Tuesday, June 12, 2018

TANROAD YADAIWA KUKWAMISHA MRADI KUFUNGULIWA

Wakala wa barabara Mkoani Ruvuma TANROAD walikwamisha mradi wa ujenzi wa Daraja mto Litete lililopo katika kijiji cha Mkongo Gulioni wilayani Namtumbo liweze kufunguliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Charles Fransis Kabeho.

Akitoa maelezo ya kutofungua mradi huo kwa mkuu wa wilaya ya Namtumbo kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge kitaifa alisema kuwa hawezi kufungua mradi huo kutokana na kumkosa mtu sahihi wa kumwuliza maswali ili aweze kujiridhisha na ujenzi wa daraja hilo .

Bwana Kabeho aliongeza kwa kumwambia mkuu wa wilaya kuwa haiwezekani kufungua mradi wakati wahusika waliojenga Mradi hawapo katika mradi wao na kina nipa wasiwasi kwa nini hawajafika katika mradi wao na mimi kukosa kujiridhisha kwa maswali ambayo ningeweza kuwauliza alisema Kabeho.

Pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa Daraja hilo alitaka kuwauliza maswali wahusika wa mradi TANROAD ambao hawakujitokeza kuhudhuria ufunguzi wa daraja hilo na kuwashangaza wananchi wa kijiji cha Mkongo ambao walitegemea daraja hilo liweze kufunguliwa.

Awali akisoma taarifa ya daraja hilo kaimu Ofisa mipango wa Halmashuri ya wilaya ya Namtumbo bwana Hancy Ngogo alisema kuwa Daraja hilo mpaka kukamilika kwake limegharimu shilingi 64,682,172 .na alipotakiwa kueleza kuhusu ukubwa wa eneo la kujenga daraja hilo alionesha kutojua na kumweleza kiongozi wa mbio za mwenge kuwa taarifa hiyo ilitakiwa isomwe na waliojenga daraja hilo na baada ya kuona hawapo katika eneo hili nimeamua niisome kwa kuwa taarifa yao walishaiwasilisha katika ofisi ya mkuu wa wilaya Namtumbo.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckness Adrian Amlima alimwambia mkimbiza mwenge kitaifa kuwa ameshangazwa na wakala wa barabara TANROAD kutofika kwenye mradi wao kwani mawasiliano na taarifa zote za mradi wao kuwa moja ya miradi ya kufunguliwa na mwenge wa uhuru walikuwa nayo alisema mkuu wa wilaya huyo.

Mwenge wa uhuru wilayani Namtumbo ulipita katika vijiji 19 kata 9 na Tarafa 2 ambapo wanachi wa wilaya ya Namtumbo waliweza kushiriki katika kuushangilia kila ulipokuwa ukipita na kufanya kazi ya kukagua kuzindua na kutembelea miradi mbalimbali wilayani humo.

No comments: