Tuesday, June 26, 2018

VYUO MBALIMBALI HAPA NCHINI VYATAKIWA KUHAMASISHA WATOTO WA KIKE KUPENDA MASOMO YA SAYANSI

Na Pamela Mollel,Arusha

Vyuo mbalimbali nchini vimetakiwa kuhamasisha wanafunzi wa kike kupenda kusoma masomo ya sayansi kuanzia ngazi za chini ili kuondoa changamoto ya uhaba wa wanasayansi wa kike uliopo hapa nchini. 

Aidha imeelezwa kuwa, kumekuwepo na uhaba mkubwa wa wanasayansi wanawake katika sekta mbalimbali hali inayochangiwa na kuwepo Kwa idadi ndogo ya wanafunzi wa kike wanaohitimu vyuoni. 

Hayo yalisemwa Jana na Mkurugenzi wa ufuatiliaji na udhibiti kutoka baraza la elimu ya ufundi, Dokta Annastella Sigwejo wakati akifungua kongamamno la kiteknolojia lililowashirikisha wanavyuo mbalimbali na makampuni jijini Arusha. Alisema kuwa, ili kuhakikisha tunapata wanasayansi wa kutosha ni lazima tuanze kuhamasisha wanafunzi wakiwa tangu ngazi za chini mashuleni ili wajijengee tabia ya kupenda masomo hayo hadi kufikia ngazi za juu .

Dokta Sigwejo alisema kuwa,kwa sasa hivi ambavyo nchi yetu inahamasisha Tanzania ya viwanda ni lazima kuwepo na wataalamu wanasayansi wa kutosha ambao wataweza kuziba mapengo mbalimbali yaliyopo na hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhamasisha wanavyuo kupenda masomo ya sayansi. 

Kwa upande wa Mkuu wa idara ya Tehama upande wa taalamu kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha, Pamela Chogo alisema kuwa, kongamano hilo ni la kwanza kufanyika jijini Arusha ambapo wameweza kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo mbalimbali wanaosoma masomo ya sayansi jijini hapa pamoja na makampuni ili wajadili changamoto mbalimbali zilizopo .

Alisema kuwa, kumekuwepo na changamoto kubwa ya makampuni mengi kutokupenda na kuzidhamini Kazi zinazozalishwa na wazawa, hivyo kupitia kongamano hilo wanavyuo wataweza kuonyesha Kazi zao Kwa makampuni mbalimbali ili waweze kuzitambua na kuanza kuzitumia. 

Aliongeza kuwa, kumekuwepo na vyuo vingi Sana hapa nchini ambavyo vimekuwa vikizalisha wataalamu wanasayansi lakini wamekuwa wakikosa ajira kwenye makampuni ya hapa nchini kutokana na kutodhamini kazi zao wanazofanya. "tumeamua kuwakutanisha wanavyuo mbalimbali na makampuni ili waweze kutambua umuhimu wa kuwatumia wanasayansi wetu na kuweza kuona Kazi wanazofanya ili mwisho wa siku waweze kuwadhamini wazawa na kutumia Kazi zao. "alisema Chogo. 

Kwa upande wa baadhi wanavyuo katika kongamano hilo, Faith Felix alisema kuwa, uwepo wa kongamano hilo unasaidia Sana kuwapa uelewa zaidi kuhusiana na kile wanachofanya sambamba na kuonyesha Kazi zao Kwa makampuni ili waweze kuwatumia. 

Naye mwanachuo mwingine, Hamis Laizer alisema kuwa, swala la kubwa lililopo katika masomo ya sayansi ni kuhakikisha wanafunzi wanahamasishwa kusoma masomo hayo wakiwa tangu wadogo, ambapo alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya vifaa vya teknolojia ili kufanya ubunifu, kutokana na vifaa vilivyopo hapa nchini kuwa vichache na ghali Sana, hivyo waliomba serikali kuleta vifaa zaidi .
Mkurugenzi wa ufuatiliaji na udhibiti kutoka baraza la elimu ya ufundi, Dokta Annastella Sigwejo wakati akifungua kongamamno la kiteknolojia lililowashirikisha wanavyuo mbalimbali na makampuni jijini Arusha,Chuo cha Uhasibu Arusha(Habari Picha na Pamela Mollel Arusha)
Mkuu wa idara ya Tehama upande wa taalamu kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha, Pamela Chogo akizungumza na waandishi wa habari , alisema kongamano hilo ni la kwanza kufanyika jijini Arusha ambapo wameweza kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo mbalimbali wanaosoma masomo ya sayansi jijini hapa pamoja na makampuni ili wajadili changamoto mbalimbali zilizopo .
Kaimu Meneja Mamlaka ya Mawasiliano kanda ya Kaskazini Francis Msungu,akizungumza na vyombo vya habari alisema ni vyema watumiaji wa mitandao wakafanya matumizi salama ya kuelimisha na kuhabarisha zaidi
Wadau wa mkutano huo
Faith Felix chipukizi katka teknolojia ,anawataka watoto wa kike kuziingiza katika teknolojia kwakuwa fani hiyo si kwa wanaume tu 
Hamis Badru ambaye pia ni mwanateknolojia anawataka watanzania kupenda maswala ya teknolojia

No comments: