Saturday, June 30, 2018

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA 11 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 29 JUNI 2018


UTANGULIZI
 Shukrani
Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutufikisha siku hii ya leo tukiwa na afya njema ambapo tunahitimisha Mkutano wa 11 ulioanza Jumanne tarehe 3 Aprili 2018. 

Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki kikamilifu katika mkutano huu tangu tulipoanza vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge na baadaye Mkutano wa Bunge. Katika mkutano huu, tumeweza kutekeleza kikamilifu wajibu wetu wa Kikatiba kwa kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019. Mtakubaliana nami kuwa Bajeti hii inatoa mwelekeo mzuri wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali kwa wananchi, kama zilivyoainishwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020 pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja tarehe 20 Novemba 2015.

Salamu za Pole
Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Mei, 2018 Bunge lako tukufu lilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kigoma. Nitumie nafasi hii kukupa pole wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu, Mke, Watoto, familia ya marehemu na wananchi wote wa Buyungu kwa kumpoteza mwakilishi wao huyo aliyekuwa na mchango mzuri kwenye Bunge letu tukufu. Vilevile, nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwa Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani Mbunge wa Korogwe Vijijini na Mheshimiwa Angelina Sylvester Mabula, Mbunge wa Ilemela, Mwanza, kwa kufiwa na wenza wao.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu pia nitoe salamu zangu za pole na kuwatakia afya njema na uponyaji wa haraka Waheshimiwa Wabunge wenzetu wote ambao hawapo nasi hapa Dodoma kutokana na sababu mbalimbali za kiafya. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea kulitumikia Taifa letu pamoja na wapiga kura wao. Wabunge hao ni Mheshimiwa Haji Ameir Haji (Mbunge wa Makunduchi); Mheshimiwa Nimrod Elirehemah Mkono (Mbunge wa Butiama); Mheshimiwa Tundu Antiphas Mughwai Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki); Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani (Mbunge wa Korogwe Vijijini); na Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo (Viti Maalum). 

Mheshimiwa Spika, vilevile, tarehe 14 Juni, 2018 tulipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya vijana wetu 10 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Afisa mmoja wa JWTZ, dereva na kondakta wa basi walilokuwa wakisafiria kuelekea Itende mkoani Mbeya kwa ajili ya mafunzo ya vitendo. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata ulemavu katika matukio mbalimbali ikiwemo ajali iliyohusisha basi dogo la abiria na lori la mchanga eneo la Dundani, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani na kuua watu 14 na gari ndogo aina ya Noah iliyopata ajali katika kijiji cha Chingweje wilayani Nanyumbu, Mtwara na kuua watu watano na kujeruhi wengine watatu. Tuendelee kuwaombea marehemu wote Mungu aweke roho zao mahali pema peponi na tuwaombee majeruhi wote Mungu awape nafuu na wapone haraka.

Pongezi
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi; Mheshimiwa Musa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala na Mheshimiwa Najma Murtazar Giga, Mbunge wa Viti Maalum kwa kuchaguliwa tena kumsaidia Mheshimiwa Spika kuliongoza Bunge kwa awamu hii. Mtakubaliana nami kwamba Wenyeviti hawa wameongoza vikao vyetu kwa busara na umakini mkubwa. Vilevile, niwapongeze na kuwashukuru Katibu wa Bunge, Ndugu Stephen Kagaigai na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha kazi zote zilizopangwa kwenye mkutano huu kwa ufanisi mkubwa. 

Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza  Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga Mjini kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), na Mheshimiwa Mboni Mohamed Mhita, Mbunge wa Handeni Vijijini kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Vijana wa Bunge la Afrika. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba na Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kwa juhudi na ushirikiano wao mkubwa uliochangia ushindi wa Mheshimiwa Stephen Julius Masele. Ushindi wake umelipa heshima kubwa Bunge letu na Taifa kwa ujumla. Serikali itaendelea kushirikiana na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika na Rais wa Umoja wa Vijana wa Afrika ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa majibu mazuri waliyotoa wakati wa kujibu maswali mengi ya msingi na ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kujibu hoja za Kamati za Kudumu za Bunge zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kipindi chote cha Bunge hili. Serikali inaahidi kuendelea kuzingatia maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge na kuufanyia kazi. Vilevile, nitumie fursa hii kuwashukuru Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Serikali na Taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kufanikisha shughuli zote za Bunge la Bajeti. Mwisho, nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Watendaji wake kwa kuandaa miswada ya sheria na maazimio yaliyowasilishwa kwenye mkutano huu.

SHUGHULI ZA BUNGE

Mheshimiwa Spika, tunapohitimisha mkutano huu, tumeweza kukamilisha mjadala wa miswada miwili, kupitisha maazimio ya Bunge mawili na kupokea kauli saba za Serikali. Aidha, Serikali ilipokea maswali ya msingi, ya nyongeza na ya papo kwa papo kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.

Maswali na Majibu
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu jumla ya maswali 530 ya msingi na mengine 1,852 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge. Maswali hayo yalijibiwa na Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Katika kipindi hiki Ofisi ya Bunge iliendesha semina mbalimbali kwa Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa uelewa mpana wa masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu.

Miswada ya Serikali
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Bunge lako tukufu  limejadili na kupitisha bajeti za Wizara zote 21 na bajeti nzima ya Serikali Kuu. Aidha, Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa Mwaka, 2018 (The Appropriation Bill, 2018) na Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018 (The Finance Bill, 2018) ilijadiliwa na kupitishwa kwa hatua zake zote.

Maazimio ya Bunge
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika Mkutano huu Bunge liliridhia maazimio mawili ambayo ni: 
Azimio la Bunge la kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (The Paris Agreement Under the UN Framework Convention on Climate Change). 
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uamuzi wake wa kuendeleza mji wa Dodoma na kuupa hadhi ya Jiji.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaungana na Bunge lako tukufu kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi huu muhimu ambao naamini utasaidia kuendeleza kwa kasi Jiji la Dodoma. Aidha, katika kuhakikisha Jiji la Dodoma linaepuka adha ya kuwa na msongamano wa magari; Serikali ina mpango wa ujenzi wa barabara ya pete (outer ring road). Barabara hiyo yenye urefu wa km. 104, itahusisha maeneo ya Mtumba, Veyula, Nala na Matungulu. Kukamilika kwa barabara hiyo ambayo ipo katika hatua ya usanifu, kutasaidia Jiji la Dodoma kukabiliana na changamoto za msongamano barabarani.

Kauli za Serikali
Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu, Serikali ilitoa kauli mbalimbali kama ifuatavyo:
Kauli ya Serikali kuhusu watumishi walioondolewa kwenye Mfumo wa Malipo ya Mshahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kufaulu mtihani wa elimu ya kidato cha nne;
Kauli ya Serikali kuhusu Matumizi ya shilingi trilioni 1.51;
Kauli ya Serikali kuhusu upungufu wa mafuta ya kula;
Kauli ya Serikali kuhusu kuibuka kwa ugonjwa mpya kwenye zao la korosho;

Maelezo ya Serikali kuhusu katazo la Serikali la kusafirisha Activated Carbon kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine; 
Maelezo ya Serikali kuhusu Maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuingia katika Mgahawa wa Bunge kufanya ukaguzi wa samaki waliovuliwa kimakosa; na
Kauli ya Serikali kuhusu fursa kwa wasichana kujipima uwezo katika riadha ili waweze kuiwakilisha nchi kwenye mashindano yajayo ya kimataifa ya Olimpiki, All – Africa Games na mengineyo.

MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI 2018/2019 

Mheshimiwa Spika, mkutano huu tunaouhitimisha leo ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango mingi mizuri mliyoitoa wakati wa mjadala wa hoja kuhusu Mpango na Bajeti ya Serikali.  

Mheshimiwa Spika, wakati wa kuhitimisha mijadala ya bajeti za wizara, ilionekana dhahiri kwamba muda haukutosha kwa Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kutokana na hali hiyo, kama walivyoahidi Waheshimiwa Mawaziri wakati wa majumuisho ya Hotuba za Wizara zao, Serikali itaendelea kutoa majibu na maelezo ya ufafanuzi kwa maandishi kwa zile hoja ambazo hazikupata nafasi ya kujibiwa kwa sababu ya ufinyu wa muda. Napenda nami nitumie muda huu kutoa maelezo machache ya ufafanuzi kwa baadhi ya maeneo huku nikiamini kwamba mengi yamejibiwa na wizara husika wakati wa mijadala mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 20.47 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya Bajeti na shilingi trilioni 12.01, sawa na asilimia 37 ya Bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha Bajeti hii nzuri ya Serikali yenye dhamira ya “kuendelea kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Nawasihi sana Watanzania wote pamoja na wadau wa maendeleo tushirikiane kwa pamoja katika utekelezaji wa Bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, Serikali itasimamia ipasavyo utekelezaji wa Bajeti sambamba na kuongeza uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha zilizoelekezwa katika vipaumbele mbalimbali kama ilivyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu. Hali kadhalika, Serikali itaimarisha ukaguzi katika ngazi zote na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba miradi na kazi zitakazofanyika zinawiana na thamani ya fedha za umma zinazotolewa na Serikali (Value for money).  Katika kutekeleza Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali itashirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote kwa ujumla ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba malengo ya ukusanyaji wa mapato na matumizi yanazingatia Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imetoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali katika ngazi zote kuwajibika ipasavyo katika ukusanyaji wa mapato na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha na rasilimali za Taifa. Viongozi na watendaji wote wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma katika eneo la ukusanyaji wa mapato. Vilevile, taasisi zote za Serikali zinasisitizwa kutumia mifumo ya kieletroniki kukusanya mapato na wafanyabiashara wote wanahimizwa kutumia mashine za EFD na kulipa kodi kwa hiari.

KILIMO NA MIFUGO

Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II)
Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo yalikuwa na hoja nyingi katika mjadala wa Bunge la Bajeti ni suala la Kilimo hususan uendelezaji wa mazao makuu ya biashara na uwekezaji katika kilimo. Hata hivyo, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba tarehe 4 Juni 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (Agricultural Sector Development Programme - ASDP II). Lengo la Programu hii ni kuongeza tija na uzalishaji katika mnyororo wote wa thamani (value chain) ili kuvipatia malighafi viwanda vitakavyoanzishwa na kupata ziada ya  kuuza katika masoko ya nje ya nchi kwa lengo la kupata faida kubwa. 

Mheshimiwa Spika, programu hiyo inaweka mkazo katika maeneo makuu manne kama ifuatavyo:
Usimamizi endelevu wa matumizi ya ardhi na maji katika kilimo;
Kuongeza tija na faida katika kilimo, mifugo na uvuvi;
Kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza thamani ya mazao; na
Kuwajengea uwezo wadau wa sekta katika uratibu, ufuatiliaji na tathmini.

Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa wadau wa kilimo, mifugo, uvuvi na sekta nyingine watumie fursa mbalimbali zinazopatikana katika programu hii ili kutimiza ndoto ya nchi yetu kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Aidha, naagiza taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa ASDP II, ziimarishe usimamizi na ufuatiliaji ili utekelezaji wa programu hii uwe na mafanikio makubwa.

Mkakati wa kuendeleza mazao makuu ya biashara 
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo imeweka kipaumbele kuendeleza mazao ya kilimo yakiwemo mazao makuu matano ya biashara (pamba, tumbaku, korosho, kahawa na chai) kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Serikali itaimarisha mifumo ya usimamizi wa mazao hayo katika ngazi zote kuanzia kijiji hadi Taifa. Maafisa ugani, kilimo na ushirika tayari wamepewa maelekezo mahsusi katika kutekeleza jukumu hilo. Aidha, Serikali imeendelea na jitihada za kufufua na kuimarisha ushirika ili uwe mhimili wa kusimamia masoko na upatikanaji wa bei nzuri kwa mkulima.

Msukumo katika mazao mengine
Mheshimiwa Spika, sambamba na mazao makuu ya kimkakati Serikali imeendelea na jitihada za kuhakikisha mazao mengine yanapewa kipaumbele kwa kuwapa maafisa kilimo malengo ya kusimamia kwa ukamilifu maandalizi na upatikanaji wa pembejeo na masoko. Mazao hayo ni pamoja na ufuta, alizeti, michikichi, mkonge, zabibu, pareto, ngano, n.k.

Mfumo wa Stakabadhi Ghalani
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Stakabadhi Ghalani umekuwa na mafanikio katika maeneo mengi nchini. Hii ni kwa sababu wakulima wadogo na wa kati wanakuwa kwenye Ushirika na hivyo kuwa na nguvu ya soko na kuwapatia wakulima bei nzuri ya mazao yao.  Mathalani, kwa kutumia mfumo huu, mwezi huu bei ya ufuta imeongezeka kutoka shilingi 1,500 kwa mwaka 2017 hadi shilingi 2,800 kwa kilo na kuua mfumo usio rasmi wa uuzaji wa zao hilo ujulikanao kama “chomachoma” ambao  ulimpunja mkulima kwa ujazo na bei. Aidha, mfumo huu unasaidia kuzuia upotevu wa mazao unaotokana na uhifadhi dhaifu, pia unasaidia kuhifadhi mazao ili kusubiri kuuza wakati muafaka na kuyaongezea thamani mazao kabla ya kuyauza. 

Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha kuwa mfumo huu unatekelezwa kikamilifu na kuleta tija kwa wakulima. Hatua hizo ni pamoja na ushirikishwaji muhimu wa Wadau, kuimarisha ushirika, kuweka miundombinu ya masoko na kuboresha muundo wa taasisi na vitendea kazi vya Bodi ya Stakabadhi za Ghala. Natoa wito kwa watendaji Serikalini kuhakikisha kuwa mazao mengi zaidi yanaingizwa katika stakabadhi za ghala ili kuwe na tija kwa wakulima.

Soko la muhogo nchini China
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa fursa ya kipekee ya kufungua soko la muhogo mkavu kutoka Tanzania. Ili kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na fursa hiyo, mwezi Mei, 2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China.  Kufuatia hatua hiyo, mwezi huu wa Juni 2018, tani 74 za muhogo mkavu kutoka Tanzania zimeingia China kupitia Bandari ya Qingdao iliyopo Jimbo la Shandong. Tukio hili la kihistoria linafungua ukurasa mpya wa zao la muhogo kuwa miongoni mwa mazao ya biashara. 

Mheshimiwa Spika, kiasi cha muhogo tulichomudu kuingiza katika soko la China bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ambayo yanazidi tani 150,000 kwa mwaka. Nitoe wito kwa Watanzania wachangamkie fursa ya kilimo cha muhogo ambacho kimeonesha kuwa na tija kubwa. Hali kadhalika, nitoe rai kwa mamlaka zetu hususan vituo vya utafiti wa kilimo kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora na mbinu za kisasa ili kuweza kuongeza uzalishaji na kuuza muhogo China kwa faida kubwa sambamba na kukidhi mahitaji ya soko hilo. Kutokana na zao la muhogo kuonekana kuwa na matumizi mengine zaidi ya chakula, Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuchakata muhogo na kuzalisha bidhaa mbalimbali.

ARDHI

Upimaji wa Mipaka ya Vijiji
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kukabiliana na changamoto ya migogoro ya matumizi ya ardhi miongoni mwa watumiaji kwa kuunda timu ya kisekta ikijumuisha watendaji wa sekta mbalimbali zinazohusika kwa njia moja au nyingine kwenye masuala ya migogoro ya ardhi. Sambamba na hilo, Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kupima mipaka ya vijiji, kutunga na kurekebisha sera, sheria na kuandaa programu mbalimbali za kuboresha matumizi na utawala wa ardhi. Kadhalika, Serikali imeandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. Ni matumaini yangu kwamba programu hii ikitekelezwa, ardhi itatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na pia kudhibiti migogoro ya ardhi. Katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali itaendelea kutatua migogoro inayojitokeza na pia kutoa elimu kwa umma ili watumiaji wote wa ardhi waweze kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa katika vijiji. 

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kudhibiti migogoro kwenye maeneo mbalimbali ya utawala, jumla ya vijiji 11,256 kati ya vijiji 12,545 vilivyopo hapa nchini vimepimwa. Hii ni sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote vilivyopo hapa nchini. Lengo la Serikali ni kupima mipaka ya vijiji vyote vilivyopo na kuvipatia vyeti vya kijiji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo. Hatua hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji. Ili kuharakisha kasi ya upimaji nchini, Serikali itaendelea kutumia makampuni binafsi ya upimaji na upangaji makazi kwa vibali maalum.

UTALII

Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada za Serikali katika kulinda rasilimali za nchi na ushirikiano kutoka kwa wananchi idadi ya wanyama pori imeongezeka hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye wanyama wengi barani Afrika. Ili kuitumia vema fursa ya kuwa na vivutio vingi ikiwemo wanyamapori wengi na kuleta tija kwa nchi, Serikali imeendelea kuandaa utambulisho wa Tanzania kimataifa (Destination Branding). Lengo la utambulisho huo ni kuitambulisha Tanzania kama kituo mahsusi cha utalii duniani; kuvutia wageni wa kimataifa kuitembelea Tanzania; kuongeza wigo wa kutangaza vivutio na kufanya vivutio vya utalii vya Tanzania vifahamike duniani. Aidha, Serikali inakamilisha mchakato wa kuanzisha Channel maalum katika Television ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii na pia Serikali inaendelea na mpango wa kuunda chombo kitakacho simamia fukwe za bahari, mito na maziwa. Lengo la hatua hizo ni kuimarisha utalii wa fukwe Bara na Visiwani kwa kujenga hoteli, maeneo ya mapumziko na michezo mbalimbali ya majini. 

Mheshimiwa Spika, Pia, maandalizi ya kuanzisha studio ya kutangaza utalii kwa njia ya teknolojia ya habari na mawasiliano yanaendelea vizuri. Studio hiyo itawezesha kutambua, kufuatilia na kuwasiliana moja kwa moja na watu wanaofuatilia Tanzania na vivutio vyake kwa njia ya TEHAMA.

HIFADHI YA MAZINGIRA 

Mheshimiwa Spika, misitu yetu inaendelea kukatwa hovyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya mkaa na kuni. Ili kuendeleza matumizi ya nishati mbadala nchini, Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu mahsusi wa kuwawezesha na kuwaratibu wajasiramali wanaojishughulisha na nishati mbadala ili kuwa na uzalishaji wa kutosha wa nishati na iweze kusambazwa kote nchini. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha na kukamilisha Mkakati wa Tungamotaka (National Biomass Energy Strategy) na kusambaza kwa wadau nchini ili kuratibu vyema upatikanaji na utumiaji wa nishati hii. 

NISHATI

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa umeme wa kutosha, wa uhakika na usiotegemea chanzo kimoja, umeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano. Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuzalisha umeme utakaoiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Kwa kuzingatia hilo, Serikali inaendelea kutoa kipaumbele katika matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme ikiwemo maji, gesi, makaa ya mawe, jotoardhi, jua, upepo na tungamotaka. Mathalan, kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa maji katika mto Rufiji MW 2,100 (Stiegler’s Gorge), pia iko katika hatua za maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa umeme wa jua Shinyanga – MW 150 na mradi wa umeme wa upepo Singida – MW 100.

Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu Waheshimiwa Wabunge wengi walishauri Serikali iharakishe utekelezaji wa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini ili maeneo mengi katika majimbo yao ambayo hayana umeme yaweze kufikiwa na huduma hiyo. Aidha, wapo ambao walitaka fedha za REA zitolewe kwa wakati na kama ilivyoidhinishwa na Bunge. Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa  miradi ya awamu ya tatu ya mpango wa REA. 

Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquified Natural Gas – LNG)
Mheshimiwa Spika, kufuatia ugunduzi wa kiwango kikubwa cha gesi asilia, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), inashirikiana na wawekezaji ambao ni makampuni ya kimataifa ya mafuta kuendeleza rasilimali hiyo kwa kujenga Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) kama inavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020. Mradi huo ambao utatumia gesi asilia iliyogunduliwa kwenye kina kirefu cha bahari, una lengo la kuiwezesha Tanzania kuvuna na kuuza rasilimali ya gesi katika soko la dunia sambamba na kukidhi mahitaji ya soko la ndani yanayojumuisha matumizi ya viwandani na majumbani.
Mheshimiwa Spika, madhumuni ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mradi huo mkubwa, wa aina yake na wenye maslahi mapana kwa Taifa letu unatekelezwa kama ulivyopangwa. Aidha, mradi wa LNG unaokadiriwa kugharimu takriban Dola za Marekani bilioni 30 na kuchukua eneo lenye ukubwa wa hekta 2,071.7 pamoja na mambo mengine una faida zifuatazo:
Mosi: Kuongeza mapato ya Serikali kupitia mauzo ya gesi katika soko la ndani na nje;
Pili: Upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya viwanda na matumizi ya nyumbani;
Tatu: Kuwa chanzo cha malighafi za viwanda kwa ajili kuzalisha mbolea, plastiki na kemikali za petroli (Petro-chemicals);
Nne: Kuwa chanzo cha ajira ambapo wakati wa ujenzi wake, mradi huo utaajiri takriban watu 10,000 na wengine wapatao 3,000 wakati wa uendeshaji;
Tano: Kusaidia ukuaji wa uchumi wa miji ya Lindi na Mtwara utakaokwenda sambamba na kupanuliwa kwa bandari na uwanja wa ndege; na
Sita: Kuibua fursa za biashara kwa Watanzania pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kuhusu usimamizi wa miradi ya namna hii.

Mheshimiwa Spika, ni vema tukatambua kuwa mradi huu una maslahi makubwa kwa taifa. Hivyo, Serikali inachukua tahadhari kubwa kwenye majadiliano yanayoendelea baina ya Timu ya Majadiliano ya Serikali (GNT) na Makampuni ya Kimataifa ya Mafuta (IOCs). Serikali inaendelea na majadiliano na makampuni hayo ya mafuta ili mradi huo uanze kutekelezwa mapema kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi yetu.

MSAADA WA KISHERIA

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria kwa kuteua Wasajili Wasaidizi wa watoa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi za Mikoa, Majiji, Wilaya na Halmashauri zote nchini. Lengo la Serikali ni kusogeza huduma ya msaada wa kisheria karibu na wananchi. Hivi sasa Wasajili Wasaidizi wanaendelea kupatiwa mafunzo elekezi ya namna ya kuratibu, kusimamia, kutambua na kusajili taasisi mbalimbali zinazotoa na zinazotaka kutoa huduma hiyo katika maeneo husika. Nitumie fursa hii kuwasihi Waheshimiwa Wabunge, mtakaporudi majimboni, mkawahamasishe wananchi waitumie fursa hii kupata haki zao. Vilevile, ninawaasa wale wote ambao wamepewa dhamana ya kulisimamia zoezi hili la kutoa huduma hii, wafanye kazi kwa weledi na maadili ili huduma hii iwe endelevu na imsaidie mwananchi wa kawaida kuweza kupata haki yake.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini, Serikali ilianzisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kurekebisha muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nia ya Serikali ni kuimarisha huduma za mashtaka; usimamizi na ufuatiliaji wa mashauri ya madai ndani na nje ya nchi ambayo Serikali ina maslahi; kuimarisha uwezo wa Wanasheria wa Serikali katika kushughulikia mashauri ya usuluhishi na mashauri ya madai; kuimarisha usimamizi wa masuala ya mikataba; na kuimarisha uandishi na urekebu wa sheria. Ofisi hizi tatu katika muundo wake mpya, zitaanza kazi rasmi Julai 2018. Nichukue pia fursa hii kuwataka watumishi wataokuwa kwenye ofisi hizi, wafanye kazi kwa weledi, uadilifu na umakini katika kutoa huduma ambazo wamepewa dhamana nazo. 

AFYA
Uimarishaji wa huduma za uzazi, mama na mtoto
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara, wodi za wazazi, nyumba za watumishi na wodi za watoto. Hatua hii itawezesha upatikanaji wa huduma kamili za uzazi na kupunguza vifo vya mama na watoto. Katika mwaka 2018/2019, eneo litakalopewa kipaumbele ni kuimarisha upatikanaji vifaa na watumishi katika vituo 208 vinavyoendelea kuboreshwa. 

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa damu ikiwa ni moja ya mikakati ya kupunguza vifo ikiwemo vitokanavyo na uzazi. Kwa mwaka 2018/2019, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.3 ili kujenga vituo vya kuhifadhi damu (satellite blood banks) kwenye mikoa 12. Mikoa hiyo ni Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Njombe, Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu. Lengo la mpango huo ni kuboresha upatikanaji wa damu hususan kwa akinamama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. Nitumie fursa hii kuwasihi watumishi wa afya waongeze juhudi katika kuhamasisha wananchi kujitolea damu na niwaombe wananchi wawe na utamaduni wa kuchangia damu ili kuwezesha upatikanaji wa damu salama itakayohifadhiwa katika benki zetu. 

Uimarishaji wa Huduma za Kibingwa
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za kibingwa nchini. Moja ya hatua zinazochukuliwa ni kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ambapo shilingi bilioni 14 zimetengwa kwa ajili ya kuanzisha huduma ya kuchunguza mwili bila upasuaji (PET Scan). Kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hiki na kuokoa takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kulipia wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hiki. Aidha, Serikali itasogeza huduma ya tiba ya saratani katika ngazi ya Hospitali za Kanda ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya Kanda ya Kaskazini KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, jijini Mbeya. 

Vilevile, katika mwaka 2018/2019 Serikali itaimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa tiba na madaktari bingwa. Jumla ya shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha hospitali hizi. 

ELIMU

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kutokuwepo kwa miundombinu ya kutosha katika shule za msingi na sekondari. Hali hiyo imechangiwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza, kidato cha kwanza na wale wanaojiunga na kidato cha tano kila mwaka ikiwa ni sehemu ya  utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi Bila Malipo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for Results - EP4R)  imeendelea kuimarisha miundombinu muhimu kwenye shule mbalimbali zenye uhitaji mkubwa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatumia shilingi bilioni 155.58 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe 25, ununuzi wa vifaa vya maabara, ujenzi wa mabwalo 85, vyumba vya madarasa 2,000 na motisha kwa Halmashauri kutokana na ufanisi katika utekelezaji wa vigezo vya EP4R.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo Serikali inaendelea kuajiri walimu wapya. Kwa sasa, Serikali inatarajia kuajiri walimu 4,785 wa shule za msingi zenye uhitaji mkubwa. Aidha, tayari Serikali imetangaza nafasi za ajira kwa walimu 2,000 wa masomo ya sayansi, hisabati na lugha (Literature in English) ambao watapangwa kwenye shule za sekondari zenye uhitaji mkubwa. Kadhalika, Serikali pia imetangaza nafasi za ajira kwa mafundi sanifu maabara 160 ambao pia watapangwa kwenye shule zenye uhaba wa wataalamu hao.

MAJI

Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kulikuwa na hoja kuhusu hali isiyoridhisha ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini. Changamoto nyingine iliyozungumzwa ni udhaifu kwenye usimamizi wa miradi ya maji. Maeneo mengi nchini yameendelea kukabiliwa na uhaba wa maji kutokana na sababu mbalimbali. Sababu hizo ni pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji, ukataji holela wa miti na uchomaji misitu, ongezeko la watu na mifugo, athari za mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya maji yasiyozingatia tija na ufanisi. Aidha, tatizo la maji pia limechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zisizowiana na uwekezaji katika miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa miradi ya maji inatekelezwa ipasavyo, Serikali imeamua kufanya yafuatayo: 
Mosi; Kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa bora, yenye kuwiana na thamani halisi ya fedha pamoja na kukamilishwa kwa wakati kama ilivyo katika mikataba. Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa watendaji wote watakaobainika kutotekeleza majukumu yao ipasavyo. 

Pili; Kuunda Kamati Maalum itakayochunguza miradi yote ya maji vijijini ili kujiridhisha na utekelezaji wake. Kamati hiyo inatarajiwa kuwasilisha maoni na ushauri utakaowezesha Serikali kuona namna bora ya kusimamia miradi ya usambazaji maji vijijini na mijini. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla, kuipa Kamati ushirikiano wa kutosha ili ikamilishe majukumu yake kwa wakati.

UTAWALA BORA NA MASUALA YA WAFANYAKAZI

Mheshimiwa Spika, utumishi wa umma wenye ufanisi ni nyenzo muhimu ya kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Kwa kutambua hilo, Serikali inaendelea kuchukua hatua kupunguza gharama za uendeshaji na urasimu katika utoaji wa huduma, kurejesha nidhamu, uadilifu, uwajibikaji katika utumishi wa umma pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa. 

Mheshimiwa Spika, ili kufikia azma hiyo, tarehe 23 Juni, 2018, Serikali ilizindua mifumo tisa ya TEHAMA inayohusu utoaji huduma Serikalini. Mifumo hiyo ni mfumo wa usajili wa vizazi na vifo, mfumo wa taarifa za kitabibu, mfumo wa taarifa za ununuzi, mfumo wa kumbukumbu za kielektroniki, na mfumo wa ofisi mtandao. Mingine ni mfumo wa ankara pepe na ulipaji wa Serikali, mfumo wa utoaji huduma za Serikali kupitia simu za mkononi, mfumo wa baruapepe wa Serikali na mfumo wa vibali vya kusafiri.

Mheshimiwa Spika, mifumo hiyo itahakikisha kuwa huduma zinazotolewa na taasisi za umma kwa wananchi zinaboreshwa, sambamba na kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku. Hivyo, Serikali itaendelea kubuni na kutumia mifumo ya TEHAMA na teknolojia nyingine rahisi na salama kwa lengo la kuwapatia wananchi hususan wa vijijini huduma bora na kwa wakati. Viongozi na watendaji wa Serikali hakikisheni kuwa mifumo hiyo haitumiki kukwamisha shughuli za Serikali au mipango ya utoaji huduma kwa wananchi. Aidha, wale wote watakaobainika kuhujumu mifumo hii wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kufuatia zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma, Serikali ilipokea malalamiko kutoka kwa watumishi, Vyama vya Wafanyakazi pamoja na Waheshimiwa Wabunge. Hata hivyo, Serikali ilitoa maelekezo kwa waajiri wote nchini kuwarejesha kazini na kuwalipa mishahara stahiki watumishi wote waliokuwa na Ajira za Kudumu au Ajira za Mikataba (Kwa Watendaji wa Vijiji na Mitaa) au Ajira za Muda (Employment on Temporary Terms) ambao walikuwa kazini kabla ya tarehe 20 Mei, 2004 pamoja na Watumishi wa Umma 1,370 waliolegezewa Masharti ya Sifa za Muundo. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuboresha huduma kwa wananchi kwa manufaa na maendeleo ya Taifa letu.

UWEZESHAJI WA VIJANA, WANAWAKE NA WENYE ULEMAVU

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili waweze kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu ikilinganishwa na taasisi nyingine za fedha. Sambamba na hilo, naielekeza mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinatenga kiwango hicho cha asilimia 10 kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na zisaidie uundaji wa SACCOS shirikishi za makundi haya ili wote waweze kunufaika na fursa hiyo. Vilevile, naielekeza mikoa yote na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo hazijakamilisha uundaji wa kamati za kuhudumia watu wenye ulemavu zihakikishe kamati hizo zinaundwa ikiwa ni pamoja na kuziwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu. 

Napenda kusisitiza kuwa yatengwe maeneo mahsusi kwa ajili ya watu wenye ulemavu ili waweze kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi.

HUDUMA ZA HIFADHI YA JAMII

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii hapa nchini, mapema mwaka huu, Bunge lako tukufu lilitunga Sheria Na. 2 ya mwaka 2018 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma. Sheria hiyo, imeunganisha mifuko ya pensheni ya PPF, PSPF, GEPF, na LAPF na kuunda mfuko mpya wa kuhudumia watumishi wa umma (PSSSF). Aidha, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefanyiwa marekebisho ili uweze kuhudumia sekta binafsi na isiyo rasmi.

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, taratibu za kuunganisha mifuko hii zimekamilika na mifuko hiyo itaanza kutoa huduma hivi karibuni. Hatua hii, itaboresha huduma za hifadhi ya jamii katika ngazi zote, ili hatimaye wananchi wasilazimike kufuata huduma hizo makao makuu.

UTAMADUNI NA MICHEZO

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019 Tanzania itakuwa mwenyeji wa Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo linalenga kutangaza na kuuza kazi za kiutamaduni na ubunifu, filamu, utalii na masuala mbalimbali ya kihistoria. Tamasha hilo linatarajiwa kuleta wajasiriamali na wadau mbalimbali wa sekta ya utamaduni, sanaa na michezo na ubunifu zaidi ya 1,200 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika tamasha hilo, tunatarajia kuwashirikisha zaidi ya wajasiriamali wa kazi za kiutamaduni, sanaa na ubunifu takriban 20,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Hivyo natoa wito kwa wadau mbalimbali wajitokeze kufanikisha tamasha hilo lenye manufaa makubwa kwa Taifa letu likiwemo kuimarisha masoko ya bidhaa za viwanda na kazi za kiutamaduni, sanaa na ubunifu pamoja na kuitangaza Tanzania na fursa zake nyingi za kipekee zilizopo. Aidha, nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge muwahamasishe wajasiriamali kwa kazi za utamaduni, sanaa, ubunifu na filamu katika maeneo yao ili waweze kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019 Tanzania pia itakuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa miguu wa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON-U17).  Hii ni fursa nyingine ya kipekee ya kutangaza Taifa letu katika nyanja za Kimataifa. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na maandalizi stahiki ambayo yatahusisha pia ukarabati wa miundombinu ya viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo. Natoa wito kwa wananchi watumie vizuri uwepo wa mashindano hayo kujiongezea kipato hususan kupitia biashara ya bidhaa na huduma kwa wageni. Pia, tuiunge mkono timu yetu itakayoshiriki mashindano hayo iweze kupata mafanikio.

KAMPENI DHIDI YA UKIMWI NA VVU

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa Desemba Mosi 2017, katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, alizindua matokeo ya awali ya Utafiti wa Nne kuhusu viashiria vya VVU na UKIMWI. Utafiti huo uliofanyika katika ngazi ya kaya kuanzia Oktoba 2016 hadi Agosti 2017, ulionesha kuwa hamasa ya upimaji wa VVU ni ya kiwango cha chini hususan kwa wanaume.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, tarehe 19 Juni 2018 kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, nilizindua kampeni ya kuhamasisha umma wa Watanzania kupima VVU na kuanza dawa za kufubaza VVU mara wanapogundulika na maambukizo (mpango ujulikanao kama Test and Treat). Kampeni hii inakwenda sambamba na kaulimbiu ya ujumla isemayo: “FURAHA YANGU – PIMA, JITAMBUE, ISHI”.  Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba kampeni hiyo ya siku tano kwa wakazi wa Jiji la Dodoma, imewezesha watu 4,725 kupima afya zao na kujitambua ambapo kati yao wanaume walikuwa 3,061 na wanawake walikuwa 1,664. 

Aidha, kupitia kaulimbiu ya “MWANAUME JALI AFYA YAKO, PIMA VVU” niliridhia kuwa KINARA WA KUHAMASISHA wanaume kupima na kuanza dawa mapema kwa wale wanaogundulika kuwa na maambukizo ya VVU. 

Mheshimiwa Spika, hali ya kujikinga na maambukizo ya VVU nchini bado si ya kuridhisha sana. Mathalan, hadi kufikia Machi, 2018 jumla ya watu wanaoishi na VVU ilikuwa ni 1,022,745. Kati yao watu 1,007,026 walikuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU. 

Mheshimiwa Spika, Tanzania inatekeleza malengo ya 90-90-90 (TISINI TATU) ifikapo mwaka 2020 katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. TISINI TATU zina lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizo; asilimia 90 ya waliopima VVU na kugundulika kuwa wana maambukizo wapatiwe dawa za kufubaza VVU (ARVs); na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU. Nitumie fursa hii kuendelea kuhamasisha wananchi wapime VVU. Nitumie fursa hii kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni ya upimaji na kuongoza Waheshimiwa Wabunge katika upimaji wa hiari tarehe 21 Juni, 2018.  Jambo hili ni muhimu kwetu sisi viongozi. Aidha, kufuatia zoezi hilo, wale watakaogundulika wana maambukizo ya VVU, ninawasihi waanze mara moja kutumia dawa za kufubaza. Waheshimiwa Wabunge, nasi pia katika majukwaa yetu ya kisiasa tuendelee kuunga mkono kaulimbiu ya “FURAHA YANGU - PIMA, JITAMBUE, ISHI” ili Watanzania wajitokeze kwa wingi kupima afya zao popote pale walipo.

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwa mafanikio ningependa kusisitiza masuala yafuatayo:

Mosi: Uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi hususan wale wa vijijini;

Pili: Taasisi zote ziimarishe mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha watanzania;

Tatu: Kusimamia ipasavyo utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II) ili mpango huo uweze kuleta mapinduzi ya kilimo na tija kwa wakulima sambamba na kuchangia ukuaji wa sekta ya viwanda;

Nne: Matumizi ya Mifumo ya Kielektroniki katika kutoa huduma mbalimbali kwa lengo la kuondoa urasimu usio wa lazima katika utoaji huduma kwa wananchi;

Tano: Kuendelea kutumia EFD katika ukusanyaji wa mapato;

Sita: Kuendeleza ushirikiano baina ya Waheshimiwa Wabunge na Halmashauri katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo; na

Saba: Viongozi, watendaji na wananchi wote kuifanyia kazi kaulimbiu ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI isemayo: “FURAHA YANGU - PIMA, JITAMBUE, ISHI”

Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kuwatakia safari njema Waheshimiwa Wabunge wanaporejea majimboni kwao kuwaeleza wananchi mambo yaliyojiri hapa Bungeni. Waelezeni wananchi matarajio yetu kwao na kuwasihi waendelee kutuunga mkono kwenye jitihada zetu za kuwawekea mazingira wezeshi ya kujikwamua kiuchumi. 

Mheshimiwa Spika, vilevile niwashukuru watendaji wa Serikali kwa kufanikisha shughuli zilizopangwa na Bunge lako tukufu kwa weledi, maadili na ufanisi mkubwa. Aidha, niwashukuru wanahabari kwa uchambuzi wao wa hoja zilizokuwa zikiendelea bungeni na kufikisha habari hizo kwa wananchi. Nivishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma wanazozitoa kwa washiriki wa Bunge hili bila kuwasahau madereva waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa bungeni. Nawatakia safari njema.

Mheshimiwa Spika, tunatarajia kwamba tarehe 22 Agosti, 2018 kutegemea mwandamo wa mwezi, kutakuwa na sikukuu ya Eid El Hajj. Nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu na Watanzania wote nchini maadhimisho mema ya sikukuu hiyo.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 04 Septemba 2018 siku ya Jumanne, saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: