Tuesday, September 25, 2018

WAKULIMA WADOGO WA MKONGE WAIPINGA KAMPUNI YA KATANI MBELE YA WAZIRI WA KILIMO WATAKA MFUMO WA SOKO HURIA

Na Mathias Canal-WK, Tanga

Wakulima wadogo wa zao la mkonge Wilayani Korogwe mkoa wa Tanga, wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuanzisha soko huria kwa ajili ya ununuzi wa zao hilo ili malengo yaliyowekwa na serikali ya kuzalisha tani 100,000 kwa mwaka yafikiwe.

Wakulima hao wameilalamikia Kampuni ya Katani Ltd. kwamba inachukuwa asilimia 54 na kumuachia mkulima asilimia 46 jambo walilodai ni unyonyaji unaofanywa na kampuni hiyo kinyume na utaratibu wa kiutendaji.

Wakulima hao wametoa malalamiko yao mbele ya waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba wakati akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili kutekeleza maagizo aliyopewa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa ya kutembelea mashamba ya Mkonge mkoani humo na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.

Katika mkutano huo pia wakulima hao walijadili suala la bei na namna ambavyo sera iliyowekwa na serikali inayoelekeza kuwa kila mwaka mkonge uzalishwe tani 100,000 na kwamba sera hiyo haisimamiwi ipasavyo kwani endapo kama ikisimamiwa ipasavyo zao hilo litaingia kwenye zao kuu la kibiashara nchini.

Akizungumza katika mikutano hiyo Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba alisema kuwa Tanzania ilikuwa ndiyo nchi pekee barani Afrika kupokea zao la mkonge kutoka Jimbo la Yucatan, nchini Mexico mwaka 1893. Mkoa wa Tanga ndio ulikuwa kinara wa kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa na mashamba makubwa ikifuatiwa na Morogoro.
Hadi kufikia mwaka 1964, uzalishaji wa mkonge nchini ulikuwa ni tani 235,000 kwa mwaka, hivyo kuifanya Tanzania kuwa ndiyo nchi pekee iliyokuwa ikifanya vizuri katika zao la mkonge barani Afrika.
Aliongeza kuwa Kutokana hali hiyo, sekta ya kilimo hicho ndiyo sekta ambayo ilikuwa imeajiri watu wengi hususani katika maeneo ya mashambani. Hivyo Mkoa wa Tanga ulikuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi kutokana na faida ya uwapo wa zao hilo ukitoa viwanda vilivyokuwepo enzi hizo.
Licha ya zao hilo kuwa na manufaa ya kiuchumi, ni bidhaa ya nyuzi pekee ndiyo ilikuwa ikisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya dunia. Hata hivyo, ujio wa kamba mbadala za nailoni katika miaka ya 1970 uliweza kuua soko la mkonge kwa kiasi kikubwa hali iliyolazimu kushusha uzalishaji na kufikia tani 32,000 pekee kwa mwaka.
Dkt Tizeba alisisitiza kuwa zao la Mkonge ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara hivyo serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli imejidhatiti kuhakikisha zao hilo linaendelea kukua na kuongeza uzalishaji maradufu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanufaikaji wakubwa ni wakulima na sio vinginevyo.

Akijibu malalamiko ya wananchi ambao ni wakulima wa mkonge katika Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga Dkt Tizeba alisema kuwa serikali haiwezi kuchukua hatua za haraka katika kutatua mgogoro huo badala yake inaendelea kujiridhisha ili kubaini ukweli kuhusu uendeshaji wa zao hilo kupitia kampuni ya Katani LTD na ndani ya wiki mbili itatoa maelekezo ya serikali.

Dkt Tizeba ameitaka kampuni ya Katani LTD pamoja na wakulima wa katani kutunza kumbukumbu zao zote ili ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itakapoanza kazi ya ukaguzi iweze kupata taarifa za uhakika.
Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa zao la Mkonge kwenye Shamba la Mgombezi lililopo katika Kijiji na kata ya Mgombezi katika Wilaya ya Korogwe wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tanga jana tarehe 24 Septemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK, Tanga)
Kikao kazi wakulima wa zao la Mkonge na Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba kilichofanyika katika kijiji na kata ya Makuyuni Wilaya ya Korogwe  wakati wa ziara ya waziri huyo ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tanga, jana tarehe 24 Septemba 2018. 
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe Martin Shigela akitoa maelezo mafupi Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba kuhusu zao la Mkonge mkoani humo mbele ya wakulima wakulima katika kijiji na kata ya Makuyuni, Wilayani Korogwe jana tarehe 24 Septemba 2018. 
Wakulima wa zao la Mkonge kwenye Shamba la Mgombezi lililopo katika Kijiji na kata ya Mgombezi wilaya ya Korogwe wakifatilia kwa makini mkutano wa Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba wakati wa mkutano wa pamoja kujadili zao la Mkonge Mkoani Tanga jana tarehe 24 Septemba 2018. 
Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa zao la Mkonge kwenye Shamba la Mgombezi lililopo katika Kijiji na kata ya Mgombezi wilaya ya Korogwe wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tanga jana tarehe 24 Septemba 2018. 

No comments: