Thursday, October 18, 2018

MPINA AWATAKA VIONGOZI WOTE WA SERIKALI KUSHIRIKI KIKAMILIFU KWENYE ULINZI WA RASLIMALI ZA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikata utepe kufungua Mnada wa Kimataifa wa Mifugo Kirumi ulioko wilayani Butiama mkoani Mara juzi, wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima{kushoto},Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi}kulia} na Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akifunua kitambaa katika jiwe la msingi la ufunguzi wa Mnada wa Kimataifa wa Mifugo Kirumi ulioko wilayani Butiama mkoani Mara juzi, wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima{kulia} na Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel }kushoto}.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyenyanyua mkono akiwa na Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel (kulia kwake) wakati wa ufunguzi wa Mnada wa Kimataifa wa Mifugo Kirumi ulioko wilayani Butiama mkoani Mara juzi. Picha na Mpiga Picha Wetu


NA JOHN MAPEPELE, MARA

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewataka viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi za vijiji,wilaya kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali za mifugo badala ya hali ilivyo sasa ya kuiacha ikitoroshwa kwenda nchi za nje kwa kuamini kwamba jukumu la ulinzi wa rasilimali hizo ni la Wizara ya Mifugo na Uvuvi peke yake na ikosesha serikali mapato.

Waziri Mpina ameyasema hayo wakati akizundua mnada wa mpakani wa Kimataifa wa Mifugo katika eneo la Kirumi Wilayani Butiama mkoani Mara ambapo ameagiza kufungwa kwa minada yote ya mifugo iliyofunguliwa kinyemela kwani imekuwa kichocheo cha upotevu wa mapato wa Serikali na kuonya wanaoanzisha minada hiyo bila kufuata taratibu zilizopo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Aidha amemuagiza Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel kuanza mara kuihakiki minada yote iliyopo nchini ili kuibaini ambayo imeanzishwa kinyume cha sheria iweze kufutwa.“wako watu wanafungua minada kila sehemu wanaamua tu wakati taratibu za ufunguzi wa minada wanazijua kabisa ya kwamba ni lazima wizara iridhie kufunguliwa kwa mnada huo”alisisitiza Waziri Mpina

Amesema Serikali inapotaka kuanzisha mnada inakuwa na malengo ya kuhakikisha biashara ya mifugo inafanyika vizuri na kwamba uanzishaji holela wa minada unadhoofisha mipango inayowekwa na Serikali jambo ambalo haliwezi kukubalika.

Naye Katibu Mkuu Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel alisema kufunguliwa kwa mnada huo kutasaidia usimamizi na kudhibiti utoroshaji wa mifugo na kuongeza mapato ya Serikali ambapo amesema mnada wa Kirumi umewekwa kimkakati na unatarajia kuvuta wafanyabiashara wa mifugo kutoka katika nchi za jirani na kuliingizia taifa mapato makubwa.

Waziri Mpina amewataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanapanga matumizi bora ya ardhi na kuwawezesha wafugaji kupata huduma zinazostahili ikiwemo malisho na maji badala ya hali ilivyo sasa ambapo kila kiongozi anaona mifugo ni laana kwa taifa.Pia Waziri Mpina pia alimuagiza Katibu Mkuu Mifugo kuanzisha haraka ofisi itayotoa huduma ya vibali kwa watu wanaotaka kusafirisha mifugo nje ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyabishara hao hulazimika kwenda hadi jijini Mwanza kufuatilia vibali hivyo.

Ameagiza kupelekwa kwa mitungi ya kupandikiza mbegu bora ya mifugo katika Mkoa wa Mara na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa gharama isiyozidi sh 5,000 tofauti na ilivyo sasa ambapo hulazimika kugharamia hadi sh, 100,000 kupata huduma hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema Serikali ngazi ya mkoa huo itaendelea kuwachukulia hatua kali watu wote wataoshiriki vitendo vya utoroshaji mifugo nje ya nchi huku akiwaonya watu wanaondeleza vitendo vya wizi wa mifugo kwamba hawatapata tena nafasi katika kipindi hiki cha utawala wa Serikali ya awamu tano.

Malima alisema tayari mkoa huo umepokea mwekezaji wa kiwanda cha maziwa kitakachokuwa na uwezo wa kusindikiza tani 200,000 kwa siku na kusema kuwa itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wafugaji wa mkoa huo kupata soko la uhakika la maziwa yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Mara, Mrida Mshoja amesema ngombe zilikuwa zinatoroshwa kwenda Kenya na kwamba kufunguliwa kwa mnada huo kutawezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao na kumshukuru Waziri Mpina kwa kufanikisha azma ya kuanzisha mnada huo.

No comments: