Friday, October 26, 2018

BENKI YAJINASUA KWENYE HASARA,YATANGAZA KUPATA FAIDA

YAJIVUNIA FAIDA YA BIL 1.4/- ROBO YA TATU 2018

BENKI ya Biashara ya DCB imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha inatoka kwenye hasara iliyopata mwaka 2017 ya Sh.bilioni 1.6 na kurudi kwenye faida na kwamba baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni kuboresha mfumo wa endeshaji biashara ambapo gharama za uendeshaji zimeshuka na huduma mpya za kidigitali zimeanzishwa ambapo zimevutia wateja wengi zaidi kufungua account na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama zitokanazo na amana za wateja.

Hayo yameelezwa na Benki ya DCB jijini Dar es Salaam wakati ikitangaza kufanikiwa kupata faida ya Sh. bilioni 1.4 katika kipindi kinachoishia Septemba mwaka 2018 huku ikiipiku hasara ya Sh.bilioni 1.6 iliyopatikana kipindi kama hicho mwaka 2017 ambayo inawakilisha ongezeko la asilimia 187.Faida hiyo ni kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka 2018.

Taarifa ya DCB inaeleza kuwa moja ya huduma za kidigitali ambazo benki imezindua ni akaunti ya kidijiti (DCB Digital Account), DCB Kibubu Digital Account na DCB FDR Digital account.Hivyo akaunti hizo zinamuwezesha mteja wao kufungua akaunti na kufanya miamala yote ya kibenki, kutunza fedha na kuwekeza kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Kuhusu kukua kwa faida ,benki hiyo imesema kukua huko kwa faida umechagizwa na ukuaji wa mikopo ghafi ya wateja kutoka Sh. bilioni 89.3 Septemba mwaka 2017 kufikia Sh. bilioni 91.3 mwezi Septemba, 2018. Ukuaji huo umechagizwa na utoaji wa mikopo ambapo mikopo ya jumla ya Sh.bilioni 50 imetolewa hadi kufikia Septemba mwaka 2018.

"Idadi ya wateja imeongezeka kutoka 144,445 Desemba mwaka 2017, kufikia wateja 157,366 Septemba mwaka 2018. Mapato halisi ya benki yatokanayo na riba yameimarika katika robo ya tatu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita hali ambayo imechagizwa na mkazo wa benki katika kuongeza amana za gharama nafuu kupitia bidhaa za amana za kidijiti, usimamizi wa mizania wenye ufanisi na usimamizi wa gharama za uendeshaji wa benki. Uwiano wa mikopo ghafi na jumla ya amana za benki umeongezeka kwa asilimia 3.1 ikilinganishwa na robo ya pili ya mwaka huu.

"Ili kuhakikisha ufanisi wa mizania, benki imeendelea kulinganisha amana aghali na zenye unafuu, ili kuendana na hali ya amana katika masoko ya kibenki ambapo amana za wateja zimepungua katika robo ya tatu ya mwaka 2018 ikilinganishwa kipindi kama hicho mwaka 2017. Upunguaji huu wa amana aghali umechangia kupungua kwa gharama za riba za amana na kuiwezesha benki kutoa mikopo nafuu kwa wateja, kuongeza mapato halisi na faida kwa ujumla,"imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Pia uongozi wa benki hiyo umefafanua pamoja na ongezeko la mikopo ghafi, benki ya DCB imefanikiwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu kutoka asilimia 18.9 mwezi Desemba 2017 kufikia asilimia 17.8 Septemba mwaka 2018 (Juni 2018 asilimia 17.7). Upunguaji huo umechagizwa na ongezeko la ufanisi katika ukusanyaji wa madeni, utoaji wa mikopo kwa riba nafuu na kuboreshwa kwa huduma kwa waateja.

Pamoja na kujivunia faida hiyo imeelezwa kwamba DCB ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa kama Benki ya Jumuiya ya Wananchi “community bank” na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kutokana a kilio cha wakazi wengi wa Jiji kutokuwa na njia rahisi ya kupata mitaji midogo midogo ya biashara. Katika miaka yake 16 ya utoaji huduma, benki imeongeza idadi ya wateja kufikia 157,366 Septemba mwaka 2018, idadi hii ni kubwa kwa sababu benki ya DCB inalenga zaidi wananchi wa kipato cha chini. Benki ya DCB ambayo ni ya kwanza kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa, imeweza kukuza mtandao wake wa matawi kufikia matawi nane likiwepo tawi la Dodoma, na inatarajia kuongeza matawi mengine mikoani katika miaka ya mbeleni.

Pia benki hiyo imejiimarisha zaidi katika teknohama na mifumo mbalimbali ya utoaji huduma huku ikiwa mstari wa mbele katika utoaji wa mitaji midogo kwa wananchi wa kipato cha chini, ambapo hadi mwishoni mwa Septemba mwaka 2018, imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Sh.billioni 150 kwa wafanyabiashara wadogo wa vikundi, ikiwemo Sh.billioni 16 zilizotolewa kwa mfuko wa wanawake na vijana wa halmashauri za Jiji la Dar es salaam. No comments: