Halmashauri
za Wilaya ya Msalala, Shinyanga (Shinyanga) Nyang'hwale (Geita),
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (kupitia Wizara ya Maji na
Umwagiliaji) na Wadau wa Maendeleo ambao ni ACACIA Mining PLC (kupitia
Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu) wamesaini hati za makubaliano ya
kisheria kutekeleza Mradi wa Pamoja wa Maji ujulikanao kama JOINT WATER
PARTNERSHIP PROJECT (JWPP).
Akizungumza
jana wakati wa kutia saini makubaliano hayo (Legal Agreement) kijiji
cha Ilogi halmashauri ya Msalala, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa
Kitila Mkumbo amesema katika mradi huo sehemu kubwa ya fedha za mradi
zimetolewa na Serikali kupitia wizara ya maji na ACACIA Bulyanhulu Gold
Mine Ltd ambapo pia halmashauri hizo tatu zinachangia kiasi cha fedha
kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mradi huo kutoka katika
makusanyo yake ya ndani.
Mradi huu utanufaisha jumla ya vijiji kumi na nne (14) kutoka katika Halmashauri za Wilaya tatu ambapo kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga vijiji viwili ambavyo ni Mwenge na Mahando vitanufaika na mradi huo.
Kwa
upande wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang'hwale vijiji 6 ambapo ni
Nyugwa, Mwamakiliga, Izunya, Kharumwa, Kafita na Lushimba vitanufaika
kupitia mradi huo na kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Msalala pia ni Vijiji 6 ambavyo ni Kakola Na. 9, Lwabakanga, Bushing'we, Kakola, Bugarama na Ilogi.
Profesa Mkumbo amesema Utekelezaji wa Mradi huu umegawanyika katika Awamu mbili.
Awamu
ya kwanza ambayo inahusisha utandazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji
kutoka bomba kuu la KASHWASA katika Kijiji cha Mhangu (Halmashauri ya
Wilaya ya Shinyanga) hadi Tanki la kuhifadhia maji katika kijiji cha
Ilogi (Halmashauri ya Wilaya ya Msalala) Bomba hili kuu la kusafirisha
maji yaani Mhangu - Ilogi.
Amesema
Transmission Main ni la chuma na lina urefu wa kilimita 58.5 na vipenyo
kati ya milimita 110 hadi milimita 400; zikiwemo bomba za matoleo
kuwezesha usafirishaji wa maji kwenda kwenye vijiji 14 vitakavyonufaika
na mradi huo. Utekelezaji wa shughuli za Mradi katika Awamu ya Kwanza
umekwishaanza.
Amesema
Awamu ya pili ya Mradi itahusisha ujenzi wa matanki mapya 11 ya maji
yenye ujazo kati ya lita 45,000 hadi lita 900,000 pamoja na utandazaji
wa bomba za mfumo wa usambazaji maji katika vijiji vyote 14 vilivyotajwa
hapo juu. Utekelezaji wa shughuli za Mradi Awamu ya pili bado
haujaanza.
Kuhusu Mkandarasi wa Utekelezaji wa Shughuli za Mradi Awamu ya Kwanza,amesema,
utekelezaji wa shughuli za mradi kwa Awamu ya Kwanza unafanywa na
Mkandarasi, Kampuni ya Kichina inayoitwa M/s. Beijing Construction
Engineering Group (BCEG) Co. Ltd ambapo muda wa mkataba ni miezi kumi na
mbili (12).
Mkumbo
pia amebainisha kwamba Msimamizi wa Shughuli za Ujenzi wa Mradi Awamu
ya Kwanza ni Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza
(MWAUWASA), na kwamba awamu ya Kwanza ya Utekelezaji wa Shughuli za
Mradi huu inatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni
13,860,873,200.
Mchanganuo
wa uchangiaji wa Serikali pamoja na Wadau wa ACACIA Bulyanhulu Gold
Mine Ltd katika gharama za mradi kwa upande wa serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji imechangia TSH 4,000,000,000/=, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala TSH 600,000,000/=,Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale TSH 600,000,000/= na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga TSH 40,000,000 na ACACIA Bulyanhulu Gold Mine Ltd USD 2,000,000.
Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo akitia saini hati za makubaliano hayo (Legal Agreement) kutekeleza Mradi wa Pamoja wa Maji ujulikanao kama JOINT WATER PARTNERSHIP PROJECT (JWPP).
Wa kwanza kulia ni Meneja Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi,Benedict Busunzu.
Viongozi wa ACACIA na Serikali wakitia saini hati za makubaliano hayo (Legal Agreement).
Viongozi wa ACACIA na Serikali wakielekea katika kijiji cha Ilogi halmashauri ya Msalala ambapo bomba la maji litapita.
Katibu
Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo akishiriki kuchimba mtaro
katika eneo la Kijiji cha Bushing'we halmashauri ya Msalala ambapo bomba
la maji litapita.
Meneja Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi,Benedict Busunzu akishiriki kuchimba mtaro katika eneo la Kijiji cha Bushing'we halmashauri ya Msalala ambapo bomba la maji litapita.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo akizungumza baada ya kusaini hati za makubaliano ya kisheria kutekeleza Mradi wa Pamoja wa Maji ujulikanao kama JOINT WATER PARTNERSHIP PROJECT (JWPP).
Meneja
Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi,Benedict Busunzu akizungumza
baada ya kusaini hati za makubaliano ya kisheria kutekeleza Mradi wa
Pamoja wa Maji ujulikanao kama JOINT WATER PARTNERSHIP PROJECT (JWPP).
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha akizungumza.
PICHA NA MPIGA PICHA WETU
No comments:
Post a Comment