKA



Na. WFM, Bali Indonesia

Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinatakiwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye maarifa na elimu ili kuendana na soko la ushindani linaloendelea kwa kasi Duniani

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni mwakilishi wa Tanzania katika Bodi ya Magavana wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Dkt. Philip Isdor Mpango, wakati wa mikutano ya WB na IMF mjini Bali Indonesia.

Dkt. Mpango alisema kuwa, katika mikutano hiyo ya Kimataifa yapo mambo ambayo Tanzania inatakiwa kuyafanyia kazi wakati huu ambao inapiga hatua kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda ambapo elimu inayotolewa inatakiwa kujikita katika kukuza maarifa na ujuzi .

“Wakati suala la teknolojia likiangaziwa katika bara la Afrika ni vema kuangalia pia namna ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na teknolojia hiyo kwa kuwa katika maeneo mengi ajira za watu zimepungua kutokana na mashine kuchukua nafasi za watu”, alisema Dkt. Mpango.

Alisema mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa imekua na umuhimu mkubwa kwa kuwa wadau wamebadilishana mawazo ambayo yamelenga kukabiliana na changamoto za kiuchumi ambazo zimeendelea kutokea Duniani ikiwa ni pamoja na baadhi ya nchi kuwa juu kiuchumi na nyingine kuendelea kuporomoka kwa kasi. 

Katika mikutano hiyo Tanzania imetajwa kuwa uchumi wake unaendelea kuimarika ambapo kwa sasa unakua kwa takribani asilimia sita hivyo kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na Dunia kwa ujumla.

Wajumbe wa mikutano hiyo wametakiwa pia kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabia nchi katika nchi zao kwa kuwa yanaathari kubwa katika uchumi hasa katika Sekta ya afya kutokana na kuongezeka kwa magonjwa lakini pia mafuriko na ukame.

Naye Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Rubuka, alisema kuwa suala la amani duniani limejadiliwa kwa kina katika mikutano hiyo kwa kuwa ni chachu ya maendeleo si tu ya kiuchumi lakini pia ya kijamii.

Mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa inaendelea Mjini Bali Indonesia, ambapo imewakutanisha Mawaziri, Magavana na wadau wa masuala ya Fedha na Uchumi kutoka nchini mbalimbali duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Mjini Bali Indonesia

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Benki ya Dunia (WB,) anayewakilisha Afrika (Africa group 1 constituency), Bi. Anne Kabagambe, wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayoelendelea mjini Bali Indonesia, kushoto kwake ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).
Wajumbe wa Benki ya Dunia (WB) kundi la Afrika (Africa group 1 constituency), wakiwa katika Mkutano Mjini Bali Indonesia.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wa pili kulia, akijadili jambo na Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoelendelea mjini Bali Indonesia.
Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Ushauri wa Masuala ya Fedha wa Benki ya Dunia- WB kwa nchi za Afrika (Africa group 1 constituency) Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisoma ujumbe wa nchi hizo, wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoelendelea mjini Bali Indonesia (kushoto ) ni  na Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Mjini Bali Indonesia)

No comments: