Saturday, October 20, 2018

IGP SIRRO AELEZA HATUA KWA HATUA NAMNA MO DEWJI ALIVYOPATIKANA...INASIKITISHA

*Atangaza msako mkali kuwasaka watekaji,agusia walivyotaka kuchoma gari kupoteza ushahidi 
*Silaha ya kivita,bastola zakutwa ndani ya gari ya watekaji ,atoa onyo kali


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

JESHI la Polisi nchini limesema baada ya mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji 'MO' kupatikana, kwa sasa linaendelea na uchunguzi na msako mkali kuwakamata watekaji.

Akizungumza mchana huu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amewaambia Watanzania leo kupitia vyombo vya habari kuwa MO yupo salama na kwa sasa wao ndio uchunguzi kama umeanza upya kubaini watekaji na lazima wapatikane aidha wakiwa hai au wamekufa.

 Amesema wametoa taarifa za tukio hilo kwa nchi jirani,hivyo waliohusika na utekaji huo wajue hawana pa kukimbilia kwani kokote watakaoenda watapatikana tu.

Pia amesema watekaji hao baada ya kumtupa mfanyabiashara huyo katika viwanja vya Gymkhana barabara ya ya Ghana jirani na Ubalozi wa Denmark walitaka kulichoma moto gari waliyoitumia yenye namba za usajili T 314 AXX lakini kwenye vioo vya pembeni kukiwa na namba za usajili AGX 404 MC yenye rangi ya blue nyeusi na ufito wa rangi ya shaba kwa chini kwa lengo la kupoteza ushahidi lakini hawakufanikiwa.

"Jeshi la Polisi linaendelea na msako kuhakikisha waliokuwa wamemteka mfanyabiashara huyo wanapatikana," amesema IGP Sirro na kusisitiza Jeshi la Polisi litahakikisha linafanikiwa kuwapa wahusika wa tukio hilo.

NAMNA MO ALIVYOPATIKANA 

IGP Sirro amesema kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu Alhamisi ya Oktoba 10 mwaka huu ,anaufahamisha umma kuwa MO amepatikana akiwa mzima wa afya usiku wa kuamkia Oktoba 20 baada ya kutekelezwa na watekaji eneo hilo la Gymkhana.

Amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa baada ya kutekwa mfanyabiashara huyo alifungiwa kwenye nyumba ambayo bado haijajulikana na kufungwa miguu na mikono huku wakimziba macho.

Ameongeza uchunguzi wa awali umebaini kuwa watekaji hao walitumia gari aina ya Toyota Surf yenye namba za usajili T 314 AXX lakini kwenye vioo vya pembeni ilikuwa na namba AGX 404 MC yenye rangi ya blue nyeusi.

 ATOA PONGEZI KWA SERIKALI, MO ,WANANCHI

Wakati huo huo IGO Sirro ametoa pongezi kwa Serikali,vyombo vya ulinzi na usalama, familia ya Mohamed Dewji ,waandishi wa habari na wananchi wote kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kipindi chote ambacho mfanyabiashara huyo alikuwa ametekwa kwa jitihada walizofanya hadi kufanikiwa kumpata.

"Ninawaomba muendelee kushirikiana nasi kwa kutupatia taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa watuhumiwa wote wa tukio hili ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.Bahati nzuri watuhumiwa wamelitelekeza gari walilotumia kutekeleza azma yao mita chache kutoka eneo alipotelekezwa mfanyabiashara huyo.

" Ukaguzi wa kina wa gari hilo umefanyika na umewezesha kupatikana kwa bunduki aina ya AK 47 moja na risasi zake 16 ,bastola aina ya Glock 19 ikiwa na risasi 13, bastola aina ya P.Bereta ikiwa na risasi 3 na Gas Pistol 4.5 mm.Nitaendelea kuwapa taarifa kadri maendeleo ya upelelezi yatakavyokuwa yakipatikana,"amesema Sirro.

NAMNA MO ALIVYOOMBA MSAADA WA ASKARI

IGP Sirro pia amesema taarifa za kupatikana kwa MO zilitolewa na  askari wa getini katika eneo hilo la  Ghykhana  baada ya MO kumuomba askari huyo kutoa taarifa kwa  familia yake ndipo walipofika eneo hilo.

"Baada ya kuja katika eneo hilo ndipo walipotujulisha Polisi na hivyo tukafika eneo la tukio na kujiridhisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo Dewji."Ilikuwa saa saba usiku  maeneo ya Gymkhna  gari iliyohusika na utekaji huo lilitelekezwa aina ndani yake likiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji," amesema.


MAZUNGUMZO KATI YAO NA MO

Pia IGP Sirro amesema baada ya kufanya mazungumzo na Mo Dewji amewaeleza waliomteka walikuwa wanazungumza lugha ya kingereza na mmoja lugha ya Kiswahili cha hovyo.

Kwa mujibu wa kamanda sirro amesema Mo aliwaeleza kuwa baada ya kumteka walitaka atoe fedha ambapo aliwaeleza yeye alikuwa hana hela na badala yake aliwaeleza awape namba za simu za baba yake.

Amesema hata walipopewa na za simu za baba yake hawakumpigia kwani  waliogopa mtego wa Polisi.

ATOA ONYO KALI

Wakati huo huo IGP Sirro  ametoa onyo kali kwa kikundi cha baadhi ya watu ambao wanaingilia utendaji kazi  wa Jeshi la Polisi kupitia mitandao ya kijamii.

" Kuna kikundi ambacho chenyewe kipo kwa ajili ya kuingili majukumu ya Polisi.Jamani Polisi wanafanya kazi usiku kucha tena wakipita kukagua katika kila eneo na kwamba wenyewe wamelala na wake zao lakini kazi yao kuingilia kazi za Polisi."amesema  Sirro na kuwaonya wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kutika viwanja vya Gymkhana,jijini Dar kuhusiana na tukio la kupatikana Mfanyabiashara Mohammed Dewji a.k.a MO

No comments: