Saturday, June 16, 2018

TFDA YATOA MSAADA TAULO ZA KIKE KWA WANAFUNZI WA KIKE ZAIDI YA 3000 KIDATO CHA NNE WALIOPIGA KAMBI ZA KITAALUMA SIMIYU

Kutoka kulia Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Kanda ya Ziwa, Moses Mbambe na Meneja Mawasiliano wa TFDA Guadencia Simwanza wakimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka taulo za kike zilizotolewa Mamlaka hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa kidato cha nne zaidi ya 3000 walio katika kambi za kitaaluma mkoani humo, kushoto ni baadhi ya wananfunzi hao wakipokea kwa niaba ya wenzao, katika Shue ya Sekondari Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa saba kulia) katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu na wanafunzi wa kike walio katika Kambi ya kitaaluma Shule ya Sekondari Bariadi baada ya kupokea msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 wa kidato cha nne walio katika kambi za Kitaaluma ambao umetolewa na wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) .Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa saba kulia) katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu na wanafunzi wa kike walio katika Kambi ya kitaaluma Shule ya Sekondari Bariadi baada ya kupokea msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 wa kidato cha nne walio katika kambi za Kitaaluma ambao umetolewa na wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) .

Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) Kanda ya Ziwa, Moses Mbambe akizungumza na wanafunzi wa Shule za Sekondari Bariadi, Somada, Chenge na Gudui kabla ya kukabidhi msaada wa taulo za kike uliotolewa na Mamlaka hiyo kwa wanafunzi wa kike wa kidato cha nne walio katika kambi za kitaaluma mkoani Simiyu, katika Shule ya Sekondari ya Bariadi Mjini Bariadi.


Meneja Mawasiliano wa TFDA Guadencia Simwanza akizungumza na wanafunzi wa Shule za Sekondari Bariadi, Somada, Chenge na Gudui kabla ya kukabidhi msaada wa taulo za kike katoni 210 uliotolewa na Mamlaka hiyo kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 wa kidato cha nne walio katika kambi za kitaaluma mkoani Simiyu, katika Shule ya Sekondari ya Bariadi Mjini Bariadi ambapo shule hizo zimeweka kambi.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye suti nyeusi katikati) katika picha ya pamoja wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Bariadi walio katika Kambi ya kitaaluma Shuleni hapo baada ya kupokea msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 wa kidato cha nne walio katika kambi za Kitaaluma ambao umetolewa na wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) .

……………………………………………………………………………

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imetoa msaada wa taulo za kike katoni 210 zenye thamani ya shilingi milioni tano na kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa ajili ya wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 wa kidato cha nne walio katika kambi za kitaalum mkoani humo, ambao wanajiandaa na mtihani wa Taifa kwa mwaka 2018.



Akizungumza na viongozi, walimu na wanafunzi wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Bariadi Mjini Bariadi, Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa, Bw. Moses Mbambe amesema msaada huo umetolewa kujibu ombi la Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alilolitoa kwa Mamlaka hiyo kuwasaidia watoto wa kike wa kidato cha nne walio kwenye kambi ya Kitaalum mkoani humo ili wawapo kambini wasome kwa utulivu na kujiamini hususani wakati wa hedhi.



“Tunakabidhi taulo hizi za kike kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa TFDA, Bi. Agnes Sitta Kijo ambazo Mkuu Mkoa wa Simiyu alimuomba ili ziweze kuwasaidia watoto wa kike wa kidato cha nne walioko kwenye kambi za kitaaluma katika maeneo mabalimbali hapa mkoani katika kuwawekea mazingira mazuri ya kusoma kuwa utulivu na kujiamini wakati wa siku zao za hedhi” alisema



Aidha, Mbambe ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa kuanzisha utaratibu wa kambi za kitaaluma na akawataka wanafunzi kuwa na ndoto, kusoma kwa bidii na kuweka mikakati ya kuwawezesha kufikia ndoto zao; huku akiwaasa kufanya vizuri katika mitihani yao ili kutoa nafasi kwa walio nyuma yao kuwekewa utaratibu endelevu wa kambi za kitaaluma katika kuuwezesha mkoa huo kufanya vizuri kielimu.



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bi. Agnes Sitta Kijo kwa msaada taulo za kike ambao amesema utawasaidia sana watoto wa kike ambao wengi wao wamekuwa wakitumia vipande vya kanga na vitenge kujisitiri wakati wa hedhi.



“Ni wazazi wachache sana wenye uelewa kwamba binti zao wamevunja ungo na wao kama wazazi wanatakiwa kuwapa fedha ya kununulia taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri wakati wa siku zao za hedhi, matokeo yake mtoto wa kike katika mazingira fulani anajikuta anashawishika kuingia kwenye mambo yasiyofaa kwa kupewa pedi tu na bodaboda kwa kuwa anaona huyo ndiyo boyfriend(rafiki wa kiume) mzuri” alisema Mtaka.



Kwa upande wa wanafunzi hao wameshukuru kwa msaada wa taulo hizo ambazo wamesema zitawasaidia sana kwani baadhi yao wamekuwa wakitumia vipande vya kanga, vitenge na njia nyingine za kienyeji kujihifadhi wakati wa hedhi , hivyo wamefarijika kwa msaada huo

“Tunawashukuru sana TFDA kutupa hizi taulo za kike maana wengi wetu huwa wanatumia kanga na vitenge kujisitiri, msichana akiwa hedhi halafu akatumia taulo maalum anakuwa anajiamini, anasoma kwa amani na utulivu mkubwa tofauti na atakayetumia njia za kienyeji” alisema Magulu Deogratius kutoka Shule ya Sekondari Bariadi.

Katika hatua nyingine walimu na wanafunzi wa shule za sekondari Bariadi, Chenge, Gudui na Somanda zote za Wilaya ya Bariadi walimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Viongozi wote kwa kuanzisha utaratibu wa kuwa na kambi za kitaaluma, ambao wamekiri umewasaidia wanafunzi kuwa na mtazamo tofauti katika masomo na wakaomba uwe endelevu.

“Utaratibu wa makambi umewasiadia sana wanafunzi wetu, kwanza wameongeza ari ya kusoma yaani hawalali, kila tunapowafundisha wamekuwa wasikivu kwa kuwa wanakiri wanapokea vitu vipya ambavyo hawakousoma shuleni kwao, tunaomba utaratibu huu uendelee maana tuaimani utawasaidia wanafunzi wetu kujiandaa vema na mitihani ya Taifa” alisema Mwalimu Zuhura Yahaya

“Tangu tumeanza kambi hii tarehe 03 Juni imetusaidia sana kuleta mabadiliko ya Kitaaluma, tunapata nafasi ya kubadilisha uzoefu wa kujibu maswali, mada ngumu tunasaidiwa na walimu wetu, tunaelekezwa namna sahihi ya kujibu maswali; naomba tukuhakikishie Mkuu wa Mkoa matokea ya mwaka 2018 yatakuwa ya mfano; yaani binafsi naona siku hazitoshi kama itawezekana mwezi wa tisa turuhusiwe kuja kambi tena” alisema Veronica Kidana kutoka Shule ya Sekondari Chenge.

Jumla ya Kambi za kitaaluma 149 zinaendelea kwa muda wa siku 21 mwezi huu katika maeneo mbalimbali ya mkoani Simiyu, ambapo kambi 35 ni kwa jili ya wanafunzi wa kidato cha nne na kambi 114 ni kwa shule za msingi, kwa ajili ya maandalizi ya Mitihani ya Taifa ikiwa ni moja ya mkakati wa kuondoa daraja sifuri na daraja la nne kwa kidato cha nne na kupandisha ufaulu wa darasa la saba.

No comments: