Saturday, June 30, 2018

SUMATRA YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO

Na EmanuelMadafa,Mbeya.

MAMLAKA ya Udhibiti na Usafirishaji wa Nchi Kavu na Reli, (SUMATRA),imeanza kutekeleza agizo la Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi . Atashasta Nditiye,ambalo lilielekeza kuanza kutoa elimu kwa wadau na watumiaji usafiri njia ya reli ili kupunguza vitendo vya uhujumu uchumi vinavyofanywa na watu ambao si waadilifu.

Akizungumza Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya Mdhibiti na Mkaguzi wa Usalama wa Reli, kutoka Mamlaka ya Udhibiti SUMATRA, Mhandisi . Hanya Mbawala,amesema tayari Mamlaka hiyo imenza kutekeleza agizo la Waziri ambapo wameanza kutoa elimu hiyo kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa reli hiyo katika stesheni ya Chimala.

Amesema, kazi ya kitengo cha reli ndani ya SUMATRA ni kuhakikisha usafiri wa reli unakua salama na uhakika na jambo hilo linafanyika kwa kitengo kuendesha kaguzi za mara kwa mara ikiwa na kuishauri serikali na TAZARA kwa ujumla ya nini kifanyike.

Amefafanua kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mwezi Mei mwaka huu akiwa Ifakara, alitoa maagizo ambayo tayari mamlaka imeanza kuyafanyia kazi, hivyo hatua iliyopo kwa sasa ni kutoa elimu kwa wadau na watumiaji wa reli kuanzia eneo la Makambako hadi Tunduma.

Amesema, eneo la Makambako/ Tumduma ambako reli hiyo inapita , limekuwa likihujumiwa sana kwa watu kuiba vifaa na kuharibu miundombinu ya reli hivyo mamlaka hiyo inakusudia kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kupitia viongozi wa serikali ambao ndio walengwa wakubwa wa elimu hiyo.

Mhandisi Hanya ameeleza kuwa usafiri wa reli ni salama na usioleta madhara kwa barabara, nani usafiri wa haraka na bei nafuu kwa usafirishaji hivyo serikali imeona umuhimu huo na ndio maana sasa maboresho yanafanyika na reli kurejea kwenye ubora wake, kwani usafiri wa reli ndio usafiri pekee unaoaminika na ndio unaokuza uchumi wa nchi.

Akizungumzia hali ya Usalama wa Reli hiyo ya Tazara Ndugu Sadiki Athony ,ambaye ni meneja usalama Tazara amesema eneo korofi kwa sasa ambalo limekuwa likihujumiwa mara kwa mara ni eneo la Inyala hadi Mbeya ambapo matukio ya kutoa vyama ndani ya daraja hali ambayo imekuwa ikihatarisha usalama wa abiria wanaotumia usafari wa reli hiyo ya Tazara.

Amesema wizi wa vyuma vya madaraja stesheni ya Ilongo na Mbeya Mjini, unaendelea kuitia hasara serikali kwani hivi karibuni daraja namba 248 kuna vyuma vimeibiwa na hii si mara ya kwanza, hivyo elimu hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza madahara hayo.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya mbarali Ndugu Rubeni Mfune amesema atahakikisha elimu hiyo inawafikia zaidi wananchi walio wengi pamoja na kuwataka watendaji wa vijiji kuingiza agenda ya ulinzi wa reli kwenye vikao vyao .
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Ndugu Rubeni Mfune akizungumza na Viongozi wa vijiji na wananchi (hawapo pichani)ambao wana ishi maeneo ya jirani na njia ya Reli ya Tazara katika Stesheni ya Chimala Wilayani humo .
Mdhibiti na Mkaguzi wa Uslama wa Reli, kutoka Mamlaka ya Udhibiti SUMATRA, Eng. Hanya Mbawala akisisitiza jambo katika mkutano na wananchi na watendaji wa vijiji (hawapo pichani) ambao wanaishi pembezoni na njia ya reli ya Tazara katika stesheni ya Chimala wilayani Mbarali Mkoani Mbeya June 29 ,2018.
Wananchi na Viongozi wanaoishi pembezoni mwa Reli ya Tazara katika Stesheni ya Chimala Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya wakisikiliza kwa makini maelezo yanayotolewa katika mkutano uliotishwa na viongozi wa Sumatra na Tazara katika kutoa elimu ya ulinzi wa Reli hiyo.
Meneja Usalama wa Reli ya Tazara Ndugu Sadick Anthony akizungumza na wananchi na Viongozi wa vijiji wanaoishi pembezoni mwa reli ya Tazara (hawapo pichani)katika mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Sumatra kwa lengo la kutoa elimu juu ya ulinzi wa reli ya Tazara .
Afisa mtendaji kijiji cha Iliumfilo kata ya Chimala Wilaya Mbarali Ndugu Adel Mwalioteti akitoa maoni yake katika mkutano huo katika ukumbi wa stesheni ya Chimala .
Afisa Mtendaji kijiji cha Matamba kata ya Mapogolo Wilayani Mbarali Anyagile Adam ,akichangia jambo katika mkutano uliotishwa na Sumatra pamoja na Tazara kwa lengo la kutoa elimu ya Ulinzi wa Reli ya Tazara katika ukumbi wa stesheni ya Chimala Mbarali

No comments: