Saturday, October 20, 2018

KAMISHNA MKUU WA TRA AFUNGUA FAINALI ZA MASHINDANO YA VILABU VYA KODI

Na Veronica Kazimoto -Dar es Salaam

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amefungua fainali za mashindano ya kumi na moja (11) ya vilabu vya kodi katika Shule za Sekondari za Mikoa ya Dar es salaam na Pwani yaliyofanyika leo katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati akiwahutubia wanafunzi na wageni waalikwa, Kichere amesema lengo la mashindano hayo ni kuwafundisha wanafunzi uzalendo na kukuza uelewa wao juu ya masuala mbalimbali ya kodi ili waweze kuelewa umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari. "Haya mashindano yanafanyika kama sehemu ya kujenga uzalendo kwa wanafunzi wetu ili waweze kuelewa umuhimu wa kulipa kodi na hatimaye waweze kulipa kodi kwa hiari maana tunasema samaki mkuje angali mbichi," alisema Kichere.

Ameongeza kwa kusema kuwa, "Sisi Mamlaka ya Mapato Tanzania tunasema kwamba elimu ndio kitu muhimu sana kwasababu watu wakielewa umuhimu wa kulipa kodi, tutakusanya kodi nyingi zaidi ambazo hutumika katika kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, utoaji wa elimu bure, uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, mabweni, nyumba za walimu na ununuzi wa vifaa vya maabara na kufundishia."

Aidha, Charles Kichere amebainisha kuwa, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali inafanya mpango wa kuingiza mtaala wa somo la kodi kuanzia Shule za Msingi hadi vyuoni ili kujenga uzalendo wa kulipa kodi kwa hiari nchini. Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha vilabu vya kodi mwaka 2008 na mpaka sasa kuna jumla ya vilabu 226 Tanzania Bara vikiwa na jumla ya wanafunzi 27,250 ambao ni wanachama hai wa vilabu hivyo.

Mashindano ya mwaka huu yameshindanisha jumla ya shule 50 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo shule 28 zimeingia fainali zikiwa zimegawanyika katika makundi mawili, shule 18 zinashindana katika kujibu maswali wakati shule 10 zinashindana kuwasilisha mada mbalimbali zinazohusu kodi. 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akiwahutubia wanafunzi na wageni waalikwa wakati wa ufunguzi wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa mwaka 2018 wa Shule za Sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani uliofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.
Jopo la majaji likifuatilia na kutoa alama kwa makundi ya wanafunzi wanaojibu maswali mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa mwaka 2018 yaliyofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wanafunzi wa shule za Sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (hayupo pichani) wakati wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa mwaka 2018 yaliyofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Zanaki Salma Mtanda akiwasilisha mada kuhusu mapato yatokanayo na uwekezaji wa rasilimali wakati wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa mwaka 2018 yaliyofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Zanaki Salma Mtanda akiwasilisha mada kuhusu mapato yatokanayo na uwekezaji wa rasilimali wakati wa fainali za mashindano ya vilabu vya kodi kwa mwaka 2018 yaliyofanyika katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) Jijini Dar es Salaam.

No comments: