Monday, October 29, 2018

Italia yaiahidi Afrika Ushirikiano wa kiuchumi


Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika wameazimia kukuza na kuimarisha Ushirikiano katika nyanja mbalimbali, hususan biashara na uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya kweli barani Afrika.

Mawaziri hao walifikia azimio hilo wakati wa mkutano wa pili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika uliofanyika Farnesina, Italia tarehe 25 Oktoba 2018 na kuhudhuriwa na Mawaziri wa zaidi ya nchi 40 akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb). 

Mawaziri hao walikutana kwa madhumuni ya kujadili kwa pamoja changamoto zinazohusu usalama, uhuru, amani, demokrasia na namna wadau wa Italia (wenye viwanda, Wafanyabiashara, wanazuoni na taasisi zisizo za kiserikali) watakavyoweza kushiriki katika kukuza uchumi barani Afrika hasa katika sekta ya uwekezaji na biashara. 

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo ambao ulifunguliwa na Rais wa Italia, Mhe. Sergio Mattarella, Mhe Waziri Mahiga alisisitiza suala la amani kuwa ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi barani Afrika. Aidha, alieleza umuhimu wa Jumuiya za Kikanda katika kusuluhisha migogoro mbalimbali inayotokea kwenye Bara la Afrika. Katika hilo, alijulisha jitihada zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kusuluhisha mgogoro nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Sanjari na mkutano huo, Waziri Mahiga alipata fursa ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe Enzo Moavero na Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Gilbert F. Houngbo.

Kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Viongozi hao walikubaliana kuwa, kuandaliwe Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Italia ya kufanya majadiliano ya mara kwa mara yenye lengo ya kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, elimu na utamaduni.

Kuhusu mazungumzo na Rais wa IFAD, wawili hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Mfuko huo kwenye maeneo makuu mannne ambayo ni Huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, kuwajengea uwezeo vijana ili waweze kufanya kilimo kama sehemu ya ajira, kuboresha sekta ya mifugo pamoja na masuala ya lishe bora. 

Aidha, Rais wa IFAD alimuahidi Mhe Waziri kuwa mfuko huo utaendelea kushirikiana vizuri na serikali ya Tanzania hata kwenye miradi inayoendelea ikiwemo Programu ya Miundombinu ya masoko, uongezaji wa thamani na kuwawezesha wakulima wadogo wa vijijini kifedha (Marketing Infrastructure, Value Addition and Rural Finance-MIVRAF). Madhumuni ya programu hiyo ni kupunguza umasikini na kuharakisha ukuaji wa uchumi vijijini ili kuboresha kipato na usalama wa chakula kwa jamii ya watu wa vijijini.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
29 Oktoba 2018 

No comments: