Thursday, October 18, 2018

KLINIKI YA HEAMEDA ILIYOPO BUNJU B DAR YAWEKA KAMBI KUPIMA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA


*Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo Dk. Mwandolela azungumzia mfumo wa maisha unavyochangia

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KLINIKI ya Magonjwa ya Moyo Heameda iliyopo Bunju B jijini Dar es Salaam imeanzisha kambi maalumu ya siku mbili kwa lengo la kupima na kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo huku ikielezwa sababu za kuongeza kwa magonjwa hayo ni mfumo wa maisha.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Mkurugenzi wa Kliniki hiyo ambaye pia ni Daktarii Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Dk. Hery Mwandolela amesema watatoa huduma hiyo kwa siku tatu kuanzia leo, kesho na keshokutwa watafunga rasmi ambako mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Reginald Mengi.

Amesema kuwa wameamua kutenga siku hizo kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kwa wananchi mbaliimbai ambao wamefika kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na kwamba uamuzi huo ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii ya Watanzania.

“Tunatoa mwito kwa wananchi waje wapime afya zao bure, Heameda tumeamua kutoa huduma ya matibabu kama sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi wote.Hivyo kwa mwaka huwa tunatenga siku maalumu za kuwa na kambi hiyo.Kwa leo waliofika hadi saa saba mchana ni watu zaidi ya 130 na wanaendelea kuja.Nasi tunawakaribisha maana tupo kwa ajili ya kuwahudumia,”amesema Dk.Mwandolela.

Kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini amesema kasi imekuwa kubwa sana na takribani kwa miaka 30 hali inazidi kuwa mbaya hasa katika magonjwa ya kupanda kwa shinikizo la damu, sukari na saratani.”Mfumo wa vyakula tunavyokula na kutofanya mazoezi ni moja ya sababu kubwa ya magonjwa hayo.Pia msongo wa mawazo nao umechangia kuongeza kwa ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu,”amefafanua.

Dk.Mwandolela amesema katika kila watu wazima watu watatu kati yao wanakuwa na ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu na kwamba mtu anapokuwa na shinikizo la damu la kupanda kwa muda mrefu anakuwa na uharibifu wa mifumo ya mwili haswa macho, uono unakuwa mdogo au kupata upofu, kufeli kwa figo na moyo na magonjwa ya kiharusi.

Akifafanua kuhusu msongo wa mawazo amewashauri Watanzania kupanga malengo ambayo yanaendana na uwezo wao badala ya kuwaza mambo makubwa ambayo mwisho wake yanasababisha mhusika kupata ugonjwa wa shinikizo la damu. 

Ameeleza umuhumu wa watu kupima afya zao mara kwa mara kwani uchunguzi unapofanyika mapema na wakibaini viashiria vya magonjwa hayo wanaweza kuchukua hatua kabla havijafikia hatua ngumu ya kutibika au kufikia hatua ya gharama kubwa kutibika.

Kuhusu watu ambao wamefikia kwenye Kliniki hiyo na kupata vipimo wengi wao wamegundulika na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu na wamewapatia dawa na ushauri.

Wakati huo huo Meneja Masoko wa The International Eye, Claudius Katundu amesema wameshirikiana na Heameda kwa kutoa huduma ya uchunguzi wa macho na kwa wale ambao wamebainika kuwa na matatizo wamepata matibabu.

Kwa upande wa baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma za uchunguzi wa afya katika Kliniki ya Heameda akiwamo Mkazi wa Mabwepande Amanyisye Mwakasyuka ameshukuru huduma ambazo amezipata na kutoa ombi ka wananchi kupima afya zao. 

Naye Mkazi wa Bunju B Kitunda jijini Dar es Salaam Anna Mihambo amesema huduma za wananchi kupima afya zao ni muhimu na ametoa shukrani kwa uongozi wa Heameda kwa kutambua kurudisha shukrani kwa vitendo.

“Kufa kupo tu na binadamu lazima ipo siku tutakufa, hivyo ni vema tukapima afya zetu mara kwa mara na pale unapobaini kuna tatizo basi unapata huduma za tiba mapema,”amesema.Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo . Dk. Henry Mwandolela wa Heameda Madical Clinic akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali yake iliyoko Bunju B jijini Dar es salaam wakati wa kambi ya siku mbili ya uchunguzi wa Magonjwa mbalimbali inayofanyika hospitalini hapo kuanzia saa mbili asubuhi mpaka jioni , Kiliniki hiyo itafungwa rasmi ziku ya jumamosi 
Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo . Dk. Henry Mwandolela wa Heameda Madical Clinic akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa kiliniki hiyo.
Baadhi ya madaktari wakiendelea kutoa huduma kwa wananchi mbalimbali waliokwenda kupata huduma ya matibabu.
Bwana Claudius Katundu wa Ofisa Uhusiano wa The International Eye Hospital akiwaelezea waandishi wa habari kuhusu huduma za Macho wanazozitoa.
Zacharia Sanga Ofisa Utawala Heameda Medical Clinic kulia na Dk Isack Maro wakijadiliana jambo wakati kambi hiyo ikiendelea hospitalini hapo. 
Baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo wakitoa huduma kwa wananchi waliofika katika kambi hiyo.
Picha mbalimbali zikionyesha wananchi mbalimbali wakipata huduma wakati wa kambi hiyo.
  
Baadhi ya wananchi wakisuburi huduma wakati kambi hiyo ikiendelea kwenye hospitali ya Heameda Medical Clinic.

No comments: