Wednesday, October 31, 2018

BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO KUHAMASISHA UZALISHAJI WA MAZIWA

Katika kuhakikisha tasnia ya maziwa inawanufaisha wazalishaji wadogo wadogo wa maziwa nchini Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ipo kwenye mikakati ya kuanzisha Jukwaa la Ushirikiano wa Tasnia ya Maziwa.

Akizungumza na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo imejipanga kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongezeka nchini ili kutoa fursa kwa wazalishaji wadogo kuweza kuchangia ukuaji wa tasnia hiyo.

Bw. Justine alisema kuwa shughuli za usindikaji wa maziwa zipo chini ya kiwango kwa viwanda vyote vinavyosindika maziwa nchini kutokana na uzalishaji duni wa maziwa hali inayorudisha nyuma ukuaji wa tasnia hiyo. “Fursa za kimasoko na uendelezaji wa tasnia ya maziwa ni kubwa hivyo tumejipanga kuhakikisha tunachagiza tasnia hii ili kuongeza uzalishaji na kuwaongezea kipato wazalishaji hasa wale wadogo wadogo,” alisema.

Aliongeza kuwa TADB imejipanga kuwakutanisha wadau wa tasnia ya maziwa ili kujadili kwa kina mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu ili kuja na mpango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini. Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya NARCO, Prof. Philemon Wambura alisema NARCO imejipanga kuwezesha wazalishaji wa wadogo kote nchini kwa kuwapatia huduma za ugani ili waweze kuongeza uzalishaji wa maziwa.

Prof. Wambura aliongeza kuwa mchango wa Benki ya Kilimo katika kuhakikisha tasnia ya maziwa inachangia shughuli za uzalishaji ni jambo la kuungwa mkono. “Mchango huu wa TADB utasaidia kuongeza uzalishaji hali itakayowaongezea kipato wazalishaji wadogo nchini na hivyo kutasaidia kuwaongezea kipato wafugaji wetu,” alisema.

Kwa mujibu wa twakwimu za Bodi ya Maziwa Tanzania, tasnia ya maziwa inachangia asilimia 3.9 ya GDP huku ikikadiriwa kuwa na ng’ombe wa maziwa zaidi ya milioni 1.1 kati ya jumla ya ng’ombe milioni 30.5.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (kulia) akimkaribisha Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Philemon Wambura (kushoto) alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dar es Salaam. 
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine akizungumza na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Philemon Wambura (hayupo pichani) wakati walipokutana kuzungumzia nafasi ya TADB na NARCO katika kusaidia tasnia ya maziwa nchini. 
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Philemon Wambura akizungumza wakati wa kikao hicho. 
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Japhet Justine (kulia) akizungumza na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Philemon Wambura (kushoto) wakihimiza jambo wakati wa kikao cha kujadili nafasi ya taasisi zao katika kuchagiza uzalishaji wa tasnia ya maziwa nchini. 

No comments: