Friday, August 31, 2018

16 WANAODAIWA KUKWAPUA FEDHA ZA USHIRIKA WILAYANI HAI ,WAWEKWA NDANI KWA AMRI YA DC SABAYA



Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,
Kanda ya Kaskazini.


-WADAIWA KUFANYA UBADHILIFU WA ZAIDI YA MIL 200.
-WENGINE WAUZA VIPURI VYA MASHINE.
WATU 16 wakiwemo viongozi wa Bodi ya Ushirika wa Umoja wa watumia maji katika kijiji cha Mijongweni (UWAMI) wanashikiliwa na Jeshi la  Polisi kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya  wakituhumiwa kuhusika na ubadhilifu wa fedha za mradi zaidi ya Sh Mil 200.
Mbali na Viongozi wa Bodi ya ushirika huo wakiongozwa na Mwenyekiti wake ,Nuru Ndoma pia wamo baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji, Viongozi wa kamati ya mpito ya kusimamia mradi huo ikiongozwa na Alex Mkwizu.
Kukamatwa kwa Viongozi hao kunatokana na taarifa ya uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa na  Mkuu huyo wa wilaya kuchunguza madai ya ubadhilifu wa fedha baada ya kukataa taarifa yaawali ya  kamati kama hiyo iliyoundwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Gelasius Byakanwa.
Tuhuma zinazowakabili watu hao zimetajwa kuwa ni pamoja na kuuzwa kinyemela kwa Mashine ya kulimia (Power tiller ) aina ya Kubota iliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwa kijiji cha Mijongweni ambayo inatajwa kuuzwa kwa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Yusuph Losindilo.
Baadhi ya viongozi hao pia wanatajwa kutakatisha fedha za malipo ya ukodishwaji wa mashine ya kuvunia Mpunga kwa kuziingiza katika akaunti ya kijiji na kasha kuzitoa wakati huo huo na kuzipangia matumizi yasiyokuwa na maelezo ya kutoshereza.
Aidha watu hao pia wanadaiwa kuuza baadhi ya vipuri vya Mashine hizo na baadae kuonesha kuwa wamenunua vipuri kwa ajili ya matengenezo ya mashine hizo huku ikionyesha vipuri vinavyodaiwa kununuliwa ni vile vilivyoletwa pamoja na mashine.
Katika taarifa yake ,Mwenyekiti wa kamati hiyo maalumu ya uchunguzi ,Valeria Banda alisema wizara ya Kilimo ,chakula na Ushirika kupitia Halmashauri ya wilaya ya Hai ilipeleka mashine tano za kuvuna na moja ya kupura mpinga kwa lengo la kupunguza adha ya wananchi kuvuna na kupura mpunga kwa kutumia mikono.
“Lengo jingine la kutolewa kwa mashine hizi ilikuwa ni kuongeza chanzo cha mapato kwa wananchi wa kijiji cha Mijongweni ,mashine tatu zenye thamani ya Sh Mil 222.5 zilikuwa ni Combine Harvester aina ya Kubota , mbili aina ya Daedong na moja ya Kupura mpunga (Paddy thresher) zenye thamani ya Sh Mil 152.8”alisema Valeria.
Alisema katika kuendeleza ubadhilifu watu hao wanadaiwa kushindwa kusimamia matumizi ya mashine hizo  ambapo inadaiwa wajumbe wa bodi walipangiana zamu ya kusimamia mashine izo wakati wa zoezi la uvunaji kwa maslahi yao binafsi huku wengine wakivuna nyakati za usiku bila kuwasilisha hesabu za mavuno hayo kwa uongozi.
 “Mfano Mayunga Mathayo anatuhumiwa kuvuna nyakati za usiku na kutowasilisha hesabu za fedha alizokuwa anapata ,hali iliyosababisha afukuzwe kuwa mjumbe wa bodi.Mayunga pia aliuza Hydrolic pump (Orignal) aina ya Kubota yenye thamani ya sht Mil 5 ya mashine namba tisa ya kuvuna mpunga na kufunga pump isiyo na ubora kwenye mashine hiyo ambayo kwa sasa imeharibika.”alisema Valeria.
Valeria alisema fedha zilizokuwa zinapatikana shambani zaidi ya asilimia 50 zilifanyiwa matumizi shambani na wakati mwingine fedha zote zilitumika huko huko shambani bila kufikishwa ofisini na hata zilizofikishwa bado zilipangiwa tena matumizi.
“Baada ya fedha kufanyiwa matumizi zilizobaki zilipelekwa SACCOS ya jitegemee na kutolew wakati huo huo kwa matumizi mengine yasiyo na kibali wala vithibitisho vyovyote ,mfano Oktoba 18 ,2016 kiasi cha sh 810,000 ziliingizwa kwenye akaunti na tarehe hiyo hiyo Sh 800,000 zikatolewa ,katibu wa Bodi Severa Kimati aliyehusika kuziweka na kuzitoa hakuwa na maelezo ya kutosha zaidi ya kusema alitumwa na mwenyekiti wa Bodi Nuru Ndoma”alisema Valeria.
Alisema fedha ambazo zingetakiwa kuwekwa katika akaunti ya kijiji toka Machi,2016 wakati mashine hizo zikianza kufanya kazi hadi kufikia Juni ,2018 kipindi ambachowalifanya kazi wajumbe wawili kutoka kwenye jamii zilipaswa kuwa Sh Mil 285.6 lakini kiasi kilichopo ni Sh Mil 10.9 ambazo zilipatikana baada ya afisa mtendaji na afisa ugani kuamua kusimamia mashine moja katika kipindi cha mwezi mmoja.
Akizungumza baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo ,Mkuu wa wilaya ya Hai,Lenga Ole Sabaya alimuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Hai,Lwelwe Mpina kumkamata aliyekuwa Mkuu wa idara ya Ushirika wa wilaya hiyo , Raphael Mbwambo ambaye alitajwa pia kuhusika katikaubadhirfu huo.
Alisema viongozi wa Bodi, ya Ushirika huo hawakuwa na uhalali kutokana na kwamba hakuna wanahisa wala wanachama waliokaa  na kuwachagua  na kwamba waliteuana kwa maslahi yao binafsi huku akitaka fedha zote zilizopotea kurejeshwa.
“HAwa viongozi wa Bodi kwa kushirikiana na wajumbe wa serikali ya kijiji warudishe fedha walizoiba za wananchi wanyonge wa kijiji cha Mijongweni ,Nimeelekeza wasiingie kwenye ofisi yoyote ya umma,hawa ni waharifu kama waharifu wengine hadi itakapothibitika vinginevyo.”alisema Ole Sabaya.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya ushirika huo ,Nuru Ndomba  na Katibu wake wake  Severa Kimati  pamoja na wajumbe wengine, Salama Amani,Sadiki Msangi, Abuu Musa na D eogratius Bruno,.
Wengine ni Alex Mkwizu, Mashati Amani, Bakari Malola, Adamu Mdaki,Mayunga Mathayo ,Abdalah Dhamiri,Richard Msele,Ramadhan Miraji ,Miraji Araba na Koswai Mrisho.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya akizungumza wakati wa mkutano wa utoaji wa taarifa ya uchunguzi wa kamati iliyoundwa na mkuu huyo kuchunguza ubadhilifu wa fedha za Ushirika wa watumia maji katika kijiji cha Mijongweni.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya akiwahoji baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji cha Mijongweni kuhusiana na ubadhilifu uliofanyika katika Ushirika huo.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya ,akizungumza juu ya maamuzi yaliyochukuliwa mara baada ya kamati aliyoiunda kuwasilisha taarifa yake.
Baadhi ya wananchi wakisikiliza kwa makini juu ya maamuzi yaliyochukuliwa na Mkuu huyo wa wilaya .
Baadhi ya wananchi wakionesha mabango yenye ujumbe mbalimbali wakati wa mkutano huo.
Katibu tawala wa wilaya ya Hai,Upendo Wera akizungumza katika mkutano huo.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mijongweni ,Omary Mohamed akizungumza kwa niaba ya wananchi wengine katika mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya akitizama baadhi ya mashine zilizotolewa kwa Ushirika huo ambazo zinatajwa kutumika huku mapato yake hayajulikani yalipo.
Moja ya Mashine hizo ikiwa tayari imeharibika baada ya kuondolewa Roller inayotumika kwa ajili ya kutembelea.
Mashine mpya ya Ushirika huo ambayo haijaanza kutumika bado.
Baadhi ya watuhumiwa wa ubadhilifu wa fedha za Mradi wa Ushirika huo wakiwa kwenye gari la Polisi mara baada ya kukamatwa wakiwa eneo la mkutano.

No comments: