Friday, August 31, 2018

MAWAKILI WA SERIKALI KUWA NA CHAMA CHAO – AG

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi akitoa mada kuhusu Nafasi na Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wakati wa mkutano unaoendelea wa Mawakili wa Serikali waliokatika utumishi wa umma. Pamoja na mambo mengine Dk. Kilangi amesema Mawakili wa Seriakali walio katika utumishi wa umma watakuwa na chama chao.
Sehemu ya mawakili wa serikali kutoka wizara mbalimbali, Idara na Taasisi zinazojitegema, Wakala na Serikali za Mitaa ambao wapo Jijini Dodoma kwa mkutano wao wa siku mbili.

Na Mwandishi Maalum, Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi amesema, anakusudia kuanzisha Chama cha Wanasheria walio katika utumishi wa Umma. Dk. Kilangi ameyaeleza hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Nafasi na Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Mawakili wa Serikali walio katika utumishi wa umma wanaokutana katika mkutano wao wa siku mbili unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.

Mawakili hao wa Serikali wapatao mia tisa ( 900) wanatoka Wizara mbalimbali, Idara za Serikali, Taasisi na Mashirika yanayojitegemea, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mkutano huo ambao ni wa pili kufanyikia ulifunguliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha kwamba, kuanzishwa kwa Chama hicho ni kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Muswaada wa Sheria ya Marekebisho Mbalimbali ( Na.2) 2018 inayoeleza kuwa , “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaweza kuanzisha Chama cha Wanasheri katika Utumishi wa Umma”.

Amewaeleza Mawakili wa Serikali kwamba Chama hicho kitakuwa kinakutana mara moja kwa mwaka kwaajili ya kujadili masuala mbalimbali ya kisheria ikiwamo maendeleo ya taaluma hiyo. Dk. Kilangi amesema, pamoja na wanachama wa chama hicho kukutana mara moja kwa mwaka, Waziri mwenye dhamana na mambo ya sheria anaweza kuitisha mikutano ya wanasheria waliokatika utumishi wa umma kila anapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Amefafanua zaidi kwa kusema, ripoti ya mikutano ya chama hicho itawasilishwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria na kwamba, Waziri atatunga Kanuni kuhusu usimamizi, uongozi, muundo na uendeshaji wa shughuli za chama. Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuanzishwa kwa chama cha Mawakili wa Serikali walio katika utumishi wa Umma hakutawanyima fursa mawakili hao ya kujiunga au kuwa wanachama wa vyama vingine vya kitaaluma kikiwamo Tanganyika law Society ( TLS).

Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa daftari la mawakili wa serikali, Mwanasheria Mkuu amesema, daftari hili litaanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Muswaada wa Sheria ya Marekebisho mbalimbali ( Na. 2) 2018 unaotamka kwamba, “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataanzisha Daftari la Mawakili wa Serikali ( Roll of State Attorneys)”.

Amesema daftari hilo likuwa na majina ya mawakili wa serikali kwa kuzingatia ukuu ( seniority ) miongoni mwao na kusisitiza kwamba, hatua hiyo haitaathiri sifa au hadhi ambayo mtu alikuwa nayo kabla ya kuazishwa kwa daftari hilo.

Kuhusu mawakili hao sasa kutambulika kama wanasheria wa Serikali ( State Attonerys ) Mwanasheria Mkuu wa Serikali amelitolea ufafanuzi kwa kusema Kila Afisa Sheria aliyeteuliwa au kuajiriwa katika Wizara, Idara inayojitegemea, wakala au serikali za mitaa sasa anakuwa wakili wa serikali na kwa sababu hiyo yuko chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali isipokuwa kwa Wanasheria wa Serikali ambao wapo chini ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

“Hivyo Afisa huyo anachukuliwa kuwa anafanya kazi na kutekeleza majukumu na mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Wizara zao , Idara zinazojitegemea, wakala wa serikali na Serikali za mitaa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataweweza kutoa maelekezo ya jumla au maelekezo mahsusi kwa mawakili wa serikali walio katika utumishi wa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria.

Akawahimiza wanasheria hao kila mmoja wao kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa bidii, maarifa na ujuzi wake huku akitanguliza maslahi ya taifa lake katika kila jambo analokishughulikia. Akahadharisha kwamba, hatasita kuchukua hatua dhidi ya mtumishi yeyote atakaye kiuka maadili ya Mawakili katika utumishi wake.

Awali akifungua Mkutano huo Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, amewataka Mawakili wa Serikali kutumia njia mbadala ya usuluhi katika baadhi kesi za madai pale inapobidi na kufikia usuluhishi nje ya Mahakama. Jaji Mkuu amesema , ikiwa njia ya usuluhishi nje ya mahakama utafanyika, basi utapunguza muda wa undeshaji kwa kesi hizo ambazo nyingine huchukua hadi miaka kumi bila kufikia muafaka.

“Niwaombe wanasheria wa Serikali katika kesi nyingine za madai pale inapobidi wajaribu sana kulenga kufikia usuluhishi wa nje ya mahakama badala ya kuendesha kesi kwa miaka hata kumi, kuanzia kesi inapoanza ngazi ya chini hadi kufikia Mahakama ya Rufani” amesema Jaji Mkuu na Akasisitiza kwamba, “ Kuna wakati wanasheria wa Serikali wanakiri kwa pembeni, kuwa kesi wanayoendesha haina nafasi ya kushinda au hata wakishinda gharama hadi kupata ushindi huyo ni kubwa. Wanapambana tu kwa sababu Mkuu wa Idara au Kitengo amesema hivyo”.

Akasisitiza kwa kusema. “Hapa ndipo ipo haja ya kujenga Imani ya Mawakili hawa ( wa Serikali) na kuwaruhusu wapate usuluhisho wa mashauri nje ya mahakama”.

Akitoa takwimu za Kituo cha Usuluhishi ( Mediation Centre) cha Mahakama Kuu Dar es Salaam kwa mwaka jana ( 2017) kinaonyesha kuwa jumla ya mashauri 41 yalisuluhishwa na kituo bila ya kufikishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa na kati ya hizo, ni 10 tu zilikuwa za taasisi ya Umma.

No comments: