Friday, June 15, 2018

WAISLAM TABORA WAMPONGEZA JPM KWA MISAADA YAKE

SHEIKH wa Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi amemupongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za kusaidia shughuli mbalimbali za kuendeleza miradi ya madhehebu mbalimbali ikiwemo  ya Waislamu hapa nchini.
Alitoa kauli hiyo mara baada ya Swala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa Kimkoa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana (leo) mjini Tabora

Sheikh Mavumbi alisema misaada anayochangia ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za Ibada ni jambo zuri na linamuonyesha kuwa yeye sio mbaguzi  na ameonyesha mapenzi makubwa aliyonayo kwa watu wote bila kujali tofauti zao , hali inayosaidia kuimarisha umoja wa Kitaifa ulioasisiwa tangu uhuru wa Nchi ya Tanzania.

Sheikh huyo wa Mkoa aliwataka Waislamu wote nchini kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli na Serikali yake katika jitihada zake mbalimbali za kuwaletea wananchi maendeleo hapa nchini.

Alitoa wito kwa wakazi wote Mkoani hapa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha mshikamano na upendo ili amani iliyopo iendelee kudumu na waumini waendelea kusali bila wasiwasi katika nyumba zao za Ibada.

Aidha Sheikh Mavumbi aliwataka Masheikh wa ngazi zote na Maimam kuhakikisha kuwa ndoa wanazofungisha zingatie maandiko matakatifu ili kuepuka kusababisha kuwepo na ndoa za utotoni mkoani humo.

Alisema ni vema kabla ya kufungisha ndoa  viongozi hao wakahoji ili kujua kama binti anayekusudiwa kufungishwa ndoa umri wake unaostahili na sio mtoto.

Kwa upande wa suala la elimu Sheikh huyo aliwasisitiza Waislamu wote kuhakikisha wanawahimiza watoto kuzingatia masomo na kuhudhuria shuleni bila kukosa ili kuuepusha Mkoa wa Tabora kuwa miongoni mwa Mikoa inaoongoza kwa watoto watoro.

Alisema hata Mtume Muhammad SAW pamoja na kutoa mafunzo elimu ya dini anawahimiza Waislam watafuete elimu hata ikiwa mbali kama vile China na kuongeza ndio maana ni vema kuwahimiza watoto wasome.

Akitoa salamu za Eid El Fitri kwa niaba ya Serikali Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Mwandizi wa Magereza(SACP) Hamza Hamza aliwataka Waislamu wote kuonyesha wamefuzu kwa kuendeleza mema yote waliofundishwa na viongozi wa dini kwa ajili ya kudumisha amani na upendo hapa nchini.

Alisema mafundisho waliyopata katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani yakawe Darasa la kuwafanya Waislam waendelee kutii Sheria za Nchi na Serikali kwa ajili kuendelea kuwa na mazingira mazuri na tulivu ya kufanya Ibada.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Tabora Ramadhan Rashid aliwataka Waislam Mkoani Tabora kutumia mafunzo waliyoyapata katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuendeleza mazuri yote na kuacha vitendo kama vile ulevi, ugomvi, uzinifu na vingine ambavyo vitawafanya kutenda dhambi.

Alisema ni vema kuanzia sasa na kuendelea wakaendeleza mshikamano , upendo na matendo ya uhuru kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu baina yao na watu wa madhehebu mengine.
 Sheikh  wa Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi (mbele) akiongoza Swala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa Kimkoa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana (leo) mjini Tabora.
 Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislaam wakiwa katika Swala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa Kimkoa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana (leo) mjini Tabora.


 Baadhi wakimama wa dini ya Kiislam wakisikiliza salamu za Eid El Fitri kwa niaba ya Serikali kutoka kwa  Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Mwandizi wa Magereza(SACP) Hamza Hamza (hayupo katika picha) mara baada ya Swala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa Kimkoa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana (leo) mjini Tabora.
 Sheikh  wa Mkoa wa Tabora Ibrahim Mavumbi (mbele) akisikiliza salamu za Eid El Fitri kwa niaba ya Serikali kutoka kwa  Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Mwandizi wa Magereza(SACP) Hamza Hamza mara baada ya Swala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa Kimkoa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana (leo) mjini Tabora.
Baadhi ya Wakinababa wa dini ya Kiislam wakisikiliza salamu za Eid El Fitri kwa niaba ya Serikali kutoka kwa  Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Mwandizi wa Magereza(SACP) Hamza Hamza (hayupo katika picha) mara baada ya Swala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa Kimkoa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi jana (leo) mjini Tabora.

No comments: