Thursday, October 18, 2018

RC GAMBO:MTUMISHI ALIYECHUKUA PESA ZAIDI(YA MWANANCHI) YA KUUNGANISHA UMEME AIREJESHE HARAKA

Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi Theresia Mahongo wakipata maelezo kutoka kwa wahandisi wa TARURA wilaya ya Karatu juu ya maendeleo ya ujenzi wa daraja la Getamong wilayani humo. Picha na Vero Ignatus
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Karatu Edward Mwakapaju akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo juu ya hali ya utekelezwaji wa mradi wa umeme vijijini REA wilayani humo.Picha na Vero Ignatus
Wananchi wa eneo la Kilimamoja wilayani Karatu wakiwa katika mkutano wa hadhara kutoa kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo. Picha na Vero Ignatus 

Na. Vero Ignatus, Karatu. 

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemwagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)Wilaya ya Karatu, Edward Mwakapaju kuhakikisha mtumishi wa shirika hilo aliyechukua pesa kiasi cha Sh. 70,000/= kwa mmoja kati ya mwananchi wa eneo la Mang'ola badala ya Sh. 27,000/= za kuunganishiwa umeme wa REA kuzirudisha mara moja.

Gambo  amesema kuwa haridhishwi na kasi ya usambazwaji umeme unaofanywa na Kampuni ya NIPO Group Ltd kwenye vijiji na vitongoji mbalimbali vya wilaya hiyo na kumpa agizo Meneja wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Henry Mhina kuhakikisha anachukua hatua ili wananchi waweza kuunganishiwa umeme.

RC Gambo  aliyasema hayo katika ziara yake ya siku tatu kwaajili ya kukagua miradi ya umeme wa Vijijini ( REA) miradi ya maji  na barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).

Alisema mtumishi huyo wa Tanesco (jina hakumtaja) alichukua fedha kwa mwananchi wa Man'gola kiasi cha Sh. 70,000 ili amuunganishie umeme wa REA ilihali akijua kuwa gharama ya kuunganisha umeme huo ni Sh. 27,000/= huku wananchi wengine wa vijiji vya Tloma na Ganako wakitozwa Sh. 177,000/= badala ya Sh. 27,000/=. 

Alisema ingawa mtumishi huyo wa Tanesco amefukuzwa kazi lakini hela alizochukua Sh. 70,000/= kutoka kwa mwananchi huyo haijarudishwa hivyo ni vyema sasa hela hizo zikarudishwa kwa mwananchi huyo mara moja huku akiziagiza vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia tatizo hilo mara moja.

Pia alimwagiza Meneja wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Mhina kuhakikisha anakaa na watendaji wa NIPO Group Ltd kuhakikisha wanakaa kwa pamoja ili kutatua changamoto za  msambazaji wa umeme wa kampuni ya Lesheya Investment Ltd  aliyeingia mkataba na kampuni ya NIPO Group Ltd kwaajili ya kusambaza nguzo hadi eneo husika ili kufunga umeme kwa wananchi.

"Nataka huyu mtumishi wa Tanesco arejeshe hela ya huyu mwananchi mara moja na pia lazima hatua zichukuliwe kwa hao wanaowachukulia wananchi kiasi kikubwa cha kuwaunganishia umeme wananchi huko vijijini pia siridhishwi na kasi ya usambazwaji umeme unaofanywa na kampuni ya NIPO Group Ltd na naomba hii kampuni kama mnaona wakala anawakwamisha chukueni hatua " Alisema Gambo.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Bi. Theresia Mahongo alisema kuwa suala la mwananchi huyo kuchukuliwa kiasi cha Sh. 70,000/= ni la kweli na lipo mezani kwake hivyo vyombo vya ulinzi na usalama vinalishughulikia suala hilo.

Awali Mhandisi wa kampuni ya NIPO Group Ltd, Hussein Said alisema kuwa kampuni hiyo inaendelea na kazi katika wilaya hiyo pamoja na vijiji mbalimbali lakini changamoto kubwa ni mahitaji ya nguzo ambapo hadi sasa mahitaji ya nguzo hizo ni makubwa kuliko usambazwaji wa umeme wanaofanya kwani mahitaji ya nguzo kubwa ni 1,661 hadi sasa nguzo zilizopo ni 795 huku nguzo ndogo zikiwa zimekuja 257.

Pia wana changamoto kubwa ya usambazwaji wa Transfoma zilizopo ni 21 badala ya 70 kutoka Kiwanda cha kutengeneza Transfoma cha Tanelec huku akisisitiza kuwa endapo watasanbaziwa vifaa hivyo ikiwemo nguzo na transfoma kwa wakati wataweza kusambaza umeme kwa kasi.

Awali wananchi wa kijiji cha Kibaoni na Kilimamoja akiwemo Yusuph Said na Elizabeth Sabaha waliomba kero hiyo ya maji kushughulikia mara moja kwani hivi sasa badala ya wananchi hao kulipia Shilingi 20 kwa ndoo moja ya maji ya kijiji wao wanalipa Sh. 100 kwa ndoo moja.

Gambo anaendelea na ziara yake ya siku tatu katika wilaya za Karatu na Ngorongoro ambapo anakagua maendeleo ya miradi ya barabara na maji katika wilaya hizo.

No comments: