Tuesday, June 12, 2018

RAIA 19 WA CHINA, WATANZANIA SITA KORTINI KWA TUHUMA ZA UHUJUMU UCHUMI

Na Karama Kenyunko, blogu ya Jamii

RAIA 19 wa China na watanzania sita, wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao wanashtakiwa chini ya vifungu vya sheria ya uhamiaji, chini ya sheria ya watu ambao siyo raia wa Tanzania na uhujumu uchumi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Huruma Shaidi washtakiwa hao walitajwa kuwa ni, Bo Song, Liu Yunley, Chen Chao Hui, Fu Zeng, Wu Hai Quing, Ke Qiu Fang na Frederick Kumalija.

Wengine Jing Jing Lin, Ku Liao, Yan Yan Geng, Chen Ying Gong, Salim Mahsein Al-Amry, George Elikana, Fatuma Songoro, Bhoke Mwita, Kelvin Ponela, Chen Gwandi, Lin Ben, Rui Guo, Lin Xiangqui, Chen Fa, Wan Li, Robert Mkini na Revocatus Mugisha.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa  Serikali Patrick Mwita akisaidiana na Shedrack Kimaro alidai, kati ya Juni 1 mwaka 2017 na Mei 18 mwaka 2018 walitenda kosa la kwanza, ambapo wanadaiwa siku hiyo, chini ya sheria ya watu ambao siyo raia wa Tanzania, walitoa taarifa za uongo kwa lengo la kupata kibali cha kufanya kazi nchini.

Katika shtaka la pili imedaiwa, Siku na mahali hapo hapo, washtakiwa wote kwa makusudi huku wakijua kuwa ni kosa, walitoa taarifa za uongo kwa Kamishna wa kazi kwa lengo la kupata vibali vya kufanyia kazi. Imeendelea kudaiwa kuwa, katika shtaka la tatu, mshtakiwa Bo Song alijihusisha na kazi nchini bila ya kuwa na Paso ya kuishi nchini. 

Katika shtaka la nne,  washtakiwa, Kumalija, Mwita, Songoro, Ponela, Mkini na Mugusha wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi 2017 na Mei 17 mwaka 2018 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walimsaidia raia wa China, Bo Song kujihusisha na kazi katika Jamihuri ya Muungano wa Tanzania huku wakijua kuwa hana kibali cha kuishi nchini wala kufanya kazi.Katika shtaka la tano, washtakiwa wote wanadaiwa Kuandaa, kusimamia na kusaidia kutoa taarifa za uongo kwa dhumuni la kujipatia kibali cha kufanya kazi na kuishi nchini.

Katika shtaka la mwisho, washtakiwa wote kinyume na sheria ya uhujumu uchumi, walijihusisha na makosa ya kiudanganyifu kwa kuonyesha kwamba walikuwa na vibali vya kuishi nchini Tanzania kutoka idara ya Uhamiaji na vibali vya kufanya kazi kutoka kwa Kamishna wa kazi nchini huku wakijua kuwa siyo kweli.Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Aisha DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya washtakiwa kwa ajili ya maslahi ya nchi na washtakiwa. Wakili wa utetezi Peter Kibatala alipinga hati hiyo na kudai hati hiyo ya DPP haizuii mahakama kuangalia na kutoa uamuzi.Aidha amedai kuwa, hati hiyo haioneshi ni jinsi gani maslahi ya nchi wala watuhumiwa yatakavyoathiriwa.

Wakili wa Serikali, Mwita amepinga hoja hizo na kudai, kwa mujibu wa sheria ya kesi za uhujumu uchumi, DPP akiweka hati mahakama haina mamlaka ya kuhoji hicho kibali .Baada ya mabishano ya kisheria, Hakimu Shaidi amesema atatoa uamuzi dhidi ya washtakiwa kama wapate dhamana ama la Juni 14, mwaka huu.

No comments: