NA DANIEL MBEGA, KISARAWE
KUWEKWA
kwa jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata zao la muhogo katika
Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe kumetoa fursa kubwa kwa kikundi
cha akinamama wanaojihusisha na kilimo cha zao hilo pamoja na wananchi
wengine.
Kiongozi
wa Kikundi cha akinamama cha Kitanga Green Voices, Mama Abia Magembe,
anasema uwekaji wa jiwe hilo la msingi uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya
Kisarawe Jumamosi, Septemba 15, 2018 umefufua matumaini si ya akinamama
pekee, bali hata wananchi wengine ambao walikuwa wamekata tamaa ya
kulima muhogo kutokana na kutokuwepo kwa soko la uhakika.
“Matumaini
sasa yapo ingawa bado tunayo safari ndefu ya kufikia malengo, tunataka
kuchakata na hatimaye kutengeneza bidhaa mbalimbali zaidi ya 300 kwa
kutumia zao la muhogo,” anasema Mama Magembe, Ofisa Kilimo mstaafu
ambaye amefufua upya matumaini ya wakulima wa eneo hilo.
Tayari
amekwishawafundisha akinamama zaidi ya 60 kijijini hapo ambao wanaweza
kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo na
anaendelea kuwafundisha wengine, kwani anasema, mahali kilipo kiwanda
hicho patakuwa kituo cha kudumu cha mafunzo kwa wote, wanaume kwa
wanawake.
Wakati
wa uzinduzi huo, DC Mwegelo aliahidi kuwasaidia akinamama hao pamoja na
wakulima wengine kukuza zao la muhogo, ambalo alisema ni miongoni mwa
mazao mawili ya kipaumbele wilayani humo, likiwemo zao la korosho.
Alisema
atawasaidia akinamama hao kuwaunganisha na wadau mbalimbali ili kupata
mikopo nafuu, ikiwemo mikopo isiyo na riba huku pia akiahidi kwamba,
changamoto ya umeme na maji zitatatuliwa haraka.
Pengine
unafahamu faida tatu au nne tu za muhogo ambazo ni kuutafuna mbichi,
kuuchemsha au kuuchoma; unga wake kwa ajili ya lishe, majani yake kama
mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti yake inapokauka kutumika kama
kuni.
Inawezekana hujui kama maganda ya mihogo baada ya kumenywa ni chakula bora cha mifugo yakikaushwa au mabichi.Siyo
ajabu pia hujui kwamba muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake
yake yanatoa wanga (starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa,
gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na
pia ni lishe nzuri.
Lakini
zao la muhogo ni zaidi ya linavyofikiriwa kwa sababu licha ya faida
hizo chache, lakini pia linazalisha bidhaa zaidi ya 300 kama ambavyo
akinamama wa Kijiji cha Kitanga, Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe
wameamua kufanya.
Akinamama
hao kupitia kikundi chao cha Kitanga Green Voices mbali ya kuzalisha
unga pamoja na chips, sasa wanatengeneza bidhaa lukuki zenye ubora kama
chapatti, maandazi, skonzi, biskuti, tambi, cassava chop, na nyinginezo
nyingi.
Hatua
hiyo imekuja baada ya kupatiwa mafunzo kupitia mradi wa Green Voices
unaofadhiliwa na taasisi ya maendeleo ya wanawake wa Afrika
inayojulikana kama Women of Africa Foundation, ambayo iko chini ya
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.
Kuanzishwa
kwa mradi huo wa kusindika muhogo pamoja na bidhaa zake kumeliokoa zao
hilo ambalo licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, lakini limekuwa
likidorora hata katika soko la vyakula.
“Tangu
tumeanzisha kikundi hiki miezi mitatu iliyopita hivi sasa muhogo
hauwezi kuozea shambani na wananchi wanaona umuhimu wa zao hilo,”
anasema Mama Magembe, ambaye ni mratibu wa mradi huo.
Mama
Magembe, ambaye yeyé pamoja na akinamama wengine tisa walipatiwa
mafunzo nchini Hispania kwa nia ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali
unaoendana na utunzaji wa mazingira pamoja na kupambana na mabadiliko ya
tabianchi, anasema kwamba zao la muhogo sasa limepata thamani kubwa
kijijini hapo na wana uhakika wakulima wa wilaya ya Kisarawe wanaweza
kugeukia miradi kama hiyo ili kuongeza mnyororo wa thamani.
Akinamama
10 wanaofanya miradi mbalimbali ya ujasirimali kutpia mradi wa Green
Voices wanatoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro,
Pwani na Mwanza.Silvera
Mujuni, Ofisa Chakula na Lishe wa Wilaya ya Kisarawe, anasema kwamba
wilaya hiyo ina fursa kubwa ya kusindika na kuchakata mazao mengi
yatokanayo na muhogo kwa kuwa zao hilo ndilo kuu kwa chakula na
biashara.
Anasema
kwamba, ardhi katika vijijini vingi vya wilaya hiyo inastawisha muhogo
kwa wingi, hivyo ikiwa wananchi watajizatiti na kujifunza namna ya
kuchakata bidhaa za muhogo wanaweza kupata faida kubwa kiuchumi.
“Muhogo
ndilo zao kuu katika maeneo mengi ya wilaya hii ambayo haiwezi
kustawisha mazao mengine kama mahindi, hivyo ni vyema wananchi
wakajifunza utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo,”
anasema Bi. Silvera aliyemwakilisha mkurugenzi wa wilaya hiyo na ambaye
ndiye alikuwa akiwafundisha akinamama hao namna ya kutengeneza bidhaa
mbalimbali.
Awali
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Wazir Yakoub Wazir, aliwataka akinamama
hao wajipange wasajiliwe rasmi ili waweze kunufaika na mikopo
inayotolewa na serikali na taasisi nyingine za binafsi.
“Ofisi
yangu iko wazi wakati wote, mkitaka kwenda kusajiliwa wilayani hata leo
niko tayari kuwasaidia, nawaombeni mje niwasaidie hata namna ya kuandaa
katiba ya kikundi pamoja na taratibu nyingine,” alisema.
Naye
Diwani wa Kata ya Msimbu, Anna Lilomo, amesema atajitahidi – kwa
kushirikiana na diwani mwenzake wa viti maalum Mossy Sultan Kufurumbaya –
kuwapigania akinamama hao kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ili
waweze kupatiwa misaada na mikopo hata kupitia katika asilimia 10 ya
bajeti ya halmashauri ambayo hulenga kuwasaidia wanawake na vijana.
“Bahati
nzuri sisi hapa ni madiwani wanawake, kwa hiyo tutalipeleka suala la
akinamama hawa kwenye Baraza la Madiwani na kuelezea umuhimu wa kuongeza
thamani kwenye zao letu la muhogo ili limkomboe mkulima,” alisema
Diwani Lilomo.
Mratibu
wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya,
anasema kwamba anafarijika anapoona wanawake wakihamasika kushiriki
shughuli za maendeleo, hasa ujasiriamali unaolenga kupambana na
mabadiliko ya tabia nchi.
“Suala
la kuhakikisha usalama wa chakula, kutokomeza umaskini, kuwawezesha
wanawake kiuchumi na mapambano dhidi ya tabianchi ni mambo yaliyopewa
kipaumbele katika Malengo Endelevu ya Dunia, hivyo wanawake
wanaotekeleza miradi ya Green Voices wanayatekeleza malengo hayo kwa
wakati mmoja,” anasema Secelela.
Zao lililotelekezwa, sasa mkombozi
Muhogo
ni zao linalochukuliwa na wengi kama la ziada hasa kwenye ukame, lakini
wengi hulifanya kama mlo wa hamu bila kutambua kwamba zao hilo lina
manufaa makubwa kwa lishe na kibiashara.Wengi
wanauchukulia muhogo kama chakula cha maskini, hawa wale wanaojitiahidi
kulima zao hilo, huyapa kipaumbele mazao mengine kuliko muhogo.
Lakini
muhogo ni zao mojawapo ambalo linaweza kuiepusha jamii na baa la njaa
huku katika baadhi ya mataifa likitumika kama chanzo cha nishati ili
kukabiliana na bei ya mafuta na nishati nyinginezo.Baa
la njaa ni tatizo kubwa linalozikumba nchi nyingi barani Afrika,
Tanzania ikiwa miongoni mwazo, lakini licha ya watu kuhimizwa kulima
muhogo, bado wanalipuuza zao hilo na kuliona kama zao fulani la mizizi
tu.
Katika mikoa kama Lindi na Mtwara ambayo kwa miaka mingi inalima kwa wingi muhogo, chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa muhogo.Licha
ya kudharauliwa kwa zao hilo, lakini siyo ajabu ukakuta mlo wa siku
hiyo umetokana na muhogo kasoro chumvi na nazi, kwani inawezekana kuni
zilizopikia ni matawi ya muhogo, ugali wa muhogo na kisamvu cha muhogo!
Na
wakulima wengi katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara wanakula ugali wa
muhogo pale wanapokoa unga wa mahindi, ambapo wanaokula ugali huo wa
muhogo (Wazaramo wanasema ‘bada’ na Wamakua wanauita ‘matamba’)
huonekana maskini wa kutupa.
Leo
hii wanapohamasishwa kulima muhogo kwa sababu ya kustahimili ukame,
bado wengi wanasuasua, lakini watakapoambiwa kwamba unga wa muhogo
unatoa bidhaa nyingi zenye faida kubwa, huenda wengi wakaligeukia zao
hilo na kulima kibiashara.
Inafurahisha
sana siku hizi kuona watu wengi wakikimbilia ugali wa muhogo hata
hotelini, lakini hiyo bado haijatosha kulirasimisha zao hilo ili liwe na
tija kubwa.
Akinamama
wa Kijiji cha Kitanga wanaweza kuwa mabalozi wazuri wa zao hilo, kwa
sababu tayari wameanza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo hata
wananchi wa kijiji hicho wameshangazwa nazo baada ya kuzionja na kuona
ubora wake.
Kilimo
cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza
pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za
Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula
nje, jukumu ambalo kikundi cha Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.
Faida
za muhogo ni nyingine kama zilivyoelezwa hapo juu, lakini kwa msisitizo
ni kwamba, unga wake hutumika kutengeneza vyakula mbalimbali, baadhi ni
uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, skonzi, biskuiti, mandazi,
mafuta ya lishe, sabuni ya unga, kuni, mboga, huksi pamoja na bidhaa
nyingine nyingi.
Mazao
yanayopatikana katika mzizi wenyewe, miti na majani huweza kuzalisha
bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi, mafuta,
kilevi, dawa za binadamu na plastiki wakati ambapo wanga (starch)
hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali
za ukuta na sukari (sugar syrup).
Takwimu
za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu
duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji takriban tani
milioni 102.6 kila mwaka.
Tanzania
ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika
baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu
ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao
linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima ambapo karibu
kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa
inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga,
Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa
Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa kusini. Mkoa
wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania.
Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya mahindi. Taarifa
ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula
Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.Hii
ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na magonjwa au wadudu
wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika
ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa
mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya
viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba
asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.
Kiongozi
wa Kikundi cha akinamama cha Kitanga Green Voices, Mama Abia Magembe,
akitoa maelezo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao
la muhogo kwa wageni mbalimbali, akiwemo mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya
Kisarawe, Jokate Mwegelo, na Balozi Getrude Mongella.
No comments:
Post a Comment