Saturday, June 30, 2018

NIDA KUTUMIA MAONESHO YA BIASHARA KUTOA VITAMBULISHO KWA WAKAZI WA MKOA DAR

Bi. Rose Joseph Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA akifafanua jambo wakati alipkuwa akihijiwa na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya biashara ya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam yanayoandaliwa na Mamlaka ya Mendeleo ya Biashara TANTRADE.
Baadhi ya wananchi mbalimbali wakipata maelezo kwa mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika Maonesho ya Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam leo.
Muonekano wa Banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA katika maonesho ya Sabasaba.


MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)imewataka wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao hawana vitambulisho vya Taifa kufika kwenye banda lao lililopo Maonesho ya biashara ya kimataifa Sabasaba jijini Dar es Salaam ili wapate vitambulisho.

Akizungumza leo kwenye maonesho hayo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Rose Joseph amesema pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu NIDA na majukumu yake pia wameamua kutumia maonesho hayo kutoa vitambulisho kwa wananchi wa mkoa huo.

Amesema kuwa hivyo kwa anayehitaji kitambulisho cha Taifa atatakiwa kuwa na viambatanisho muhimu vikiwemo cheti cha kuzaliwa, cheti cha taaluma, leseni au kadi ya bima ya afya.Amesema kwa watakaofika wakiwa na vielelezo vyao itakuwa rahisi kujaziwa fomu na kisha kupata kitambulisho cha taifa ambacho kina umuhimu mkubwa na ni vema kila mwananchi mwenye sifa akikapata.

“Tumeamua kutumia maonesho ya biashara ya kimataifa ya 42 kuhakikisha wananchi wa Dar es salaam ambao hawakuwa na vitambulisho vya taifa basi wanavipata.“Kwa hapa kwenye maonesho tutatoa vitambulisho kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tu na wale wananchi wa mikoa mingine wao watapata kupitia ofisi zetu zilizoko mikoani,”amesema.

Amefafanua changamoto kubwa iliyopo katika kuandikisha vitambulisho vya taifa ni baadhi ya watu kutokuwa na viambatanishi muhimu ,hivyo wanashauri ni vema kila anayekwenda kuchukua kitambulisho akawa na vilelezo vyote muhimu.Wakati huo amesema NIDA kwa kutambua uwepo wa makundi yenye mahitaji maalumu nchini , ipo katika mchakato wa kutoa vitambulisho kwa kundi la watu wenye ulemavu wa kusikia.

Amefafanua baada ya hapo watakwenda kwenye makundi mengine na lengo ni kuhakikisha nao wanakuwa na vitambulisho vya taifa.

“Ni jukumu letu kuhakikisha vitambulisho vya taifa kila mtanzania mwenye sifa anakuwa nacho, hivyo tumeamua kuanzisha mpango maalum ambao huu utajikita kusajili makundi maalumu na tutaanza na kundi la watu wenye ulemevu wa kusikia.Tutakuwa na wakalimani ili kuhakikisha tunafanikisha mpango huo na tunatarajia kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wao,”amesema.

No comments: