Bw. Paul Mtango ambaye ni Mkulima wa Kijiji cha Mpirani Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro akiwaonyesha Wajumbe wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) mfumo alioutumia kupanda Maharage katika shamba lake kwa kutumia Kilimo hifadhi, mfumo unaowafanya wakulima kupata mazao mengi tofauti na walivyokuwa wakilima awali.
Bw. Paul Mtango ambaye ni Mkulima wa Kijiji cha Mpirani Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania waliofika shambani kwake kujionea namna anavyonufaika na mradi wa kilimo hifadhi unaoratibiwa na ACT/TAP ambapo amewaeleza kwa kutumia Kilimo Hifadhi anaweza kupata gunia 12 za maharage kwa heka moja tofauti na awali alipokuwa akipata gunia 3 kwa hekari..
Bw. Paul Mtango ambaye ni Mkulima wa Kijiji cha Mpirani Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro akisisitiza jambo kwa Wajumbe wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) waliofika shambani kwake kujionea namna anavyonufaika na mradi wa kilimo hifadhi unaoratibiwa na ACT/TAP, kuhusu namna kilimo hifadhi kinavyohifadhi ardhi vizuri kwa kizazi kijacho.
UONGOZI wa Halimashauri ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro umeonyesha kuridhishwa kwake na namna Mradi wa Kilimo Hifadhi unaotekelezwa wilayani humo na Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) chini ya Mradi wake wa Ubia wa Kilimo Tanzania ulivyoweza kuwasaidia wakulima kwa kupata mavuno mengi ukilinganisha na hapo awali.
Kauli hiyo imetolewa Jana na Kaimu Mkurugenzi wa halimashauri hiyo John Nnko ,Wakati alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) waliofika wilayani humo kujionea utekelezaji wa Mradi wa kilimo Hifadhi unaotekelezwa na Baraza la Kilimo Tanzania chini ya Mradi wake wa Ubia wa Kilimo Tanzania.
Alisema kuwa mpaka sasa kumekuwa na mwikitio mkubwa wa wakulima kutaka kujifunza zaidi namna ya kulima kilimo hifadhi hasa katika mazao ya mahindi na maharage ambapo alilishukuru Baraza la Kilimo kwa kutekeleza Mradi huo wilayani Same ambao unawafanya kupata mavuno mengi na kutokuwa na hofu ya ukame.
“Mpaka sasa Mradi huu wa Kilimo Hifadhi umekwisha kuwafikia zaidi ya wakulima 1,300 na uko katika vijiji tisa pekee, lakini tunaona mwitikio wa wakulima unazidi kuwa mkubwa wa kutaka kujua namna ya kulima kwa kutumia teknolojia hii, kwakweli ACT tunawashukuru sana kwa sababu pia hata watalaamu mmetuletea nyie” Alisema.
Miongoni mwa vijiji vinavyotekeleza mradi huo wilayani humo ni pamoja na Saweni, Hedaru,Kisiwani, Njiro, Mpirani na Ishinde ambapo wakulima waliueleza ujumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya ACT iliyofika katika mashamba yao kuwa tangu mradi huo wa Kilimo hifadhi ulipoanza mwaka 2011 vipato vyao vimeimarika huku gharama za uandaaji wa mashamba zikipungua.
“Awali kabla ya mafunzo tulikuwa tunapanda robo heka ya Maharage kwa kutumia kilo 25 za Mbegu, na ukija kuvuna unaambulia debe tatu au nne tu, lakini kwa kutumia kilimo hifadhi robo heka hiyo hiyo tunapanda kwa kutumia kilo sita pekee za mbegu na mavuno yake tunapata gunia tatu hadi nne kwa kweli tunawashukuru sana hawa watu wa ACT kwa kutuletea hiki kilimo hifadhi” Alisema Bi Agnes Tumaini Mkulima wa Kilimo hifadhi kijiji cha Mpirani wilayani Same.
Wakulima wameieleza bodi hiyo kuwa licha ya mavuno mengi wanayoyapata kwa sasa changamoto kubwa inayowakabili ni uwepo wa bei ndogo ya mazao hasa ya mahindi pamoja na Pembejeo za kilimo na kuomba wadau wa kilimo kujitokeza kuwekeza katika kilimo hicho.
“Kwa sasa nimeona Kilimo hifadhi kinamaana tulikuwa tunalima kienyeji bila mpangilio lakini baada ya watalamu wa ACT kuja hapa kutuelimisha kuhusu kilimo hiki kwakweli nimenufaika sana, situmii muda mwingi shambani, natumia mbegu kigodo, sina shaka kuhusu ukosefu wa mvua lakini hatimaye kwakutumia kilimo hifadhi Napata mavuno mengi tofauti na wenzangu.”alisema Bw. Paul Mtigi Mkulima wa Kilimo Hifadhi Kata ya Maole Wilayani Same.
“Pamoja na mafanikio tunayoyapata lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya LIPA (Jembe maalum la kulimia kilimo hifadhi) Mkulima anatakiwa alime kibiashara kwa hivyo tunaomba wadau wengine wa kilimo watuwezeshe kupata LIPA kwa sababu ndio pembejeo muhimu inayomrahisishia mkulima hasa kwenye kilimo hifadhi lakini mpaka sasa hakuna na ndio changamoto kubwa katika kilimo hiki cha hifadhi” alisema
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya ACT, Bw Enock Ndondole alisema bodi imeridhishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa wilayani Same na kuwapongeza wakulima kwa kuitikia kwa wingi teknlojia hiyo ya Kilimo hifadhi.
“Kikubwa tunachowamba jitahidini kuwafikishia wakulima wenzeni hii teknlojia ili nao wanufaike kama mnavyonufaika ninyi, wakija hapa wakiona mnavyofanya kazi wengi zaidi wataanza kulima kwa teknlojia hii, kwa sababu dhamira yetu ni kuona wakulima wengi wanatumia kilimo hifadhi na kuachana na kilimo cha kizamani na nyie ndio mnanafasi ya kuwaelimisha wakulima ambao bado hawaja anza kutumia teknolojia hii alisema Bw Ndondole.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) Bi Janeth Bitegeko alisema ACT tangu kaunzishwa kwake imekuwa na mchango mkubwa katika kuinua sekta ya kilimo ambapo alitaja masuala muhimu yaliyoasisiwa na ACT kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa Benki ya Kilimo, Program ya Kilimo kwanza na kwamba tayari serikali imekwisha ondoa kodi nyingi ambazo zilikuwa kero kwa mkulima baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Baraza la Kilimo Tanzania.
No comments:
Post a Comment