NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SERIKALI mkoani Mwanza imezindua klabu ya wachangiaji damu wa kundi maalumu (RH Nagative) na kuahidi kuendelea kuhamasisha jamii iweze kuchangia damu itakayosaidia kuokoa maisha ya watu na kuipongeza Taasisi ya The Desk & Chair Foundation kwa mchango wake wa kujitoa kuhamasisha jamii kuchangia damu.
Klabu hiyo ilizinduliwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mary Tesha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wachangiaji Damu Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure.
Akizungumza baada ya kuzindua klabu hiyo Mongela alisema uhaba wa damu ni changamoto kubwa kwa Mkoa wa Mwanza ambapo mahitaji yake ya damu ni chupa 30,000 na hivyo jamii isisubiri hadi iuguliwe ndugu ndipo ichangie damu.
“Wachangiaji damu waenzie lakini niwapongeze The Desk & Chair Foundation, wamejitoa sana mkoani kwetu na taifa kwa ujumla lakini pia wanafunzi wamekuwa msaada mkubwa kwa kubeba jukumu la kukusanya damu.Hivyo kwa uhaba wa damu mkoani kwetu kila mmoja atambue umuhimu wa kuchangia damu ili wagonjwa waongezwe damu iliyo salama,”alisema Mongela.
Mkuu huyo wa mkoa aliitaka jamii, taasisi za umma, binafsi na za dini zijitoe kuchangia damu kwani damu haina dini, kabila,rangi wala chama bali sote ni wahitaji bwa damu lakini pia halmashauri zisaidie timu za uchangiaji damu ili zitimize wajibu wake wa kukusanya damu itakayokoa maisha ya watu.
Naye Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation alisema wataendelea kushirikiana na serikali kutatua changamoto ya damu katika hospitali na vituo vya afya mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa.
“Tumebaini watumiaji damu ni watoto wa chini ya umri wa miaka 5 na kwa miaka 8 wachangiaji damu ni wanafunzi wa shule za sekondari pamoja na vyuo, hao wanastahili pongezi.Mwaka huu tulikuwa na vituo vitano vya damu tukishirikiana na Kituo cha Damu Salama na tumekusanya chupa 600,”alisema Sibtain.
Hata hivyo Meghjee alieleza kuwa baada ya kubaini kuwepo kwa uhaba wa damu waliamua kushirikiana na Kituo cha Damu Salama ingawa kuhamasisha jamii kuchangia damu ni kazi kubwa na ngumu.
“ Ni kazi ngumu kuelimisha jamii sababu ya mila na desturi hasa vijijini.Wafadhili ni wachache wanaowezesha kupata vifaa muhimu vya kutolea na kuhifadhia damu.Waandishi wa habari nao watenge muda wa kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya damu,”alisema Meghjee.
Kwa upande wake Mhamasishaji Mkuu wa Kituo cha Damu Salama Kanda ya Ziwa Bernadihno Medaa alisema mahitaji ya damu kwa mwaka kanda ya ziwa kwa mwaka ni chupa 130,000 na wanapambana kuhakikisha ndugu ama mwananchi hapotezi maisha kwa kukosa damu.
“ Jamii ya kawaida haijaona umuhimu wa kuchangia damu, wanasahamu kuwa wanaweza kuugua na kuhitaji kuongezwa damu na damu tunayopata asilimia 80 hadi 85 inatolewa na wanafunzi wa vyuo na sekondari.Kila kiongozi akilibeba jukumu hilo tutafikia malengo ya damu,”alisema Medaa na kuvipongeza vyombo vya habari kwa kufikisha ujumbe kwa wakati mahali wasiweza kufika wao.
Hata hivyo Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha maadhimisho hayo kabla ya kufikia kilele Juni 14 umekusanya chupa 1,361 za damu ikilinganishwa na chupa 1,171 za mwaka jana.
Katika ukusanyaji damu huo Wilaya ya Sengerema imeongoza kwa kukusanya chupa 261, ikifuatiwa na Ilemela (240), Nyamagana (231), Ukerewe (174), Kituo cha damu Salama (110), Halmashauri ya Buchosa (107), Hospitali ya Sekou Toure (80),, Misungwi (96), Kwimba (50) na Magu (41) huku Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando ikishindwa kukusanya hata chupa moja.
Mgeni rasmi wa Siku ya madhimisho ya Wachangiaji Damu Duniani Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mary Tesha akizungumza na wadau wa damu. Kushoto wa kwanza ni Mwenyekiti wa The Bakhiyatullah Foundation (TBF) Sheikh Hashimu Ramadhan, wa pili Sibtain Meghjee wa The Desk & Chair Foundation. Kushoto ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure, Bahati Msaki an Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa Na Baltazar Mashaka.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mary tesha aliyemwalikisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela akizungumza na wadau wa damu kwenye maadhimisho ya siku ya Wachangiaji Damu jijini humo.
Mfadhili Mkuu wa Kituo cha Damu Salama Kanda ya Ziwa, Mwenyekiti wa Desk & Chair Foundation akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wachangiaji Damu Duniani iliyofanyika jijini Mwanza kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mary Tesha akichangia damu wakati wa maadhimisho ya Siku ya wachangiaji Damu Duniani wakati wa maadhimisho hayo jana yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure ya Mkoa wa Mwanza, Tesha alimwakilisha Mkuu wa Mkoa John Mongela ambaye alijuwa mgeni rasmi.
Wadau wa damu wakichangia damu kwenye maadhimisho ya Siku ya wachangiaji Damu Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya sekou Toure.
Picha zote na Baltazar Mashaka
No comments:
Post a Comment